Sunday 4 June 2017

NAMBA YA SIMU YA BEN SAANANE YATUMIKA WHATSAPP

Wakati hofu ikiwa imetenda baada ya jumla ya miezi minane kupita tangu alipopotea kwenye mazingira ya kutatanisha, matumaini mapya yameanza kuibuka baada ya simu yake kuonekana imetumika kwenye mitandao ya kijamii.
Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alitoweka mwaka jana na kumekuwapo na hisia nyingi kuwa huenda alishafariki dunia kutokana na kuwa, hakuna yeyote anayefahamu alipo kijana huyo aliyekuwa akichipukia katika siasa nchini Tanzania. 
Kwa mujibu wa gazeti la TanzaniaDaima, simu ya Ben jana alitumika majira ya saa tatu asubuhi ambapo ilionekana namba yake ikijitoa kwenye makundi ya WhatsApp. Imeelezwa kuwa namba yake ilijitoa kwenye makundi mengi huku ikiwaacha na mshangao mkubwa wajumbe (members) wa makundi hayo. Hofu ya kuwa kijana huyo hayupo hai ilichangiwa na jibu alilolitoa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa bungeni ambapo alisema, “familia ya mtajwa (Ben Saanane) aliyetangulia mbele za haki au vinginevyo, uchunguzi wa suala lake utakapokamilika, taarifa rasmi itatolewa.” Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe Aprili 20 mwaka huu aliyetaka kujua kwanini serikali imekuwa kimya sana kwenye suala la kupotea kwa msaidizi wake.