Sunday 26 April 2015

Dk. Augusine adai anashawishiwa ili agombe Urais

Balozi wa zamani wa Tanzania kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN), Dk Augustine Mahiga amesema anafuatwa na makundi ya watu wanaomshawishi achukue fomu kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM, lakini hajatoa jibu.
Balozi Mahiga anaingia kwenye orodha ya watu ambao wamejitangaza au wanatajwa kuwania nafasi hiyo ya juu kwenye siasa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utakaochagua Serikali ya Awamu ya Tano.
Tayari makada 21 wa chama chake wanatajwa kuwamo kwenye kinyang’anyiro hicho cha kumrithi Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake wa miaka 10 baada ya kuongoza nchi kwa vipindi viwili, ambavyo ndio kikomo kwa mujibu wa Katiba.
Tayari makada 21 wa chama chake wanatajwa kuwamo kwenye kinyang’anyiro hicho cha kumrithi Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake wa miaka 10 baada ya kuongoza nchi kwa vipindi viwili, ambavyo ndio kikomo kwa mujibu wa Katiba.
Dk Mahiga,(pichani) ambaye pia alikuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UN nchini Somalia, alisema makundi hayo yalianza kumfuata baada ya Rais Kikwete kutangaza kwenye sherehe za maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika Songea kuwa kama wanachama wanaona kuna mtu anafaa kugombea urais na hajajitokeza, wamfuate na kumshauri achukue fomu.
“Nimepata makundi ya watu na mtu mmoja mmoja wakinishauri  nichukue fomu ya kuwania urais baada ya Rais Kikwete kutoa kauli kule Songea mkoani Ruvuma, lakini bado sijakubali wala kukataa ushawishi huo,” alisema mwanadiplomasia huyo alipoongea na Mwananchi mara baada ya kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Tosamaganga iliyopo Iringa.
Lakini akaongeza kuwa kushawishiwa kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo nyeti kwa Taifa, ni jambo moja, lakini kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ni jambo jingine akisema kuwa CCM ina mchakato na masharti ambayo ni lazima yatimizwe.
Hata hivyo, Dk Mahiga hakusita kumwaga sera zake iwapo atajitosa kuwania nafasi hiyo na kuchaguliwa kuongoza nchi.
“Nitaimarisha demokrasia, kuongeza uwajibikaji, kuimarisha maadili, kuboresha mwelekeo wa uchumi, kilimo, kuimarisha reli na kupambana na rushwa,” alisema balozi huyo ambaye ni mhitimu wa shahada ya umahiri ya sanaa.
Kuhusu sifa za mgombea urais, Dk Mahiga alisema ni vema Rais ajaye akawa na sifa zinazoenea na kuelezeka ili kuweza kupokea kijiti kutoka kwa Rais Kikwete wa sasa na kulipeleka mbele Taifa katika kipindi cha miaka mitano mingine. Alisema Rais ajaye anatakiwa kuwa kiongozi wa watu, aliye tayari kujifunza, kuchukua uamuzi mgumu, uwezo wa kutawala hasira na kuwa na marafiki.
Pia alisema anatakiwa kuwa na uwezo wa kutatua changamoto ambazo hazijaweza kutatuliwa kwa sasa ikiwemo ya ugaidi.
Nyingine ni kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja, muadilifu na mwenye mtazamo wa mbali kwa Watanzania na Taifa, kuhimili mfadhaiko, awe mchapakazi, subira ya kupima mambo na kuwa juu ya yote kama hasira, wivu na fitina.

Akizungumzia hali ilivyo kwa sasa katika mbio za kuelekea Ikulu, Dk Mahiga alisema kumekuwepo na hali ya wanaowania nafasi ya urais kutumia fedha na kuonya kuwa suala hilo linaweza kulifikisha Taifa mahali pabaya kwa kumpata mtu asiyestahili.
Dk Mahiga aliwahi kuongea na Mwananchi wakati wa mchakato wa Katiba akielezea msimamo wake kuhusu muundo wa Muungano.
Dk Mahiga alisema wakati huo kuwa suala la muundo wa serikali tatu kwenye Muungano limekuja wakati muafaka kwa kuwa umekuwa ukilalamikiwa na wananchi wa pande zote kwa muda mrefu na kwamba Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Kamati ya Mabadiliko iliyokuwea chini ya Jaji Joseph warioba ilikuwa na jibu la kero za Muungano.
Dk. Mahiga pia amepata kuwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Liberia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati akifanya kazi ya kuongoza shughuli za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la UN (UNHCR).
Akiwa balozi wa kudumu UN, Balozi Mahiga alisifika kwa kurejesha heshima ya heshima ya nchi kiasi cha kuwa mojawapo ya zilizounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika kipindi cha kati ya mwaka 1980 hadi mwaka 1983, Mahiga alikuwa kaimu mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, nafasi ambayo ilimpa fursa ya kuifahamu Tanzania nje na ndani.
Dk Mahiga alizaliwa Agosti 28, 1945, ameoa na ana watoto watatu.
Alihitimu shahada yake ya sanaa mwaka 1971 kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na shahada yake ya uzamili aliipata Chuo Kikuu cha Toronto. Alipata shahada yake ya uzamivu katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa kwenye Chuo Kikuu cha U of T mwaka 1975.

No comments: