Friday 20 March 2015

Zitto kuwaaga wabunge leo na kuhamia ACT

Pamoja na mpango wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuliaga Bunge kukwama jana, Chama cha ACT- Tanzania kimetangaza kukamilisha maandalizi ya kumpokea mwanasiasa huyo kuanzia leo.
Mbunge huyo alipanga kuliaga bunge na alisema amekwishapata ruksa ya Spika kuwa angesimama bungeni kuwaaga wabunge na wanachama wa Chadema baada ya chama hicho kumtimua uanachama wake hivi karibuni, lakini ghafla mpango huo uliyeyuka kwa kile kilichoelezwa kuwa Spika amemkatalia.
Tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka mmoja uliopita, Zitto amekuwa akihusishwa kukianzisha, hivyo kitendo chake cha kujiunga nacho kitahitimisha mjadala wa muda mrefu wa mashabiki wake waliokuwa wakihoji wapi ataelekea baada ya kung’olewa Chadema.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa ACT, Samsom Mgamba aliangua kicheko na bila kuuma maneno alisema: “Hahahaa... tutampokea kuanzia kesho (leo) na maandalizi yamekamilika.”
Alipotakiwa kueleza wapi mapokezi hayo yatafanyika alisema: “Hilo mbona liko wazi, yatafanyikia makoa makuu yetu (yapo Makumbusho, Dar es Salaam) lakini kwa taarifa zaidi tutawajuza.”
Zitto anaingia ACT ikiwa ni siku tisa kabla ya chama hicho kufanya uchaguzi wake mkuu, huku akitajwa kuwa ameandaliwa kushika wadhifa wa mwenyekiti kuendeleza harakati zake za siasa.
Hivi karibuni, chama hicho kilimvua uongozi aliyekuwa mwenyekiti mwanzilishi, Lucas Limbu kutokana na mgogoro uliokuwapo baina ya viongozi na kufanya nafasi hiyo kubaki wazi.
Tayari washirika wa Zitto waliohusishwa naye kuandika waraka wa mapinduzi ndani ya Chadema na baadaye kufukuzwa uanachama, Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo wametua ndani ya chama hicho kipya.
Chama hicho ambacho kinaendelea na uchaguzi katika ngazi ya mikoa kikibakiza Mkoa wa Geita unaofanya uchaguzi wake kesho. Kitaanza vikao vyake vya kitaifa Machi 27 na kuhitimisha kwa mkutano mkuu Machi 29.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mwigamba alisema: “Maandalizi yanakwenda vizuri na hakuna shaka utafanikiwa kwa kiasi kikubwa na tunawaomba Watanzania watuunge mkono.”
Tangu juzi, Zitto alitarajiwa kuliaga Bunge lakini hakufanya hivyo kwa kilichoelezwa kuwa aliitwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda na kupewa ushauri kuwa afanye hivyo jana jioni.
Jana asubuhi mbunge huyo hakuingika katika kikao cha Bunge lakini alionekana katika viwanja vya Bunge akiwa amevaa shati la drafti na suruali ya kaki akizungumza na rafiki yake wa karibu, Deo Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kupitia CCM.

Katika kipindi cha jioni, mbunge huyo aliingia katika viwanja vya Bunge saa 11:10 jioni akiwa amebeba mafaili huku akizungumza na simu na baadaye kutaniana na waandishi wa habari waliokuwa nje ya ukumbi wa Bunge.
Mbunge huyo aliyekuwa amevalia shati nyeupe na suruali nyeupe kabla ya kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge alizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya.
Akwama kuliaga Bunge
Habari zilizopatikana bungeni jana jioni zilieleza kuwa Spika Bunge, Makinda alimpiga ‘stop’ mbunge huyo kuaga bungeni bila kuweka wazi sababu za kufanya hivyo.
Mbunge huyo juzi alitinga bungeni kwa mara ya kwanza tangu Chadema kitangaze kumvua uanachama na kufanya kikao cha siri na Makinda kwa zaidi ya saa moja na baadaye kulieleza gazeti hili kuwa angezungumzia hatima ya ubunge wake jana.
Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na watu wake wa karibu naye zilieleza kuwa licha ya Makinda kumshauri mbunge huyo kuaga bungeni, jana aligoma kumpa ruhusa hiyo.
“Kazuiwa kuaga sijui kwa nini, ila kwa jinsi tunavyoona Makinda ni kama anahitaji Zitto aendelee kubaki bungeni. Ngoja tusubiri kwanza tuone nini kitatokea,” zilieleza habari hizo.
Alipoulizwa juu ya taarifa hizo Zitto, alisema: “Hata mimi nasikia hivyo ila sina hakika sana. Ngoja niende ndani nitajua zaidi, mimi nataka kuaga, can’t stay any more (siwezi kuendelea kubaki).
Alipoingia katika ukumbi wa Bunge, Zitto alionekana akizungumza na baadhi ya wabunge wa upinzani na baadaye wakati mjadala wa muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji ukiendelea, alitoka nje na watu wa karibu wa mbunge huyo walisema alikuwa akishinikiza kuaga kama alivyopanga.
Spika Makinda hakupatikana kuzungumzia sababu za kukataa kumruhusu mbunge huyo na Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alipoulizwa juu ya suala hilo alisema hajui chochote.
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage alisema mbunge huyo kisheria hana mamlaka ya kushinikiza kuaga bungeni na kumtaka asubiri mamlaka husika zifanye kazi hiyo, akimaanisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kulijulisha Bunge kuwa Zitto si mbunge tena baada ya kupata barua ya Chadema.
Chadema ilitangaza kumvua Zitto uanachama siku 10 zilizopita, saa chache baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kutupa shauri lake alilofungua akitaka chombo hicho cha sheria kimlazimishe katibu mkuu wa chama hicho kumpa nyaraka za vikao vya Kamati Kuu vilivyomvua nyadhifa zote.Awali, Mahakama hiyo ilitoa amri ya muda ya kuzuia Chadema kumjadili na amedumu kwenye nafasi ya ubunge chini ya zuio hilo kwa takribani mwaka mmoja.

No comments: