Thursday 23 April 2015

Ajali nyingine shinyanga yaua 10 na 50 kujeruhiwa

Polisi wakiwa katika eneo la Ajali
Jinamizi la ajali za barabarani zikihusisha mabasi zimeendelea kugharimu maisha ya Watanzania baada ya jana watu 10 kupoteza maisha na wengine 50 kujeruhiwa vibaya wakati basi la Unique Express lililokuwa likitokea Mwanza kuelekea Tabora kugongana uso kwa uso na lori la Coca-Cola lililokuwa likitokea Tinde kuelekea Shinyanga.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 8.45 mchana katika Kijiji cha Ibingo, Kata ya Samuye, Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi uliosababisha dereva wake kushindwa kulikwepa lori hilo lililokuwa katikati ya barabara.
Alisema watu tisa walifariki dunia papohapo na mmoja alifia katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga akipatiwa matibabu.
Kamanda Kamugisha alisema dereva wa lori anashikiliwa na polisi mwenzake wa basi hali yake ni mbaya na amelazwa hospitali.
Alisema wengi waliofariki dunia walikuwa wamekandamizwa na vyuma hali iliyowalazimu kuomba msaada wa winchi kuliinua basi hilo na kuwatoa.
Kamanda Kamugisha aliwataka wananchi na abiria kutoa taarifa pindi wanapoona madereva wakiendesha mwendo ambao unaweza kuhatarisha maisha yao.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo akiwamo Diwani wa Kata ya Samuye, Amos Shija walisema walishtushwa na kishindo cha kugongana kilichofuatiwa na kelele na vilio vya abiria.
Shuhuda, John Bundala aliitaka Serikali kuendelea kuwachukulia hatua kali madereva ambao hawazingatii sheria za usalama barabarani na kupoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia na wengine kupata ulemavu.

No comments: