Friday 21 November 2014

Sakata la Escrow laibua mengi Bungeni

WAKATI Bunge likijiandaa kusomewa ripoti ya uchunguzi wa Akaunti ya Escrow bungeni Mjini Dodoma, ripoti hiyo imezidi kuwapasua vichwa wabunge baadhi yao wakienda mbali zaidi na kudai wamebaini ukweli wa fedha hizo.
Hatua hiyo inatokana na taarifa zinazodai malipo ambayo yanalalamikiwa kufanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia Kampuni ya Independet Power Supply Limited (IPTL), yalikuwa halali si ya fedha za umma.

Taarifa zaidi kutoka kwa baadhi ya wabunge wanaodai kupata yaliyomo kwenye ripoti hiyo kuhusiana na malipo hayo, zinasema wabunge wengi wamefahamu ukweli na kinachofanyika ndani ya Bunge ni kupotosha ukweli kwa maslahi ya wachache.
 mmoja wa wabunge hao ambaye hakutaka jina lake litajwe , alisema kinachoweza kufanyika sasa ndani ya Bunge ni uonevu kwa kuwa BoT ililipa malipo halali kwa IPTL na taarifa ziko wazi.

“Nimeipata ripoti ya CAG na taarifa zingine, nimezisoma kwa umakini mkubwa na kubaini kilichopo ni vita ya madaraka, kuna wakati tunafuatwa na watu ili tuwawajibishe viongozi hasa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,” alisema.

Alidai kuna baadhi ya wabunge ambao wamejiridhisha kuwa malipo hayo yalilipwa ili kutekeleza makubaliano kati ya IPTL na Serikali ambapo BoT ilichaguliwa kama wakala wa kutunza fedha.

Alisema hali hiyo ilitokana na uwepo wa mgogoro wa kimaslahi kati ya wabia wa IPTL ambao ni kampuni ya VIP (ilikuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa) inayomilikiwa na James Rugemalila na kampuni ya Mechmar kutoka Malaysia (ilikuwa inamiliki asilimia 70).

Mbunge huyo alisema taarifa zinaonyesha kwamba Mahakama Kuu iliamua pande zote mbili VIP na Mechmar zisaini hati ya makubaliano (MoU) juu ya kutunza fedha za malipo ya kila mwezi ya umeme, ambayo IPTL inauzia TANESCO.

Aliongeza kuwa, nyaraka zinaonesha mahakama ilielekeza malipo hayo yahifadhiwe katika akaunti maalumu hadi mgogoro utakapoamriwa kati ya wabia hao ambao walikubaliana kufungua akaunti ya pamoja BoT na akaunti hiyo kuitwa Escrow.

“Ukitazama kwa umakini, kinachofanywa ni kumuonea Pinda kwa sababu ya upole wake, kuna watu wanaamini atagombea urais hivyo wanataka kumharibia,” alisema mbunge mmoja kutoka mkoani Morogoro.

Mbunge mwingine kutoka Dodoma, alisema ukisoma taarifa za Escrow, zinaonesha wazi kuwa BoT ilikuwa wakala wa kutunza fedha hizo ambapo TANESCO na Serikali walisaini hati kama sehemu ya wabia wakiwa walipaji wa umeme kwa IPTL.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, ambazo  zinaonesha makubaliano hayo yalifikiwa Julai 5, 2006 na kila upande uliwakilishwa na wahusika, kutia saini ambapo kwa upande wa Serikali alisaini aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara wakati huo, Arthur Mwakapugi.

Taarifa hiyo ilionyesha kwa upande wa IPTL alisaini aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Datuk Baharuden Majid na upande wa BoT, alisaini aliyekuwa Gavana Mkuu, marehemu Daudi Balali kama wakala wa kuhifadhi fedha hizo.

Kusainiwa kwa makubaliano hayo ikiwa ni maelekezo ya mahakama, ilielezwa kuwa mgogoro utakapoisha kati ya wabia, BoT itatoa fedha zote ilizokuwa inazihifadhi katika akaunti hiyo kwa mujibu wa hati husika ya makubaliano kwa ajili ya malipo ya uuzaji wa umeme kwa TANESCO.

Kwa upande wake, mbunge mwingine kutoka mkoani Tabora, ambaye alikuwa na mbunge mwenzake kutoka Mkoa wa Pwani, alisema ukilitazama Bunge kwa umakini limeanza kugawanyika.

“Kuna wafanyabiashara waliokosa vitalu vya gesi wamekuja na yao ndani ya Bunge ili wamwajibishe Waziri wa Nishati na madini kwa maslahi yao na wengine walikuwa wanatoa ushauri wa kisheria katika suala hili,” alisema mbunge huyo.

Aliongeza kuwa, Serikali inapaswa kuwa makini na kuhakikisha inasimama imara kuelezwa ukweli wa jambo hilo kwani anaamini kinachofanyika ndani ya bunge ni hasira za watu.

No comments: