Monday, 24 February 2014

J k; Misri tuko nyuma yenu

RAIS Jakaya Kikwete, ameihakikishia nchi ya Misri kuwa Tanzania itaunga mkono jitihada za nchi hiyo kurejeshewa uanachama wake katika Umoja wa Afrika (AU), baada ya nchi hiyo kufanya Uchaguzi Mkuu wa kidemokrasia Aprili mwaka huu.
Alisema kwa mujibu wa makubaliano ya uanzishwaji wa AU, itakuwa vigumu kwa nchi hiyo kurejeshewa uanachama wake katika mazingira ya sasa.
Rais Kikwete aliyasema hayo jijini Dar es Salaam juzi baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Bw. Nabil Fahmy ambaye aliwasilisha ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa muda wa Misri, Adly Mansour.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Fahmy aliiomba Tanzania kuunga mkono jitihada za Misri kurejeshewa uanachama wake AU ambao umesitishwa baada ya kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa nchi hiyo aliyekuwa amechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, Bw. Mohamed Morsi mwaka 2013.
Akitoa msimamo wa Tanzania kuhusu matumizi ya maji ya Mto Nile, Rais Kikwete alisema nchi zote ambazo mto huo umepita kwa namna moja ama nyingine, zina haki sawa ya kutumia maji yake kwa maendeleo ya nchi hizo.
"Tunaamini nchi zote ambazo mto huu unapita zina haki ya kutumia maji, haki ya aina hii ndiyo inayotumika hata Tanzania kulingana na matumizi ya maji kwenye mito mbalimbali ndani ya nchi yetu," alisisitiza Rais Kikwete.
Mapema Bw. Fahmy alimwambia Rais Kikwete kuhusu umuhimu wa maji ya mto huo kwa Misri akisema kuwa; "Sisi katika Misri, hupata mvua siku tatu kwa wastani katika mwaka.
"Maji yote tunayotumia yanatokana na Mto Nile hivyo unaweza kuelewa umuhimu wa mto huo kwa uhaki na ustawi wa nchi yetu," alisema.
Rais Kikwete aliishukuru Serikali ya Misri kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania na kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa misaada katika sekta mbalimbali na hasa za maji na afya.
Bw. Fahmy alikuwa nchini kwa ziara ya siku tatu ambapo jana amerejea nchini kwao.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete juzi aliongoza harambee ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya matibabu kwa ajili ya wodi ya watoto katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar es Salaam.
Katika harambee hiyo, zaidi ya sh. milioni 602 zilipatikana wakati lengo lilikuwa kukusanya sh. bilioni moja. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wastaafu akiwemo Rais wa Pili wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Tatu za Tanzania, Mzee Benjamin Mkapa kama walezi wa Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania (PAT).
Katika halfa hiyo, Ikulu ya Rais Kikwete imetoa mchango wa kununua mashine iitwayo Infant Radiant Warmer yenye thamani ya dola za Marekani 15,300.
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA ) inayoongozwa na Mama Salma Kikwete imechangia ununuzi wa mashine iitwayo Compressor Nebulizer ambayo gharama yake ni dola za Marekani 12,000.

Hali yaendelea kuwa mbaya Africa ya kati

KUNDI la wanamgambo lenye nguvu kubwa huko Jamhuri ya Afrika Kati limesema litasalimisha silaha zake ikiwa tu, mahasimu wao wakuu wa kundi la Seleka linaloundwa na wapiganaji wengi wa Kiislamu litaweka silaha zao chini.
Kwa mujibu wa DW, kauli hiyo inaliweka taifa hilo katika muendelezo wa mgogoro nchini humo huku kundi la wapiganaji la anti-balaka lililoundwa mwaka jana likiwa na shabaha ya kuilinda jamii ya Kikristo ambayo imekuwa ikilengwa na waasi wa Seleka waliomuondoa madarakani rais wa taifa hilo mwezi Machi.
Tangu wakati huo kumekuwa na mauaji ya kulipiziana visasi licha ya kuwepo kwa maelfu ya wanajeshi wa kulinda amani wa kigeni nchini humo.
Msemaji wa anti-balaka, Sebastien Wenezou amesema wataweka silaha zao chini kwa masharti kwamba kundi la Seleka kuanza kufanya hivyo kwanza huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kimoon akionya kutokea mauaji ya kuangamiza jamii kwa misingi ya kidini.

simba ya pigishwa guu pande guu sawa na wanajeshiSimba yapigishwa kwata na maafande wa JKT Ruvu
Monday, February 24 2014, 8 : 41

TIMU ya Simba jana ilikiona cha mtema kuni baada ya kuzabwa mabao 3-2 na timu ya maafande JKT Ruvu katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Bao la kwanza la JKT Ruvu lilipatikana katika dakika ya 13 lililofungwa na Hussein Bunu baada ya mabeki wa Simba kujichanganya.
Dakika ya 18 nusura Amis Tambwe aipatie bao Simba baada ya kuachia shuti kali lililopaa juu ya lango JKT Ruvu.
Timu ya Simba ilifanya mabadiliko dakika ya 22 kwa kumtoa Said Ndemna na nafasi yake kuchukuliwa na Ali Badru kwa ajili ya kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
JKT Ruvu iliandika bao lake la pili katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza lililofungwa na Emmanuel Swita kwa mkwaju wa penalti iliyosababishwa na Henry Joseph baada ya kumfanyia madhambi mchezaji wa JKT Ruvu katika eneo la hatari.
Kipindi cha pili JKT iliingia kwa nguvu na kufanikiwa kupata bao la tatu kupitia kwa Bunu tena baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Damas Makwaya, dakika ya 57 nusra Amis Tambwe aipatie Simba bao.
Dakika ya 71 Simba ilifanya mabadiliko tena kwa kumtoa nje Badru na nafasi yake kuchukuliwa na Issa Rashid 'Baba Ubaya', Awadh Juma aliikosesha Simba bao la wazi akiwa ndani ya 18 akiwa yeye na mlinda mlango, lakini alishindwa kufunga.
Simba ilipata bao la kwanza katika dakika ya 63 ya mchezo kwa mkwaju wa penalti uliokwamishwa wavuni na Tambwe baada ya Amri Kiemba kuchezewa rafu katika eneo hatari.
Dakika ya 82 Simba ilipata bao kupitia kwa mchezaji Amis Tambwe baada ya kupoke pasi safi kutoka kwa Uhuru Selemani.
Wakati huo huo, mchezo kati ya Azam FC na Prison ya Mbeya ulimalizika kwa suluhu kwa kufungana mabao 2-2 huku kila timu ikionesha kandanda safi ya kuvutia.

Tuesday, 18 February 2014

Onyo la uwezekano wa shambulizi la kigaidi Uganda

Ubalozi wa Marekani Kampala wasema kuna ishara kwamba jumba la makumbusho la kitaifa ni mojawapo ya majengo yanayolengwa na magaidi

Ubalozi wa Marekani nchini Uganda umeonya juu ya uwezekano wa kutokea shambulizi la kigaidi katika mji mkuu wa Kampala.

Katika ujumbe uliotolewa Jumatatu jioni, ubalozi huo ulisema umepata habari kwamba huenda kundi la washambuliaji likiwa tayari kuvamia malengo kadhaa mjini Kampala mwezi Februari na Machi.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa kuna ishara kwamba jumba la makumbusho la kitaifa ni mojawapo ya majengo yanayolengwa. Lakini serikali ya Uganda haijatoa tamko la haraka juu ya onyo hilo.

Ujumbe huo haujawaonya Wamarekani kuondoka Kampala lakini umewatahadharisha kuepuka jumba la makumbusho na maeneo mengine yenye watu wengi.
Kundi la al-Shabab kutoka Somalia lilifanya shambulizi la kigaidi huko Kampala Julai 2010 na kuuwa watu 70.

Rubani aliyeteka ndege ya Ethiopia ajisalimisha.

Maafisa wa Polisi wakisaidia abiria kutoka kwenye ndege hiyo ya shirika la ndege la Ethiopia iliyokuwa imetekwa.


Maafisa wa Polisi wakisaidia abiria kutoka kwenye ndege hiyo ya shirika la ndege la Ethiopia iliyokuwa imetekwa
Rubani msaidizi wa ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia iliyokuwa ikielekea Roma, Italia aliteka ndege hiyo Jumatatu na kutuia salama Geneva ambako alikamatwa.

Maafisa wanasema rubani huyo ambaye jina lake halikutajwa ana umri wa miaka thelathini. Alichukua udhibiti wa ndege hiyo ya 767 kwa kufunga mlango wa rubani baada ya rubani kutoka kuelekea kujisaidia.

Maafisa wa Uswisi wanasema mara ndege hiyo ilipotua Geneva rubani huyo msaidizi alitoka kwenye ndege hiyo kwa kutumia kamba na kujisalimisha kwa maafisa na kusema kwamba alikuwa ni ‘haramia’ anayetafuta hifadhi ya kisiasa kwa sababu alikuwa akiogopa kuteswa nyumbani .

Chanzo cha mateso hayo hakijafahamika mara moja.Ndege hiyo ilitokea mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa na ilikuwa imebeba abiria 202.

Mcheki Nikki Minaj akiwa hana make up wala wigi

Nikki Minaj aamua kuonyesha uhalisia wa uzuri wake kupitia picha zake za instagram akiwa hana make up, wigi wala nguo zake tunazomuona nazo kila wakati katika picha zake. Nikki anaonekana akiwa na nguo za kawaida kabisa zinzomfanya aonekane mzuri hatari, ngozi nyororo isiyo na make up kama tulivyomzoea..
angalia picha zaidi

Maajabu ya ‘Shimo la Mungu’ Newala

Katika Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara lipo shimo la ajabu lijulikanalo kama ‘Shimo la Mungu’ lililochukua robo tatu ya ukubwa wa wilaya hiyo.

Shimo hili linalotajwa kuwa moja ya vivutio mkoani Mtwara limesheheni hifadhi za misitu, mito, mabonde, mawe ambayo yanapendeza kwa macho pia kipo kisima cha maji Newala.

Jambo hili linawasumbua wale wanaojua historia yake ni taarifa za kutupwa kwa watoto, kupotea kwa watu wale wanaojaribu kuingia bila ruhusu, wabishi wasioamini tambiko na mambo mengine kadhaa ambayo hata hivyo ni vigumu kuyathibitisha.

Ni shimo la asili ambalo limekuwapo miaka mingi, na wenyeji wa Mji wa Newala wanaliita ‘Shimo la Mungu’ kutokana na kile wanachoeleza kuwa ni maajabu ambayo hutokea yakianzia katika shimo hilo.

Miongoni mwa maajabu hayo ni yale ambayo hutokea nyakati za asubuhi kipindi cha masika ambapo upepo mkali sana huvuma kutoka lilipo shimo hilo.

Wanasema wakati mwingine hutokea moshi mzito ambao husambaa na kuufunika Mji wa Newala na kusababisha giza nene katika makazi ya watu kiasi cha watu kushindwa kuonana kwa kati ya dakika tatu na dakika saba.

Mkazi wa Newala, Sophia Saidi (90) anasema: “Sisi tumezaliwa tumelikuta, kutokana na shimo hilo kutotengenezwa na mtu yeyote ndio maana tukaliita ‘Shimo la Mungu”.

Bibi Sophia kama anavyojulikana na wengine anasema anaongeza: “Sehemu hiyo huwa panatokea miujiza kama hiyo ambayo inaleta upepo mkali, mara giza hata sisi hatujuwi ni nani ambaye ana sababisha kuwe na giza kutoka sehemu ya shimo hilo hadi sehemu ya makazi ya watu”.

Kutokana na umaarufu wake, eneo hilo limekuwa kivutio kikubwa cha watu ambao hufika kwa ajili ya kufanya matambiko ya jadi, ikiwa ni sehemu ya mila na desturi za wakazi wa Newala na wilaya nyingine jirani.

Maimuna Pinda (55) ambaye pia ni mwenyeji wa eneo hilo anasema hata waganga wa jadi kuingia na kutoka ndani ya ‘Shimo la Mungu’ kwa ajili ya kuchukua dawa mbalimbali za miti shamba ambazo hutumika kutibia magonjwa kadhaa. Pinda anasema kabla ya mtu hajaingia ndani ya shimo hilo ili kutalii au kuchukua dawa, lazima afanywe tambiko.

Pembezoni mwa shimo hilo huota uyoga ambao ni kitoweo kwa wakazi wanaolizunguka, lakini kwa maelezo ya wenyeji uchumaji huo huwa ni hatari kwani mara kadhaa watu wamepoteza maisha kutokana na kupatwa na kizunguzungu kisha kutumbukia kwenye shimo.
Kivutio kingine kuhusu ‘Shimo la Mungu’ ni madai ambayo yamekuwa yakitolewa kwamba ndege haziwezi kuruka juu yake kutokana na kuwamo kwa mvutano wa asili hivyo kuwa kikwazo cha usafiri wa anga.

Mkazi mwnigine na Newala, Said Omary (54) anasema: “Newala tuliwahi kuwa na uwanja wa ndege zamani ambao ulikuwa unajulikana kama Uwanja wa Nangwanda na ulikuwa karibu na makazi ya watu”.

Aliongeza: “Wakati zilipokuwa zikiruka, zilikuwa zikielekea sehemu ya shimo hilo na kuna habari kwamba ndege mbili zimewahi kuangukia kwenye shimo hilo ndio maana wakaamua kuhamisha kiwanja hicho katika kijiji cha Mtangalanga kati ya Makonga eneo lililopo mbali na makazi ya watu.”

Hata hivyo mmoja wa waongoza ndege mkoani Mtwara, Emmanuel Wanje alisema hakuna kumbukumbu za matukio hayo na kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yanapotokea kwa haraka husababisha ndege kushindwa kuruka kwenda juu kutokana na mvutano uliyopo kwenye ardhi.

“Sababu ambazo zinazofanya ndege kushindwa kuruka angani ziko mbili ni (winds shear pamoja na Ant- Mosipheric Pressure) upepo unazunguka kwenda juu ukajikusanya kama kibunga husababisha ndege kuwa katika hali isiyo ya kawaida husababisha kukosa mweleko na hatimaye kuanguka,” alisema Wanje.

Wanje alisema wakati ndege zinapokuwa katika harakati za kutua hutegemea Ant-Mosipherec Pressure na kwamba wakati huo ndege hutumia mafuta mengi, kama ilivyo wakati wa kupaa.

Hazina ya Utamaduni

Wakazi wa Newala wanalitizama ‘Shimo la Mungu’ kama hazina ya mila, desturi na utamaduni wa wakazi wa Mikoa ya Kusini inayojumuisha makabila makubwa matatu; Wayao, Wamakua na Wamakonde.

Katika shimo hilo ndiko wakazi hawa wanakopata miti kwa ajili ya kudumisha utamaduni wao wa kuchonga vinyago vya mapambo ya vyombo mbalimbali, ambavyo husambazwa ndani na nje ya nchi, asili yake ikiwa ni mkoani Mtwara.

Mkazi wa Newala Rashidi Ramadhani anasema: “Sisi watu wa Kusini tunapenda sana utamaduni wetu na bado tunauendeleza mfano kila mwaka tunafanya maonesho ya michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ngoma za asili ambazo huashilia kuendelea kudumisha mila na desturi za mkoa wetu.”

Kutokana na umuhimu huyo wananchi wa Newala wanasema Serikali inapaswa kuweka ulinzi kwenye eneo hilo ili kutunza uoto wa asili kwani watu wasiofahamu umuhimu wake hukata miti ovyo pembezoni na ndani ya shimo hilo kwa matumizi mbalimbali hasa kuchoma mkaa.

“Tungependa misitu ibaki kama ilivyo ili itumike kwa ajili ya maombi kwa wenyeji na wageni. Watu inabidi waheshimu sehemu hiyo ambayo inaheshimiwa na kila mtu, wageni kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huu huja kufanya maombi hivyo watu waache kwenda hovyo kwenye shimo hilo kutokana na majabu yanayojitokeza tokea enzi na enzi,” alisema Pinda.
Ofisa Utamaduni wa Wilaya ya Newala, Pontian Mutegeya anasema shimo hilo lipo katika hifadhi ya Mlima Makonde na kwamba muda si mrefu wanategemea liwe ni eneo la hifadhi kwani watu mbalimbali wamekuwa wakifika kwa ajili ya kufanya tafiti.

“Sasa Idara ya Ardhi imepima viwanja vinne karibu na shimo, tunarajia kujenga hoteli za kitalii ambazo zitakuwa ni kivutio kwa wageni kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania,”anasema Mutegeya.

Alisema elimu ikitolewa ipasavyo, ‘Shimo la Mungu’ linaweza kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa ndani na nje ya nchi, kwani limesheheni hazina ya hisotria ya mambo ya kale hasa kwa miko ya Kusini.

Maliasili Mtwara

Mkoa wa Mtwara unajivunia maeneo mengi kuwa ya uoto wa asili na sehemu kubwa ya maeneo hayo bado yanatunzwa na wazee wanaojua asili yake.

Ofisa Wanyamapori wa mkoa huo, Richard Katondo anasema misitu inachukua asilimia 42.4 ya mkoa mzima na kati ya hiyo asilimia 93.7 inahifadhiwa na Serikali Kuu.

Katondo anasema zinafanywa jitihada za kutangaza vivutio vilivyopo mkoani humo likiwamo ‘Shimo la Mungu’ pamoja maajabu mengine katika Wilaya za Masasi na Nanyumbu.

“Nasema hivyo kwani hifadhi hizo bado hazijajengewa uwezo wa kuingiza pato ndani ya mkoa ila ni hifadhi ambazo zikiangaliwa na kuandaliwa vizuri zinaweza kuokoa wilaya husika na mkoa kwa ujumla kwa kuingiza mapatao makubwa na fedha nyingi za kigeni,” alisema Katondo.

Diamondi ajiandaa kutoa ngoma na Dbanji

Mkali wa Bongo Fleva Hapa Bongo kwa sasa ambaye anafanya Vizuri na Track ya Number One RMX akiwa amemshirikisha Davido kutoka Nigeria...

Airtel yazindua mpya ya kisasa zaidi

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel imetangaza rasmi huduma ya kisasa ya kifedha kupitia huduma ya Airtel Money.

Huduma hiyo mpya ya kibunifu itatoa uzoefu tofauti wa huduma za fedha kwa wateja wake.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Airtel, Sunil Colaso, alisema huduma hiyo ijulikanayo kama ‘Hatoki Mtu Hapa’, itawawezesha wateja wa Airtel kufanya miamala bure bila kikomo kwa kununua kifurushi cha Bure Pack cha wiki au cha mwezi.

“Vifurushi vya Bure Packs vitawapa wateja wa Airtel Money uhuru wa kuchagua kifurushi kinachokidhi mahitaji yao na kuwawezesha kufanya miamala bure bila kikomo kwa wiki au kwa mwezi kulingana na matakwa yao.

Lema uzi na sindano atiwe nguvuni

Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema jana alinusurika kukamatwa na makachero wa Jeshi la Polisi ili kuhojiwa kutokana na ujumbe wake aliouposti kwenye mtandao wa kijamii akiandika: “Rais Kikwete mbona umeamua kuliangamiza taifa.”

Akizungumza na gazeti hili jana akiwa njiani kuelekea Dodoma kushiriki Kikao cha Bunge la Katiba, Lema alisema maafisa wawili wa polisi walimfuata katika hoteli aliyofikia Dar es Salaam kwa lengo la kumkamata na kumpeleka makao makuu ya polisi.

Lema alisema maafisa hao, ambao walikuwa wanatumia gari dogo, baada ya kufika hotelini hapo, waliomba aitwe na aliposhuka walimtaka kuandamana nao, hadi makao makuu ya polisi kwa mahojiano.

“Niliwauliza nikaandeke maelezo juu ya nini, walijibu kifupi wao ni chombo cha dola na walisema wametumwa na viongozi wa juu wa polisi na hawakuwa tayari kutaja tuhuma zangu,” alisema Lema.

Alisema baada ya polisi hao kusisitiza kutaka kumchukua, aliwaomba aende chumbani kujiandaa kabla ya kuwasiliana na viongozi wa chama chake na familia yake.

“Niliposhuka chini sikuwakuta na ndipo nikashauriana na viongozi wa chama hicho na kuamua kuondoka jana mchana Dar es Salaam kuelekea Dodoma.

Hata hivyo, alisema Chadema leo wanatarajia kutoa tamko juu ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wanachama wa CCM kuondoa unyonge dhidi ya wapinzani hasa pale wanapodaiwa kupigwa.

Mbeya City wabadili jezi zao

Dar es Salaam. Timu ya Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara imepanga kubadili jezi zao wanazozitumia zenye rangi ya zambarau na nyeupe ndani ya mwaka huu.

Mbeya City ambayo imepanda daraja msimu huu, imeonekana kuwa tishio kwa klabu kongwe nchini za Simba na Yanga kutokana na upinzani mkubwa wanaoutoa katika Ligi Kuu inayoendelea nchini.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa timu hiyo, Mussa Mapunda alisema kuwa lengo kubwa ni kubadilisha jezi hizo ili ziwe na mwonekano tofauti kati ya wachezaji na mashabiki wanaoishangilia Mbeya City ndani ya Tanzania na mpakani mwa Malawi na Zambia. Alisema soko la jezi zao hivi sasa limeongezeka tofauti na mwanzoni wakati timu yao inapanda kutoka daraja la kwanza kwenda Ligi Kuu, hivyo wamepanga kuzindua rasmi jezi mpya za Mbeya City ndani ya mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Aliongeza kuwa, wamepanga kuleta kontena zima la jezi likiwa pamoja na bendera, kofia, skafu, soksi zenye rangi ya zambarau na nyeupe zinazoiwakilisha timu hiyo.

“Baada ya soko la jezi kuongeza kwa kasi kubwa ndani na nje ya nchi, hivi sasa tumeona ni bora tubadili muonekano wa jezi ya timu yetu, tunataka jezi za wachezaji na mashabiki zitofautiane kidogo.

“Mpango huo tumepanga kuuanza ndani ya mwaka huu, uzinduzi wake utafanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, tayari tumeanza mazungumzo na mawakala wetu wanaotutengenezea jezi waishio nchini China,”alisema Mapunda.

Wabunge wanawajibika kuimarisha elimu majimboni?

Hali ya elimu katika maeneo mengi nchini siyo nzuri. Kinachosikitisha ni kuwa baadhi ya maeneo hayo yanasimamiwa na wabunge waliojipambanua kwa uhodari na umahiri wao wa kujenga hoja bungeni.

Kinyume cha matarajio ya wengi, umahiri na umakini wao hasa katika masuala yanayohusu Taifa, vimeshindwa kujiakisi katika utendaji wa kufuatilia sekta ya elimu jimboni mwao.

Wajibu wa wabunge katika elimuKama ulivyo wajibu wa jumla wa wabunge katika kusimamia utendaji wa Serikali, wajibu wa mbunge katika kusimamia maendeleo ya sekta ya elimu unajumuisha mambo kadhaa ikiwamo, kusimamia mgawanyo wa rasilimali za umma kwa kuhakikisha unazingatia viupaumbele na mahitaji ya elimu na kubainisha changamoto za hali ya elimu na kuitaka Serikali kuboresha hali hiyo.

Mambo mengine ni kuwaunganisha wananchi kuainisha na kuzipatia utatuzi changamoto za elimu na kushirikiana na madiwani kusimamia utekelezaji wa mipango ya Halmashauri kwa kuhakikisha inakwenda sambamba na malengo ya mipango husika.

Hali halisi mikoani

Hata hivyo, kuna utafiti mpya unaoonyesha kuwa wabunge wengi wameshindwa kutekeleza wajibu huu, hatua inayosababisha sekta ya elimu kudorora katika maeneo mengi nchini.

Ilivyo ni kuwa uwajibikaji makini wa wabunge katika kusimamia masuala ya maendeleo, ndiyo chachu ya maeneo wanayosimamia kufanya vizuri katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu. Lakini, wabunge wetu wanawajibika ipasavyo?

Utafiti uliofanywa na Shirika la HakiElimu mwaka 2013, umebaini hali isiyoridhisha ya maendeleo ya elimu ya shule za msingi katika baadhi ya mikoa.

Ripoti ya utafiti huo iitwayo Juhudi za Kuboresha Elimu ya Msingi: Je, Mbunge wako anawajibika katika mkoa wako, kwa kiasi kikubwa inahusisha udhaifu uliopo katika elimu na utendaji usioridhisha wa wabunge, inaowasema wana wajibu wa kuisaidia jamii kuboresha elimu.

“Wabunge wana nafasi kubwa sana katika kuleta mapinduzi ya kubadilisha mfumo wa elimu ili kuinua kiwango cha elimu nchini,’’ inasema sehemu ya ripoti ya utafiti huo ambao kwa sehemu kubwa umetumia takwimu zilizomo katika kitabu cha takwimu za elimu msingi kwa mwaka 2012 (BEST -2012).

Takwimu za BEST

Kwa kutumia takwimu hizo za mwaka 2011/12, utafiti wa HakiElimu ulilenga kupima uwajibikaji wa wabunge katika kuimarisha elimu kwa ngazi ya mkoa.
Viashiria kadhaa kuhusu elimu ya msingi vilitumika kupima uwajibikaji, ikiwamo uandikishaji wanafunzi darasa la kwanza, uwiano wa walimu na wanafunzi darasani, uwiano wa darasa kwa wanafunzi, uwiano wa tundu la choo kwa wanafunzi, uhaba wa madawati, ufaulu na idadi ya wahitimu wanaochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.

Makala haya yanatumia uwiano wa tundu la choo kwa wanafunzi, kuonyesha namna baadhi ya mikoa nchini ilivyoshindwa kutimiza lengo la Taifa ambalo ni shule kuwa na uwiano wa tundu moja kwa wanafunzi 25 (1:25)

Mikoa hiyo na uwiano wake kwenye mabano ni kama ifuatavyo; Arusha ( 1:45), Dar es Salaam (1:70), Dodoma (1:62), Iringa (1:42), Kagera (1:60), Kigoma (1:70), Kilimanjaro (1:28), Lindi (1:45), Manyara (1:34), Mara (1:62) Morogoro (1: 53).

Mikoa mingine ni Mbeya (1:52), Mtwara (1:57), Mwanza (1:77), Pwani (1:44), Rukwa (1:51), Ruvuma (1:50), Singida (1:85), Shinyanga (1:77), Tabora (1:69), Tanga (1:49).

Kwa mujibu wa takwimu hizi, mikoa yenye hali mbaya kwa kukosa matundu mengi ya vyoo ni pamoja na Singida, Mwanza, Shinyanga, Kigoma, Dar es Salaam, Tabora, Mara na Kagera.

Baadhi ya mikoa hii ina wabunge machachari na walio na uwezo mkubwa wa kuhoji mambo hasa yanayohusu Taifa. Cha kushangaza wameipa kisogo mikoa yao, kiasi cha shule nyingi za msingi kukosa hata matundu ya vyoo!

Uhaba wa madawati

Kigezo kingine kilichotumika kupima uwajibikaji wa wabunge ni uhaba wa madawati. Ripoti inaonyesha wabunge katika mikoa mingi wameshindwa kuvisimamia vyombo husika kupambana na changamoto tete ya uhaba wa madawati shuleni.

Wakati lengo la Serikali kitaifa ni kuwa na shule ambazo kila mwanafunzi anakaa juu ya dawati, takwimu za BEST zinaonyesha bado katika mikoa mingi wanafunzi wanakaa chini.

Pamoja na rasilimali misitu ikiwamo yenye miti ya mbao, wabunge wameshindwa kuhamasisha mamlaka husika na jamii kwa jumla kulivalia njuga tatizo la uhaba wa madawati shuleni.

Ruvu Shooting yawapiga mkwara Wazee wa Uturuki

MAAFANDE wa Ruvu Shooting ya Pwani, wametamba kuendeleza wimbi la ushindi itakapokutana na mabingwa watetezi, Yanga ‘Wazee wa Uturuki’ katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Timu hizo zitakutana Jumamosi Uwanja wa Taifa, jijini Dar
es Salaam huku Ruvu ikiingia uwanjani ikiwa na nguvu mpya kutokana na kushika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hivi sasa, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union ‘Wazee wa Oman’ mwishoni mwa wiki na kufikisha pointi 25, ikiwa nyuma ya Simba kwa tofauti ya pointi saba.

Akizungumza kwa simu kutoka Kibaha mkoani Pwani jana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Masau Bwire alisema, wanataka kuwadhihirishia mamilioni ya Watanzania kwamba, wana timu nzuri tofauti na inavyodhaniwa na wengi.

“Kwanza tunashukuru kuanza kutimiza malengo yetu, tangu mwanzo
tulitangaza tunataka ligi ikimalizika tuwe katika tano bora na hilo
limeanza kuonekana, sisi si Wacomoro (Komorozine), Yanga imecheza na timu sawa na timu ya kule nyumbani ya Mkulima SC, ndio maana ikashinda mabao mengi, mashabiki waje kwa wingi uwanjani kujionea kandanda safi la vijana wa Ruvu,” alitamba Bwire.

Alisema, Wacomoro ni timu ya kawaida sana na kuonya kuwa, mashabiki wa Yanga kama wanataka kujua ubora wa kikosi chao waanze kujipima kwa timu ngumu kama yao.

Aliongeza kuwa kutokana na maandalizi yaliyofanywa na Kocha wao, Tom Olaba, kwa sasa hakuna timu itakayowasumbua kutokana na wachezaji kumuelewa vema kocha wao.

Kili Music Awards 2014 yazinduliwa

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), ambao ni wadhamini wa Tuzo za Muziki za Kilimanjaro (KTMA), jana imezindua rasmi kinyang’anyiro cha tuzo hizo mwaka huu, huku ikiondoa kipengele kimoja na kufanya marekebisho kadhaa ya majina kwa baadhi ya tuzo.

Kati ya marekebisho hayo ni kukabidhi kwa wadau na mashabiki wa muziki nchini mchakato wa kupiga kura za kupendekeza washiriki kwa kila kipengele, tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita ambako mashabiki waliwapigia kura wateule.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema tuzo zitakazotolewa katika fainali ya shindano hilo Mei 3 ni 36, badala ya 37 kama ilivyokuwa mwaka jana, ambako Tuzo ya Mtayarishaji Bora Anayechipukia imeondolewa kwa mapendekezo ya wadau.

Alisema kwa mwaka huu wamerudisha uamuzi kwa wananchi ambao ndio watakaopendekeza majina ya wasanii watakaopenda waingie katika kinyang’anyiro hicho, kabla ya baadaye kuwapigia kura za nani awe mshindi katika kila kipengele.

“Majina ya wasanii, bendi, watayarishaji na washindani wengine yatapitishwa kwa kupigiwa kura na mashabiki kwa kutumia tovuti ya www.kilitime.co.tz/ktma, kuponi za magazeti, barua pepe na simu za kiganjani kwa kutuma ujumbe mfupi kwenda namba 15440, ” alisema Kavishe.

Aliongeza kuwa baada ya mashabiki kupitisha majina hayo, yatapelekwa katika kundi la wana ‘Academy’ watakaokaa na kuhakiki majina ya wasanii ambayo yamependekezwa kama yanakidhi vigezo na masharti na kuweka sawa.

Akielezea sababu za kukiondoa kipengele cha Mtayarishaji Bora wa Mwaka, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza, alisema ni kutokana na kukosekana kwa ujio wa watayarishaji wapya, hivyo kujirudia kwa majina ya washiriki, huku wapya wengi wakiwa hawajasajiliwa katika Baraza hilo.

Naye Mratibu wa tuzo hizo zinazoratibiwa na Basata, Kurwijira Ng’oko, alitoa msisitizo kwa watayarishaji na wasanii, kujisajili mapema, la sivyo ataishia kutangazwa na hatapokea tuzo hizo kama atashinda Mei 3.

Kesi ya Lulu yaanza kunguruma

MSANII wafilamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' ambaye anakabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba, amekiri kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na msanii huyo na kwamba walikuwa na ugomvi.
Lulu alikiri hayo jana wakati akisomewa mashtaka yake mbele ya Jaji Rose Temba wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ambapo Lulu baada ya kusomewa mashtaka alikana.
Mbali na kukiri kuwa na uhusiano, pia Lulu alikiri kuwa baada ya tukio alitoka nje ya chumba walichokuwepo na kwenda kumwambia mdogo wake marehemu Kanumba, Setti Bosco kuwa marehemu amedondoka.
Akisoma hati ya mashtaka Wakili Mwandamizi wa Serikali, Monica Mbogo, alidai kuwa Aprili 7, mwaka 2012, Sinza Vatikani, Dar es Salaam, mshtakiwa alimuua bila kukusudia msanii Kanumba .
Wakili Kombo, alidai kuwa pamoja na mambo mengine, marehemu Kanumba baada ya kufa, mwili wake ulipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo majibu yalionesha kwamba kifo chake kilisababishwa na uvimbe ndani ya ubongo.
Upande wa serikali una mashahidi watano pamoja na vielelezo wakati upande wa utetezi unatarajia kuwa na mashahidi watano na vielelezo.

Leonel Messi avunja record

Lionel Messi anaweza kuvunja rekodi yoyote iliyokuwa kichwani mwake,” kwa mujibu wa kocha Barcelona, Gerardo Martino baada ya kumshuhudia nyota wa Argentina akiwa mchezaji watatu kwa wachezaji waliofunga mabao mengi La Liga.

Messi alifunga mabao mawili wakati Barca iliposhinda 6-0 dhidi ya Rayo Vallecano na kumfunika mshambuliaji wa zamani Real Madrid, Raul aliyefunga mabao 228 katika La Liga.

“Amepoteza kumbukumbu ya rekodi zake alizovunja,” Martino aliimbia Barcelona.

Messi amefunga mabao 228 La Liga ikiwa ni mechi yake ya 263, akifunika rekodi ya gwiji wa Real Madrid, Alfredo Di Stefano aliyefunga mabao 227 katika mechi 359, na sasa anazisaka rekodi za Telmo Zarra (251) na Hugo Sanchez (234).

Kwa sasa amebakiza mabao sita tu kuifikia rekodi ya Raul ya kufunga mabao 71 katika Ligi ya Mabingwa.

Simba waigeukia JKT Ruvu J'pili

BAADA ya kuzoa pointi mbili ugenini, Wekundu wa Msimbazi Simba wamepanga kurudisha matumaini yao mapya katika harakati za kuwania ubingwa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuzoa pointi tatu katika mchezo wao wa Jumapili dhidi ya JKT Ruvu
Simba ilianza kutoa sare ya bao 1-1, na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, ikafungwa na Mgambo Shooting Uwanja wa Kwakwani Tanga na mwishoni mwa wiki ilitoa sare ya bao 1-1 na Mbeya City mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Kufuatia matokeo hayo, Simba wamepanga kurudisha heshima yake Jumapili ijayo watakapocheza na JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zdravko Logarusic alisema matokeo ya mechi ya ugenini yamemsikitisha sana na kufuta ndoto zake za kutwaa ubingwa wa bara, hata hivyo hatakata tamaa na badala yake watahakikisha wanafanya vizuri mechi zote zilizosalia.
"Mechi yetu na Mbeya City ilikuwa tushinde; mechi haikuwa ngumu kama wengi walivyotarajia, tatizo ni uzembe wa washambuliaji wangu ambao walipata nafasi nyingi za wazi za kufunga lakini hawakuzitumia," alisema Loga.
Alisema ana kazi kubwa ya kufanyia marekebisho kikosi chake hasa idara ya ushambuliaji ambako ndiko kwa sasa kuna tatizo, hivyo mechi ijayo dhidi ya JKT Ruvu hataki makosa hayo yajitokeze tena.
Pia kocha huyo aliwataka wachezaji wake kucheza kwa kujiamini na kuacha hofu wawapo uwanjani, endapo watacheza kwa kujiamini watafika mbali ikiwa ni pamoja na kushinda mechi zao zote za Ligi Kuu zilizosalia.
Kocha huyo alisema anaamini kabisa mechi yao ya Jumapili itakuwa ngumu na yenye upinzani mkali, hivyo watajiandaa vya kutosha ili kuhakikisha hawafanyi makosa na kujinyakulia pointi tatu.
Simba wanashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu, vinara ni Azam FC wenye pointi 36 sawa na Mbeya City tofauti ikiwa kwenye mabao ya kufunga na kufungwa, Yanga wana pointi 35 na wanashika nafasi ya tatu.

Friday, 14 February 2014

Lowassa, Sumaye, Ngeleja wajieleza Kamati ya Mangula

Waliowahi kuwa Mawaziri Wakuu; Edward Lowassa na Frederick Sumaye jana walifika mbele ya Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM kutoa maelezo juu ya tuhuma za kufanya kampeni za urais kabla ya wakati.

Mbali na wastaafu hao, mwingine ambaye jana alifika mbele ya kamati hiyo ambayo ilikuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana ni Waziri wa Nishati wa zamani na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Mjumbe mwingine wa kamati hiyo aliyehudhuria kikao hicho kilichofanyika kwenye Ukumbi wa White House jana ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi. Wajumbe wengine ni Dk Maua Daftari, Shamsi Vuai Nahodha na Pindi Chana ambao hata hivyo, hawakuhudhuria.

Hata hivyo, wanachama wengine watatu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Naibu wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambao wote wanatazamiwa kuitwa leo mbele ya kamati hiyo.

Vyanzo kutoka ndani ya chama hicho vilieleza kuwa Membe alikuwa katika ziara ya Rais Jakaya Kikwete na alitarajiwa kurejea nchini jana jioni.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa mahojiano ya makada hao watatu jana, Kinana alisema shughuli ya kuwahoji wengine itaendelea leo.

“Kazi haijakwisha, kesho (leo) tunaendelea.”

Waliyosema baada ya kuhojiwa

Akiwa amevalia mavazi rasmi ya CCM, Lowassa alihojiwa kwa takriban saa moja na nusu kwani aliingia katika kikao hicho saa 4:56 asubuhi na kutoka saa 6:40 mchana akiwa ametumia takriban saa moja na nusu na alitoka akiwa mwenye furaha.

Alipoulizwa kuhusu mahojiano hayo Lowassa: “Mazungumzo yalikwenda vizuri. Yalikuwa na lengo la kujenga chama kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Lowassa huku akitabasamu.

Muda mfupi baada ya Lowassa kutoka, Sumaye aliingia kuanzia saa 6:46 na kutoka saa 8:05.

Baada ya kutoka, Sumaye pia hakuwa tayari kuzungumzia kuhusu mahojiano hayo... “Tunawasubiri wakubwa watakavyotoa jawabu.” Alipoulizwa sababu za kutumia muda mwingi katika kikao hicho alisema: “Tulikuwa tunakunywa chai.”
Kwa upande wake, Ngeleja ndiye aliyetumia muda mfupi zaidi kwani aliingia katika ukumbi wa mahojiano saa 8:10 na kutoka 8:50.

Aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa nje ya ukumbi huo kuwa mazungumzo hayo yalikuwa ni ya kichama na kikazi zaidi na kwamba hizo ni taratibu za CCM kuwaita wanachama wake kwa ajili ya kutoa maelekezo.

Kuhusu kutangaza nia ya kugombea urais kabla ya muda uliopangwa na chama, Ngeleja alisema wanaongozwa na kanuni na taratibu na kwamba wakati wa kutangaza kugombea urais haujafika.

Alisema hakuitwa kuhojiwa kwa kutangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda... “Sijatangaza, sijasema, sina ugomvi huo.”

Liverpool, Tottenham 'ngoma inogile'

NAHODHA wa Liverpool, Steve Gerrard juzi usiku aliifungia timu yake bao kwa mkwaju wa penalti dakika za majeruhi na kuisaidia klabu yake kuilaza Fulham mabao 3-2. Bao la kujifunga la beki Kolo Toure, liliipa Fulham uongozi kabla y a Daniel Sturridge kusawazisha.
Lakini kadri mechi hiyo ilipoendelea Fulham , walionesha mchezo mzuri na kuongeza bao la pili kupitia k w a Kieran Richardson, baada ya kipa wa Liverpool, Martin Skrtel kufanya masihara kwenye eneo la hatari.
Uongozi huo wa mabao 2 wa Fulham, hata hivyo haukudumu baada ya Phillippe Coutinho kuisawazishia Liverpool.
Timu hizo mbili zilionekana kugawana pointi moja kila mmoja lakini Liverpool, ilibahatika pale Sascha Riether alipomfanyia madhambi Sturridge katika dakika za ziada.
Nahodha wa Liverpool Gerrard, hakufanya makosa baada ya kukwamisha mkwaju wa penalti na kuandika bao la tatu na kuifanya timu yake kuwa na pointi nne nyuma ya vinara wa ligi hiyo Chelsea.
Ushindi huo ulikuwa wa tano kwa Liverpool, mwaka huu na hii inamaanisha kuwa vijana hao wa Brendan Roggers, wana nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka huu na pia kudumisha rekodi ya kutoshindwa mechi yoyote mwaka huu.
Katika mechi nyingine, Emmanuel Adebayor kwa mara nyingine alifunga mabao mawili na kudumisha harakati za Tottenham za kusalia katika nafasi nne bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza.
Tottenham waliilaza Necastle kwa mabao 4-0 katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa juzi usiku.
Adebayor alifunga bao la kwanza dakika ya 19 baada ya kipa wa Newcastle, Tim Krul kutema mkwaju uliopigwa na Nabil Bentaleb.
Mshambuliaji huyo raia wa Togo, vilevile alichangia bao la pili wakati kipa Krul kwa mara nyingine alipoutema mkwaju wake na kuumpa nafasi, Paulinho kumalizia na kufunga la pili.
Nacer Chadli aliifungia Totenham bao la tatu, baada ya kupiga kombora kali akiwa umbali wa mita 20.
Juhudi za Newcastle ziliishia ukingoni pale kipa wa Totenham, Hugo Lloris alipookoa mikwaju iliyopigwa na Papiss Cisse, Mathieu Debuchy na Yoan Gouffran.
Newcastle sasa haijafunga bao lolote katika mechi saba kati ya nane zilizopita na pia kuandikisha rekodi ya kupoteza mechi nne mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1987.
Nayo Arsenal imepoteza nafasi ya kurejea tena kileleni mwa ligi hiyo, baada ya kutoka suluhu na Manchester United katika uwanja wao wa nyumbani wa Emirates.
Vijana hao wa Arsene Wenger, walikuwa wakijaribu kufuta aibu waliyoipata wiki iliyopita wakati walipofungwa mabao 5-1 na Liverpoool nayo Manchester United, kwa upande wake ilikuwa ikijinasua baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Fulham mwishoni mwa juma lililopita.

Fifa yabariki Okwi kuchezea Yanga

Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), limemaliza utata kwa kumruhusu mshambuliaji Emmanuel Okwi kuitumikia Yanga kama usajili wake umekidhi vigezo.

Yanga ilimsajili Okwi wakati wa usajili wa dirisha dogo, lakini mwanzoni mwa mwezi uliopita, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimsimamisha wakitaka ufafanuzi Fifa baada ya Mganda huyo kuwa na kesi tatu kwenye shirikisho hilo.

Barua ya Fifa iliyotua kwa TFF, ilisema kuwa suala la malipo ya Simba kwa Etoile du Sahel hayahusiani na Okwi kucheza mpira.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliliambia gazeti hili jana kuwa taarifa hiyo ya Fifa imemruhusu mshambuliaji huyo acheze mpira iwapo ametimiza vigezo vyote vya usajili ikiwemo ITC.

“Fifa wametuletea taarifa leo (jana) saa nne asubuhi. Wametaka Okwi aruhusiwe kucheza mpira kama anakidhi vigezo vyote, sasa vigezo ni pamoja na ITC ambayo Okwi anayo, hivyo ni ruksa kucheza mpira.”

Naye Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema aidha Fifa, imeiondoa shaka Simba kwa kuwaambia kuwa kesi yao ya madai ya fedha zao za usajili wa Okwi dhidi ya Etoile haiwezi kuingiliana na masuala ya usajili.

“Tumewajulisha Simba kwamba wasiwe na shaka kwamba kesi yao ya madai ya fedha bado inashugulikiwa na Fifa, wametuahidi watatoa majibu mara baada ya kumaliza taratibu zao. Watulie,” alisema Mwesigwa.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji, Richard Sinamtwa alitoboa siri kwa kudai kuwa Simba ilimwekea pingamizi Fifa mshambuliaji huyo raia wa Uganda asicheze Yanga.

Alisema Simba iliwasilisha pingamizi hilo mwaka jana ikiwa imeandikwa kwa lugha ya Kiswahili ambapo Fifa iliirudisha kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuomba itafsiriwe kwa lugha ya Kiingereza ili waweze kuielewa kwa ufasaha.

“Sisi tulimzuia kwa sababu Simba wamemwekea pingamizi Okwi asicheze Yanga, ndiyo maana tulimsimamisha, usajili wake CAF upo cleared kabisa hauna matatizo yoyote. CAF haijatoa leseni yake kwa vile wanasubiri Fifa itoe hukumu, imehofia isije ikatoa leseni halafu ikajikuta inaingia kwenye mkanganyiko na FIFA,” alisema.

Kwa upande wa Yanga, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Mussa Katabaro, alisema wamezipokea taarifa hizo kwa furaha kubwa, ambapo walikuwa na uhakika wa kile walichokifanya wakati wanamsajili mchezaji huyo.

UN kuzuru eneo la mauaji DRC

Kikosi cha Umoja wa Mataifa kinatarajiwa kuzuru eneo ambako mauaji ya watu wengi yalifanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Hatua hii inakuja baada ya kikosi cha walinda amani cha Umoja huo nchini humo (Monusco) kugundua vijiji vitatu viliteketezwa.

Kikosi hicho kilisema kuwa zaidi ya watu hao sabini waliuawa mwishoni mwa mwezi uliopita na mapema mwezi huu.

Katika mahojiano na BBC, afisa mmoja wa shirika la Monusco, mjini Goma, Ray Tores, amesema kuwa ndege ya wanajeshi wake, iliyokuwa ikifanya uchunguzi, katika eneo hilo iligundua kuwa vijiji vitatu viliteketezwa na kuharibiwa kabisa.

Amesema kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa watazuru eneo hilo baadaye hii leo ili kufanya uchunguzi zaidi.

Jeshi la kutunza amani la Umoja wa Mataifa limeimarisha juhudi zake katika eneo hilo, hasa tangu lilipolisambaratisha kundi la waasi wa M23, Novemba mwaka uliopita.

Bwana Torres, amesema kuwa zaidi ya makundi arubaini ya waasi yanajulikana kuendesha operesheni zao katika eneo hio la Goma.

Manne kati yao yamekuwa yakifanya mashambulio ya mara kwa mara na hivyo kuwa tishio kubwa la usalama.

Umoja wa Mataifa, umesema kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na makundi ya waasi yaliyojihami katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, ili kuwatia hofu watu wanaoishi katika eneo hilo.

Afisa huyo amesema kuwa wengi wa waliouawa walikuwa na majeraha ya mapanga.

Watu 70 wauawa Mashariki mwa Congo-UM

Ndege za umoja zizizokuwa na Rubani Goma
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, umesema kuwa zaidi ya watu sabaini waliuawa mwisho wa mwezi uliopita na mapema mwezi huu.

Katika mahojiano na BBC, afisa mmoja wa shirika la Monusco, mjini Goma, Ray Tores, amesema kuwa ndege ya wanajeshi wake, iliyokuwa ikifanya uchunguzi, katika eneo hilo iligundua kuwa vijiji vitatu viliteketezwa na kuharibiwa kabaisa.

Amesema kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa watazuru eneo hilo baadaye hii leo ili kufanya uchunguzi zaidi.

Jeshi la kutunza amani la Umoja wa Mataifa limeimarisha juhudi zake katika eneo hilo, hasa tangu ilipoisambaratisha kundi la wapiganaji wa waasi wa M23, Novemba mwaka uliopita.

Bwana Torres, amesema kuwa zaidi ya makundi arubaini ya waasi yanajulikana kuendesha operesheni zao katika eneo hio la Goma.

Manne kati yao yamekuwa yakifanya mashambulio ya mara kwa mara na hivyo kuwa tishio kubwa la usalama.

Umoja wa Mataifa, umesema kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na makundi ya waasi yaliyojihami katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, ili kuwatia watu wanaoishi katika eneo hilo hofu.

Afisa huyo amesema kuwa wengi wa waliouawa walikuwa na majeraha ya mapanga.
Wanajeshi wa DRC wakishika doria mjini Goma

Amuua mwenzake kisa Sigara

Tanga. Uvutaji wa sigara umeleta maafa, baada ya mtu mmoja kukatwa mkono na kuuawa na mwenzake wakati wakigombea sigara.

Katika tukio hilo lililotokea Korogwe, Jumapili iliyopita, Februari 2, mnamo saa nne asubuhi, Idi Mkono, mwenye umri wa miaka 30 alimkata mkono Ramadhani Gudelo (35) na kumuua baada ya kutokea ugomvi uliohusu sigara.

Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Constantine Massawe alisema kuwa Polisi Tanga wako katika msako mkali wa kumtia nguvuni Iddi Mkono (30) kwa tuhuma za mauaji.

Kamanda Massawe ameitaka jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, badala yake wafuate taratibu na sheria zilizopo.

Wakati huo huo, watu wawili wanashikiliwa na polisi, mkoani hapa kwa tuhuma za kukamatwa na lita 147 za pombe haramu ya gongo maeneo ya Handeni, mkoani Tanga.

Kamanda Massawe alisema kuwa tukio hilo la kukamatwa kwa watuhumiwa hao lilitokea Februari 2 mwaka huu saa 5:30 asubuhi.

Massawe aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Hussen Muhadu (48), pamoja na Ramadhani Ugarawe (40), wote wakazi wa Chanika Handeni.

Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili watuhumiwa waweze kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Aidha Kamanda Massawe aliwaonya wananchi kuchukua tahadhari na matendo ya uhalifu wa aina yoyote ambao unaweza kusababisha kuvunja sheria, huku akionya kuwa kwa yeyote atakayekiuka sheria zilizowekwa atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Zaidi ya watu 300 wanusurika kifo Mwanga, mkoani kilimanjaro

Familia za zaidi ya watu 300 zimenusurika vifo wilayani Mwanga baada ya mvua iliyoambatana na upepo kuezua mapaa ya nyumba zao 110 .

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga aliliambia gazeti hili jana kuwa hali katika eneo hilo ni mbaya.

Ndemanga alisema mvua hiyo ilinyesha juzi kati ya saa 10:30 na saa 11:30 jioni na kuezua mapaa ya nyumba hizo katika Kata mbili za Mwaniko na Kifula.

“Upepo hasa ulioleta madhara ulivuma kwa dakika kama tano tu hivi japo mvua ya upepo ilinyesha kwa saa moja.... Nimetoka huko hali ni mbaya,”alisema.

Ndemanga alisema upepo huo uliezua paa za nyumba 44 katika Kata ya Mwaniko na nyumba 64 katika Kata ya Kifula huku maelfu ya ekari za migomba zikiwa zimeathiriwa vibaya.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, upepo huo umeezua mapaa ya madarasa saba ya Shule ya Msingi Mangio, ofisi ya walimu na choo cha wanafunzi.

“Kutokana na athari za maafa hayo ni wanafunzi wa darasa la saba, sita na nne tu ndio watakaoendelea na masomo na wengine watabaki nyumbani,”alisema.

Ndemanga alifafanua kuwa, leo wataalamu wa ujenzi watapiga kambi katika shule hiyo kuhakikisha inarejea katika hali yake ya kawaida ndani ya siku saba.

Alisema familia ambazo zimekumbwa na maafa hayo zenye watu wasiopungua 300 zimepatiwa hifadhi na ndugu wakati serikali ikiwa katika harakati za kufanya tathmini ya haraka ili kubaini uharibifu huo..

“Ni hali ya kutisha, lakini mpaka sasa hakuna taarifa za vifo licha ya nyumba mbili kubomoka kabisa....kwa kweli tunamshukuru Mungu kuwa hakuna madhara zaidi ambayo yamejitokeza hadi sasa,” alisema.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo ametuma salamu za pole kwa waathirika wa maafa hayo yaliyotokana na mvua kubwa .

Ndesamburo ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Mjini, kupitia Chadema, leo atafanya ziara katika wilaya hiyo ambapo pamoja na mambo mengine kujionea athari za maafa hayo.
“Kesho (leo) Ndesamburo atafika Mwanga na baada ya kujionea hali halisi ndio atatoa tamko rasmi” alisema Basil Lema, Katibu wa Chadema mkoa.

Kesi ya mauaji ya Mwangosi yanguruma tena

Dar es Salaam na Iringa. Kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi inayomkabili aliyekuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mwenye namba G. 2573 Pacificus Cleophase jana ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa.

Wakati kesi hiyo ikisikilizwa, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa mmoja kati ya 11 wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi, Longishu Losingo (29) amelalamika kuwa wanalishwa mchuzi wa maharage gerezani.

Kesi hiyo ya Mwangosi inasikilizwa na Jaji Mfawidhi, Mary Shangali.

Wakili wa Serikali, Adolf Maganda alidai kuwa mtuhumiwa Cleophase ambaye alikuwa askari polisi mkoani Iringa alifanya mauaji hayo Septemba 2 mwaka 2012 katika eneo la Nyololo, wilayani Mufindi.

“Mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati alipokuwa akiwaamuru wafuasi wa Chadema kuondoka katika eneo la tukio walipopanga kufanyia mkutano,” alidai.

Maganda alidai kuwa katika tukio hilo, mtuhumiwa alifyatua risasi na kumpiga marehemu.

Wakili huyo alidai kuwa wafuasi wa Chadema walifika katika eneo hilo kwa ajili ya kuhudhuria mkutano ambao katibu mkuu wa chama hicho alikuwa anatarajia kuhutubia.

Alisema mkutano huo ulikuwa ufanyike licha ya polisi kuwaandikia Chadema ikiwataka wauahirishe ili kupisha zoezi la sensa.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya kuzuiwa kufanya mkutano, wafuasi wa chama hicho walianza kurusha mawe na kuwaumiza baadhi ya askari polisi, hatua iliyowalazimisha kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na kwamba hatua hiyo ilikuja baada ya kuwasihi kutokufanya mkutano huo.

Maganda alidai kuwa mshtakiwa akiwa na bunduki alikwenda katika eneo la tukio alilokuwa marehemu na kufyatua risasi na kumpiga marehemu ambaye alikufa papohapo. Alidai kuwa taarifa ya daktari inaonyesha kuwa kifo cha Mwangosi kilisababishwa na kupatwa na majeraha yaliyotokana na mlipuko mkali.

Wakati kesi hiyo ikiendelea, katika hali isiyokuwa ya kawaida askari polisi walimkamata Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Iringa, Frank Leonard kwa madai kuwa alipiga picha mahakamani.

Baada ya kukamatwa, Leonard ambaye pia ni mwandishi wa Gazeti la Habari Leo na Daily News alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Kati na kuhojiwa kwa muda kabla ya kuachiwa Katika kesi ya Dk Mvungi, mshtakiwa alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Geni Dudu, ambapo aliwaomba watu wa haki za binadamu kuwatembelea gerezani ili waone jinsi wanavyoishi.

Alilalamika kuwa huko mahabusu wanalishwa maji ya maharage badala ya maharage.

Mshtakiwa alitoa malalamiko hayo, baada ya Wakili wa Serikali, Charles Anindo kuieleza mahakama kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi haujakamilika.

Imeandikwa na Berdina Majinge, Zainab Maeda na Tausi Ally

Thursday, 13 February 2014

Sheria ya ndoa kupigiwa kura ya maoni

Bagamoyo. Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angellah Kairuki amesema kuwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 iko kwenye mchakato wa kurekebishwa kutokana na utata unaokinzana na sheria nyingine za masuala ya kijinsia.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa warsha ya siku moja ya waandishi wa habari na sheria na sera zinazohusu ukatili wa kijinsia iliyoandaliwa na Taasisi ya Champion na Engender Health wilayani Bagamoyo juzi, Kairuki alikiri kuwepo kwa utata wa sheria hiyo jambo linaloendelea ukatili hasa kwa wanawake.

“Utata wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ulijadiliwa katika Baraza la Mawaziri na walishafika mbali. Lakini ilionekana kwa kuwa masuala ya ndoa na mirathi yanagusa mila, desturi, dini na tamaduni za watu, ilionekana siyo rahisi kutunga sheria haraka,” alisema Kairuki na kuongeza:

“Wapo wanaosema mtoto hawezi kuolewa akiwa na miaka 14 na wapo wanaosema anaweza. Baraza la Mawaziri liliamua kuwa kuwe na kura ya maoni (white paper).”

Hata hivyo alisema kuwa wakati mchakato huo ukikaribia kuanza uliingiliana na mabadiliko ya Katiba. Hivyo alisema kura hiyo ya maoni itafanyika baada ya kupatikana kwa Katiba Mpya.

Awali akifungua warsha hiyo, Kairuki alisema kuwa Serikali imechukua hatua za kukabiliana na ukatili wa kijinsia ikiwa pamoja na kuanzisha dawati la jinsia na watoto kupitia Jeshi la Polisi na timu za ulinzi na usalama wa watoto kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii.

Akitoa mada katika warsha hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Taasisi ya Engender Health, Dk Monica Mhoja alisema Serikali ya Tanzania inasifika kwa kuridhia sheria na mikataba ya kimataifa kuhusu ukatili wa kijinsia, lakini hazitekelezwi ipasavyo.

“Tunapokuwa kwenye majukwaa ya kimataifa, Tanzania tunasifika kwa kuridhia sheria na sera nyingi, wanapotuhoji kuhusu utekelezaji inakuwa shida,” alisema Dk Mhoja.

Wafanyakazi wa Red Cross watekwa Mali

Kundi la wapiganaji la MUJAO nchini Mali

Shirika la habari la AFP linasema kuwa kundi la wafanyikazi wa shirika la msalaba mwekundu ambao walitoweka Kaskazini mwa Mali limetekwa nyara na wapiganaji wa kiislamu.

Shirika hilo linasema kuwa wapiganaji wa kundi la umoja na Jihad Magharibi mwa Afrika (Mujao) wamethibitisha kuyakamata magari manne na kusema kuwa abiria waliokuwa ndani ni maafisa wa shirika la msalaba mwekundu.

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya kati , Generali Babacar Gaye, ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za dharura kuzuia kuenea kwa ghasia zaidi ambazo anasema zinaligawanya taifa hilo .

Wafanyakazi wa shirika hilo wanasema kuwa waliotekwa nyara wako salama na bukheri wa afya mikononi mwa wapiganaji hao wa kiislamu.

Kundi la MUJAO ni moja ya makundi ya wapiganaji walio na uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda ambalo lilidhibiti kaskazini mwa Mali mwaka 2012 kabla ya kuondoshwa kutoka eneo hilo na wanajeshi wa Ufaransa mwezi Januari mwaka jana.

Kundi hilo linasemekana kutuma taarifa iliyosema, ''Asante kwa Mungu tumekamata gari lenye maadui wa uisilamu wakiwa na washirika wao. ''

Msemaji wa shirika hilo Alexis Heeb kulingana na AFP alisema kuwa wafanyakazi hao wanne wa shirika la Red Cross na mfanyakazi mmoja kutoka katika shirika lengine la misaada walitoweka Jumamosi wakiwa ndani ya gari lao katika eneo lililo kati mwa miji ya Kidal na Gao.

Watu hao wote ni raia wa Mali.

AFP ilimnukuu msemaji huyo akisema kuwa'' sasa hivi tuna wasiwasi mkubwa na tunajaribu kuwasiliana na kila mtu tunayemjua kuhakikisha usalama wao. Inaarifiwa kuwa kundi hilo linarejea katika ngome yao mjini Gao.

Kesi ya Zitto dhidi ya Chadema kutajwa leo Mahakama Kuu Dar es salaam

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe .

Kesi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe dhidi ya chama chake hicho inatarajiwa kuanza kutajwa leo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alifungua kesi hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema, akiiomba mahakama hiyo ikizuie chama kujadili uanachama wake, hadi rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama kupinga kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.

Katika kesi hiyo namba 1 ya 2014, Zitto pia aliiomba mahakama hiyo imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilichomvua nyadhifa zote alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini.

Kesi hiyo ambayo inasikilizwa na Jaji John Utamwa imepangwa kuanza kutajwa leo kabla ya kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa rasmi.

Tayari mahakama imeshatoa amri ya zuio la muda kwa Chadema kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.

Uamuzi huo ulitolewa Januari 7 na Jaji Utamwa, kutokana na maombi ya Zitto, kupitia kwa Wakili wake Albert Msando.

Awali mawakili wa Chadema, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na Mkurugenzi wake wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya kupewa zuio la muda.

Katika uamuzi wake, Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa zuio hilo.

Kizimbani kwa kumshambulia mtoto

Mkazi mmoja wa Kitangiri jijini Mwanza, Sophia Rafael (32), amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumng’ata kidole mtoto wake.

Wakili wa Serikali, Juma Sarige, alidai mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Nyamagana, Janeth Masesa, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Februari 9 mwaka huu.

Alidai kuwa siku ya tukio, mshtakiwa alimng’ata kidole mtoto wake wa umri wa miaka 10, akimtuhumu kumwibia Sh5,000.

Upande wake mtoto huyo alidai kuwa mama yake alimfanyia kitendo hicho na kusababisha kidole kukatika.

Upande wa jirani aliyejitambulisha mbele ya mahakama hiyo kuwa Jenifa Mbando (30), alidai kuwa aliposikia sauti ya mtoto huyo akipiga kelele alitoka nje na kutaka kujua kipi kilichokuwa kinaendelea.

Alisema baada ya muda mfupi, alimwona mtoto huyo akitokwa na damu nyingi mkononi na kwamba alichukua uamuzi wa kumpeleka hospitalini.

Hata hivyo mama huyo alidai kuwa hakufanya kwa makusudi ila alizidiwa na hasira.

Hakimu Masesa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 5 mwaka huu itakapotajwa tena.

Soko la Kagunga Kigoma kunufaisha maziwa makuu

Ujenzi wa Soko la Kimataifa katika Kijiji cha Kagunga, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mkoani kigoma jirani na mpaka wa Tanzania na Burundi linatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha kibiashara katika nchi za maziwa makuu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Miriam Mmbaga amesema, ujenzi huo wa soko unatarajiwa kutumia Sh2 bilioni hadi kukamilika na litaongeza fursa za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa ajira kwa wananchi wa nchi hizo tatu za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Alisema bidhaa za uvuvi na kilimo ambazo zinazalishwa kwa wingi na wananchi katika maeneo hayo, zinatajwa kuwanufaisha wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawana soko la uhakika la kuuza bidhaa zao, badala yake huzisafirisha Burundi ambako soko lake halina uhakika.

“Licha ya biashara hizo za mazao ya kilimo na uvuvi, pia tunatarajia bidhaa nyingine za viwandani zitauzwa sokoni hapo, na jambo hilo litainua uchumi wetu kama halmashauri na taifa, kutokana na wananchi wetu kujipatia kipato sanjali na kukusanya ushuru na kodi za Serikali,” alisema Mmbaga.

Mkurugenzi huo ametaja changamoto ya ukosefu wa barabara inayokwenda kijijini hapo kama kikwazo kikubwa kinachokwamisha harakati za wafanya biashara kuwekeza kwa kasi katika soko hilo la aina yake mkoani hapa.

“Hakuna barabara inayounganisha Mji wa Kigoma na Kijiji hicho cha Kagunga,hii inafanya usafiri pekee unaotegemewa kuwa kwa njia ya boti katika Ziwa Tanganyika, ambapo mara kadhaa hutokea ajali ya kuzama, kitendo kinachofanya mali kupotea ziwani na nyingine kuharibika. Hii ni changamoto kubwa kwetu,” alisema Mmbaga.

Pia ufinyu wa bajeti inayopelekea ucheleweshaji wa mradi huo, ingawa kwa sasa wamepata mbia ambaye ni Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ambao wanatarajia kutoa fedha za ujenzi huo zinazofikia Sh2 bilioni kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi.

Ujenzi wa soko hilo ulioanza mwaka 2009 tayari umetumia Sh365 milioni kutoka mapato ya ndani ya halmashauri na kuna mkakati wa kutenga Sh500 milioni.

Wednesday, 12 February 2014

Chelsea yatoka sare ya 1-1 na West Brom

Chelsea imepoteza nafasi ya kuhakikisha kuwa imesalia kileleni mwa ligi kuu ya Premier ya Uingereza, mbele ya mahasimu wao Arsenal, baada ya kutoka sare ya kufungana bao moja kwa moja na West Brom, katika mechi iliyochezewa katika uwanja wa Hawthorns.

Victor Anichebe aliifungia West Brom bao hilo muhimu kunako dakika ya 87 Na kuinyima Chelsea alama mbili ambazo zingeihakikishia Chelsea hakikisho la uongozi wa ligi hiyo hadi juma lijalo.

Branislav Ivanovic aliiweka Chelsea mbele dakika ya 45, bao ambalo lilikuwa limeipa vijana hao wa Jose Mourinho kuwa alama nne mbele ya Arsenal ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya pili.

Arsenal imeratibiwa kucheza na Manchester United, siku ya Jumatano usiku na ikiwa Arsenal itashinda mechi hiyo itajihakikisha nafasi ya kwanza kwenye msururu wa ligi hiyo inayokwenda mapunzikoni mwishoni mwa juma hili ili kuruhusu mechi za kuwania kombe la FA.
Wachezaji wa Arsenal

Matokeo zaidi

Katika matokeo mengine ya mechi za ligi kuu zilizochezwa hiyo jana, Southampton iliilaza Hull City bao moja kwa bila.

Mlinda lango wa Southampton, Jose Fonte ndiye aliye bahatika kufunga bao hilo kufuatia purukushani katika lango la Hull City.

Dakika chache baada ya kufunga bao hilo, Fonte alivurumisha kombora kali ambalo liliokolewa na kipa wa Hull Jay Rodriguez.
Kocha Sam Allardyce

West Ham imepanda hadi nafasi ya kumi kwenye jadwali ya ligi hiyo baada ya kuilaza Norwich kwa magoli mawili kwa bila.

Ushindi huo ulikuwa wa tatu mfululizo kwa timu hiyo iliyo na makao yake Mashariki mwa jiji la London.

Norwich kwa upande wake inashikilia nafasi ya kumi na sita alama moja mbele ya West Brom na Sunderland iiliyo katika nafasi ya kumi na saba na kumi na nane mtawalia.

Cardif nayo imesalia katika nafasi ya mkia baada ya kutoka sare ya kutofungana bao lolote na Aston Villa.

Katibu mkuu wa UN aonya kuhusu ghasia-CAR

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ameonya kuwa ghasia zinazoendelea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, zinaweza kuligawa taifa hilo na kuwatenga kabisa Wakristo na Waislamu.

Bwana Ban ki ameiomba Ufaransa kuwatuma wanajeshi zaidi wa kutunza amani katika taifa hilo, ambalo limekumbwa na mapigano ya kidini tangu mapinduzi ya kijeshi Machi mwaka uliopita.

Katika siku za hivi karibuni, maelfu ya Waislamu wamekimbilia nchi jirani, ili kuepuka mapigano hayo.

Katika ripoti mpya iliyochapishwa na shirika la kutetea haki za kibinadam, la Amnesty International, inasema kuwa wanajeshi wa Kimataifa wa kutunza amani nchini humo wameshindwa kuzuia kile ilichokitaja kama mapigano ya kidini yanayodhamiria kuwaangamiza raia wote ambao ni Waislamu.

Katika ripoti yake shirika hilo linasema kuwa vikosi vya kimataifa vimesita sita kukabiliana na wanamgambo wa AntiBalaka ambao wengi wao ni Wakristo wanaoendesha mashambulizi dhidi ya Waislam.

Jamii nyingi za raia wanaoishi katika miji ya Kaskazini Magharibi mwa taifa hilo wameachwa bila ulinzi.

Tuesday, 11 February 2014

Ajali ya ndege yaua 100 Algeria

Ndege ya usafiri ya jeshi imeanguka ikiwa imebeba zaidi ya watu 100.

Redio ya taifa inasema ndege hiyo imeanguka katika eneo la milima katika jimbo la Oum El Bouaghi kusini mashariki mwa mji mkuu , Algiers na ilikuwa imewabeba abiria 103 wakiwemo wafnyakazi wa ndege hiyo.

Kuna taarifa kwamba ndege hiyo ilikuwa imebeba familia za maafisa wa jeshi.

Ndege hiyo ya wanajeshi inaripotiwa kuanguka katika eneo lililo na milima mingi mashariki ya nchi hiyo. Kituo cha Redio ya nchi ya Algeria inasema kuwa kulikuwa na waabiri 103, wakiwemo watumishi wa ndege hiyo.

Hakuna ripoti rasmi za majeruhi, ila vituo vya habari vya nchi hiyo vinapeana matumaini kwa uchache mno juu ya manusura.

Ndege hiyo inasemekana ilikuwa ikibeba wanajeshi na watu wa familia zao waliokuwa wakisafiri kuelekea jiji la Constatine. Jeshi halijatoa taarifa yoyote mpaka sasa.

Namweshimu sana Jaquar

Mwanamuziki Vivian Wambui, amewaomba wapenzi wa muziki kumheshimu na kuacha kumuhusisha na tuhuma za uhusiano wa kimapenzi na Jaguar.

Amesema anaweza kuwa na uhusiano na mtu yeyote anayempenda lakini siyo kwa watu anaowaheshimu kama Jaguar.

“Naomba mniheshimu, Jaguar ni kama kaka yangu jinsi tunavyoheshimiana na anavyonishauri kwa nia njema, sioni sababu ya kila kukicha kusema ni mpenzi wangu mnanidhalilisha,” alisema Vivian, alipohojiwa kwa njia ya simu na mtandao wa Bigeye.

Vivian alifafanua kuwa jambo la maana kwao ni kutathmini muziki wanaokufanya badala ya kuanzisha maneno ya ajabu ambayo yanaishushia hadhi tasnia ya muziki, kwa kuonekana ni kama kituo au kazi ya kuendeshea uhuni.

Ahueni kwa wafanyikazi wa Qatar 2022

Kamati andalizi ya kombe la dunia mwaka wa 2022 itakayoandaliwa huko Qatar imetoa mustakabali mpya utakaosimamia uhusiano baina ya wenye kandarasi na wafanyikazi wa kigeni wanaojenga viwanja vitakavyotumika katika michezo hiyo.

Takriban wajenzi 200 raiya wa Nepal waliripotiwa kufariki katika miradi ya ujenzi mwaka uliopita.


Kulingana na Shirika la International Trade Union iwapo hali itasalia ilivyo sasa nchini Qatar wafanyi kazi takriban 4000 watakuwa wamepoteza maisha yao katika ujenzi wa viwanja na muundo msingi wa kombe hilo la dunia.
Mapendekezo mapya:Qatar 2022
Kufanya kazi kwa jumla ya saa 48 kwa wiki na likizo ya majuma matatu kwa kila mwaka.
Kuwekwa kikao ilikushughulikia malalamiko ya wafanyikazi
Kuwekwa laini ya simu itakayotumika kuripoti visa vya dhuluma
Kukomeshwa kwa kazi za lazima

Taifa hilo la Ghuba lilikuwa na makataa ya hadi tarehe 12 Februari 2014 kuifahamisha shirikisho la soka duniani Fifa mikakati ya kuboresha hali ya utendakazi wa wafanyikazi .

Mustakabali huo mpya wa utendakazi wenye ukurasa 50 ,umeundwa kwa ushirikiano wa shirika la wafanyikazi duniani ILO.

Mbali na vifo vya wafanyikazi 185 mwaka uliopita,inaaminika kuwa idadi kubwa ya wafanyikazi wamejeruhiwa kazini kutokana na mazingara mabaya ya kufanyia kazi.
Kumeibuka ,pia maswali kuhusiana na makazi duni ya wafanyikazi.

Mashirika ya wafanyikazi na yale ya kupigania haki za kibinadamu yamelalamikia vikali mfumo wa Qatar wa uajiri uitwao ''Kefala '' ambao unapatanisha hati ya usafiri ama VISA na kampuni inayowaajiri mfanyikazi.
Wafanyakazi Qatar 2022

Mashirika hayo yanasema kuwa mfumo huo unawanyima wafanyikazi haki ya kuondoka Qatar bila ya idhini ya mwajiri wao pindi wanapotofautiana ama kudhulumiwa.

Katibu Mkuu wa kamati andalizi ya qatar 2022 Hassan Al-Thawadi, amesisitiza kuwa mashindano hayo hayatafaidi jasho na damu ya watu.

Hali na haki ya wafanyikazi wanaojenga viwanja vya kombe la dunia vitakavyotumika mwaka wa 2022 ilizua mjadala mwaka uliopita baada ya mashirika ya kupigania haki za wafanyikazi duniani kudai kuwa wenye kandarasi za kujenga viwanja na muundo msingi wa Qatar 2022 walikuwa wamewaajiri raiya wa kigeni ambao walikuwa wanafanyishwa kazi bila malipo ama kwa malipo duni.

Qatar2022Rais wa shirikisho la soka duniani Sepp Blatter aliingilia kati na kuahidi kufanya mashauriano na Kiongozi wa taifa hilo lenya utajiri mkubwa wa mafuta.

Mashindano hayo yameripotiwa kuwa yataigharimu Qatar dola bilioni 200

Kocha wa simba asema kuhusu kombe wanasimba wasahau

KOCHA Mkuu wa Simba Zdravko Logarusic amesema kuwa matokeo ya mchezo wao wa juzi dhidi ya Mgambo Shooting, yamezidi kumkatisha tamaa kabisa katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba juzi walijikuta wakipoteza mechi yao hiyo iliyopigwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kwa kukubali kichapo cha bao 1-0.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha huyo alisema hakutegemea kama timu yake ingepoteza pointi tatu katika mchezo huo, ikizingatiwa kuwa taarifa alizonazo kabla ya kuwa kocha wa Simba ni kwamba timu ya Mgambo mechi ya mzunguko wa kwanza walifungwa mabao 6-0.
"Kwa kweli ndoto za kutetea ubingwa wa bara zinazidi kupotea, nasikitika pia kwa jinsi matokeo ya mechi mbili zilizopita jinsi yalivyokuwa, kwa upande wangu imeniuma sana," alisema Loga.
Alisema hata hivyo atazidi kufanyia marekebisho kikosi chake, ili mechi zilizosalia wafanye vizuri hasa mechi ijayo dhidi ya Mbeya City ambayo anaamini itajaa upinzani mkubwa.
Hata hivyo kuna taarifa kuwa kuna hujuma katika timu hiyo na ndiyo maana matokeo yamekuwa mabaya kwa timu hiyo, hali ambayo jana iliwalazimu viongozi wa timu hiyo kukutana na Kocha Mkuu kwa ajili ya kujadili mwenendo wa timu hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa klabu hiyo Aden Rage alipanga kukutana na kocha mkuu, ambapo leo atakutana na wachezaji wote ili kujua nini tatizo mpaka kupelekea kufanya vibaya katika mechi mbili zilizopita.
Pia kuna taarifa kuwa huenda wachezaji hao wakawa katika mgomo baridi, baada ya kudaiwa kuwa walikasirishwa mechi yao na Mtibwa Sugar ambayo walitoka sare kufokewa na kocha wao timu hizo zikiwa mapumziko.

Liverpool ya sababisha mauaji Kenya

MWANAMUME raia wa Kenya anayeshabikia klabu ya soka ya Uingereza ya Liverpool amechomwa kisu na mwenzake wa klabu ya Arsenal na kufa katika eneo la Meru Mashariki mwa Kenya.
Kwa mujibu wa polisi wa eneo hilo, wawili hao walianza malumbano baada ya mechi kati ya vilabu hivyo kumalizika hapo Jumamosi.
Kwa mujibu wa BBC, mashabiki hao walikuwa katika baa moja iliyojaa wapenzi wa timu hizo mbili.
Shabiki wa Arsenal anayefanya kazi ya bodaboda alijawa na hasira baada ya timu yake kuzomewa na shabiki wa Liverpool kiasi cha kumchoma mwenzake kisu mara kadhaa, kabla ya kutoweka.
Watu waliokuwa karibu na eneo la tukio, walimsaidia majeruhi aliyetambuliwa kwa jina la Anthony Muteithia na kumpeleka Hospitali Kuu ya Meru, ambapo alifariki wakati akipatiwa matibabu.
Mkuu wa polisi eneo la Meru, Tom Odero, amesema wanamsaka shabiki huyo wa Arsenal ambaye amekwenda mafichoni.

Waandishi wa habari waigomea CCM

SIKU moja baada ya kukamatwa, kupigwa na kisha kuporwa vifaa vyake vya kazi, mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi wilayani Bunda, Christopher Malegesi, na kiongozi mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa, Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), kimetangaza kugoma kuandika habari za chama hicho.

Mwenyekiti wa chama hicho, Emanuel Bwimbo, aliiambia Tanzania Daima kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kuona kitendo hicho kimefanyika kwa makusudi.

“Kitendo alichofanyiwa ni cha kinyama na kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 18. Sisi kama chama pia tumeamua kamwe hatutaandika habari za CCM, bali tutaandika maovu yao kama yakijitokeza.

“Kamwe hatutaenda katika ziara zao na wala mikutano yao maana wao ni mabingwa wa kupiga,” alisema Bwimbo.

Alisema kwa muda mrefu waandishi wa habari wamekuwa wakionewa na kupigwa katika mikutano ya CCM huku serikali ikifumbia macho, jambo ambalo limekuwa likiweka chuki kati ya waandishi na chama hicho.

Bwimbo aliwataka watendaji wa serikali likiwemo Jeshi la Polisi na CCM kutambua kuwa taaluma ya habari inatambulika ulimwengu mzima, na kwamba kama CCM wanataka kufanya mchezo basi wataona nguvu ya kalamu.

Awali akizungumzia tukio la kupigwa kwa mwandishi huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ferinandi Mtui, pamoja na kulaani kitendo hicho aliahidi kusimamia suala hilo na kuhakikisha waliofanya hivyo wanafikishwa mahakamani.

Dk. Maua Daftari ashinda kesi dhidi yake

ALIYEKUWA Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dk. Maua Daftari, ameshinda rufani aliyokata dhidi ya mfanyabiashara Fatuma Salimini Said, aliyetakiwa alipwe sh milioni 100.

Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani linaloongozwa na Jaji Angela Kileo, Sauda Mjasiri na William Mandia.

Jopo hilo lilitengua hukumu ya awali iliyotolewa na Jaji Laurean Kalegeya Julai 9, 2010, iliyomtia hatiani Dk. Maua Daftari na kumtaka alimlipe malamikaji sh milioni 100.

Dk. Daftari ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM, alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani, kupinga Mahakama Kuu iliyomwamuru kumlipa mfanyabiashara huyo sh milioni 100.

Katika kesi ya msingi iliyofunguliwa mwaka 1999 mlalamikaji Fatuma Salimin Said, alikuwa akimlalamikia Dk. Daftari kumtapeli pesa taslimu pamoja na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya sh 200 milioni. Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Fatma alikuwa akimdai Dk. Daftari sh 100,092,400 alizompa ili amnunulie vifaa mbalimbali kati ya mwaka 1994 na 1997, lakini mlalamikiwa hakufanya hivyo.

Vitu hivyo ni pamoja mashine ya kusindika matunda kutoka nchini Afrika Kusini, king’amuzi kutoka Uingereza, magari na pesa.

Hata hivyo majaji wa Mahakama ya Rufani walisema baada ya kupitia hukumu iliyotolewa na Jaji Kalegeya, hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu suala linalolalamikiwa.

Majaji hao walisema wamekosa ushahidi wa kumtia hatiani mkata rufaa huyo Dk. Maua Daftari, hakukuwa na ushahidi wowote kuonyesha kuwa kiasi hicho cha sh milioni 100 kilipita kati ya mikono ya Fatuma Salmini kwenda kwa Maua Daftari.

Walisema walitaka swali la msingi lijibiwe kuonyesha ushahidi usiotiliwa shaka kuonyesha kama kweli mlalamikaji alimpa mlalamikiwa kiasi hicho cha fedha ambapo ilionekana kuwa mlalamikaji alilipa kiasi hicho cha fedha kwa njia ya hundi kupitia akaunti iliyokuwa haina fedha ya kiwango kinachotajwa, isipokuwa mlalamika aliegemea zaidi ushahidi wa mtu mmoja anayesadikiwa ndiye aliyepeleka hundi hiyo.

Kwa mujibu wa majaji, akaunti hiyo haikuwa na fedha, ndio maana hundi hiyo haikuheshimiwa ili malipo halali yafanyike.

Awali wakili wa mkata rufaa, Peter Swai, alidai Mahakama Kuu haikutenda haki kumhukumu Daftari kulipa kiasi hicho cha fedha.

Akizungumza na Tanzania Daima, Dk. Daftari alisema amefurahia uamuzi huo kwakuwa hakuna baya lolote alilofanya kwa mfanyabiashara Fatuma Salimini Said.

Kimbunga chavuruga makazi, na miundo mbinu

Upepo mkali uliovuma mithili ya kimbunga, umeezua mapaa ya nyumba zipatazo 200 katika Mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro na kusababisha mamia ya familia, kokosa mahali pa kuishi.

Maafa hayo yametokea wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikiwa imetoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua na upepo mkali katika maeneo mbalimbali kuanzia leo hadi keshokutwa.

Katika Mkoa wa Morogoro, nyumba 183 zimeezuliwa kutokana na upepo mkali uliojitokeza jana katika Kata za Kidatu Sanje, Mkamba na Mkula, wilayani Kilombero.

Upepo huo uliodumu kwa takriban saa mbili, pia umeharibu mazao na kuangusha miti ambayo mingine iliangukia kwenye nyumba na kuzibomoa.

Taarifa kutoka katika maeneo hayo zilibainisha kuwepo kwa majeruhi mmoja aliyeangukiwa na mti, lakini aliwahishwa katika Hospitali ya Mtakatifu Francis, mjini Ifakara kwa matibabu.

Kwa mujibu wa habari hizo, watu waliokosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa, wamepata hifadhi kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, David Ligazio, alikiri kuwa upepo uliovuma katika maeneo hayo, haujawahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 iliyopita.

“Ni kweli kumetokea upepo mkali uliodumu kwa muda wa saa mbili na baadhi ya nyumba za watu zimeathirika, watu wanaishi kwa ndugu na jamaa zao. Kwa sasa tunaangalia namna ya kusaidia,” alisema mwenyekiti huyo.

Katika maeneo ya Shule ya Msingi Itefa, kulibainika kuwa vyumba vinne vya madarasa na viwili vya ofisi za walimu vimeezuliwa kwa upepo huo ulioanza wakati tayari wanafunzi wakiwa wameruhusiwa kurudi nyumbani.

Tofauti na ilivyotokea Kilombero, katika Wilaya ya Same, upepo huo uliandamana na mvua kubwa yaliyosababisha mapaa ya nyumba kuezuliwa na Barabara ya Dar es Salaam – Moshi eneo la Hedaru kufungwa kwa muda.

Katika Kata ya Makanya, zaidi ya nyumba nane zimeezuliwa na nyingine kuanguka.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi, alisema maafa hayo yametokana na mvua zilizoanza kunyesha tangu juzi na kusababisha maji kutoka maeneo ya milimani kufurika katika uwanda wa chini ambao ni tambarare.
“Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya milimani zimesababisha maji kujaa katika maeneo ya tambarare. Nyumba zimejaa maji, pia imeathiri ujenzi wa madaraja katika Barabara ya Same –Mombo,” alisema.

Kujaa kwa maji katika barabara hiyo, kumesababisha msururu mkubwa wa magari yaliyokuwa yakitoka Arusha kwenda Dar es Salaam na Tanga.

Pia yaliyotokea Moshi Kilimanjaro na Arusha kwenda katika majiji ya ya Dar es Salaam na Tanga.

Keshi awachagua wachezaji wapya

Kocha wa Nigeria Stephen Keshi, amewajumuisha wachezaji watatu ambao hawajawahi kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo Super Eagles, katika kikosi chake kitakachochuana na Mexico, mjini Georgia, Atlanta tarehe tano mwezi ujao, katika mechi ya kimataifa ya kirafiki.

Wachezaji hao ni pamoja na Imoh Ezekiel, Ramon Azeez na Michael Uchebo

Mshambulizi matata wa Standard Liege Imoh Ezekiel, sasa amepewa fursa ya kujitafutia nafasi katika kikosi cha Nigeria, kitakacho wakilisha taifa hilo kwenye fainali ya kombe la dunia nchini Brazil.

Msimu huu Ezekiel, mwenye umri wa miaka 20, amefunga magoli tisa na kwa muda mmrefu amekuwa katika hali nzuri hali iliyomfanya kocha Keshi kumjumuisha kwenye kikosi chake.

Uchebo, ambaye anasakata soka nchini Ubelgiji, ameifunguia klabu klabu yake ya Cercle Brugge amegoli matano naye mcheza kiungo Azeez kwa upande wake hajakuwa na bahati ila amekuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanauwezo wa kucheza safu ya kati na ushambulizi kwa wakati mmoja.

Wachezaji wawili wa kutegemewa wa Nigeria, Shola Ameobi wa NewCastle na Brown Ideye wa Dynamo Kiev kwa sasa wako chini kimchezo na aliyekuwa mshambulizi wa timu ya taifa ya Nigeria Uchebo huenda akajikatia tikiti ya kwenda Brazil.

Mwenyekiti wa CCM Dar kizimbani kwa kusambaza ARV feki

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI), Ramadhani Madabida (kulia) na Ofisa Ubora wa Bidhaa wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Evance Mwemezi walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kusomewa mashtaka ya kuuza na kusambaza dawa feki za ARV

Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Ltd cha Dar es Salaam (TPI), Ramadhani Madabida na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kusambaza dawa bandia na kusababisha hasara ya Sh148.3 milioni.

Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi aliwataja washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo kuwa ni Mkurugenzi wa Operesheni wa TPI, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msofe, Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango pamoja na wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD), Sadick Materu na Evans Mwemezi.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nyigulile Mwaseba, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema katika shtaka la kwanza, Aprili 5, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango wakiwa na nyadhifa hizo kwenye kiwanda cha TPI walisambaza makopo 7,776 ya dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) aina ya Antirectroviral.

Kimaro alidai kuwa washtakiwa hao, walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 76 (1)(2) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003, wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halali na kwamba zimetengenezwa Machi, 2011 na muda wake wa kutumika unakwisha 2013 wakati wakijua kuwa si kweli.

Katika shtaka la pili, Wakili Kimaro alidai kuwa Aprili 11, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango walisambaza na kuuza makopo 4,476 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral walizokuwa wakijaribu kuonyesha kuwa zilikuwa na viambatanisho vya Starudine 30mg, Nevirapine 200mg, Lamivudine 150mg pamoja na fungu namba OC 01.85.

Alidai kuwa washtakiwa hao waliweka viambatanisho hivyo wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halisi na kwamba zilitengenezwa Machi 2011 na muda wake wa kutumika ulikwisha Februari 2013 huku wakijua kwamba ni uongo.

Katika shtaka la tatu wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kinyume na Kifungu cha 302 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Wakili Kimaro alidai kuwa kati ya Aprili 12 na 29, 2011, washtakiwa hao wakiwa na nia ya kulaghai, walijipatia Dola za Marekani 98,506 sawa na Sh148,350,156.48 wakijaribu kuonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha ni malipo halali ya makopo 12,252 ya dawa aina ya Antirectrovial yaliyokuwa katika fungu (batch) namba OC 1.85.

Alidai pia kuwa washtakiwa hao walikuwa wakionyesha dawa hizo bandia zilikuwa zimetengenezwa Machi, 2011 na kwamba muda wake wa kumalizika kutumika ni Februari, 2013 na wakafanikiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka MSD.

Katika shtaka la nne, Materu na Mwemezi wakiwa ni Meneja wa Udhibiti Viwango na Ofisa Udhibiti Viwango wa MSD, kati ya Aprili 2 na 13, 2011 huku wakijua nia ya kutendeka kwa makosa hayo ya usambazwaji wa dawa bandia, walishindwa kuzuia kinyume na Kifungu cha Sheria namba 383 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Katika shtaka la tano, wakili huyo wa Serikali alidai kuwa kati ya Aprili 5 na 30, 2011, washtakiwa Madabida, Shamte, Msofe, Shango pamoja na Materu na Mwemezi, kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi, walishindwa kutekeleza majukumu yao wakiwa watendaji.

Alidai kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kusambaza makopo 12,252 ya dawa bandia wakijaribu kuonyesha kuwa zilitengenezwa Machi 2011 na kwamba zitakwisha muda wake wa kutumika Februari 2013 na kuisababishia mamlaka hiyo ya Serikali hasara ya Sh148,350,156.48.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na upande wa mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Mwaseba alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao wanafanya kazi kwenye taasisi zinazotambulika kisheria na kwamba kila mdhamini angesaini bondi ya Sh6,181, 256.

Pia alimtaka kila mshtakiwa kutoa kiasi cha Sh12, 362,513 milioni taslimu mahakamani hapo au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Madabida na Materu waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti hayo huku wenzao wakipelekwa mahabusu kusubiri kuyakamilisha.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, mwaka huu itakapotajwa.

Sunday, 9 February 2014

Medali zaanza kunyakuliwa Olimpiki

Sage Kotsenburg akishangilia medali yake

Mwanariadha wa Marekani Sage Kotsenburg amekuwa mwanariadha wa kwanza kunyakua medali ya kwanza ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi inayofanyika katika mji wa Sochi nchini Urusi.

Sage Kotsenburg, amenyakua medali hiyo katika mchezo wa kuteteleza katika barafu kwa kwa kutumia ubao kwa upande wa wanaume, ukiwa ni mmoja katika michezo 12 mipya iliyoingizwa katika michuano hiyo, ili kuwavutia vijana.

Mwanamke wa kwanza kushinda medali ya dhahabu ni Marit Bjoergen wa Norway,katika mbio za marathon za kilomita 15. Umati mkubwa wa mashabiki wa Uholanzi wanatarajiwa kumshangilia bingwa mtetezi wa mchezo wa kuteleza katika barafu, Sven Kramer, akijaribu kutetea taji lake kwa upande wa wanaume mita elfu tano.

Rais Vladmir Putin wa Urusi alifungua rasmi jana(Ijumaa), mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi katika mji wa utalii wa Sochi katika sherehe zilizofana.

Waliokuwa wanariadha mashuhuri nchini Urusi waliubeba mwenge wa Olimpiki kabla ya kuwashwa na aliyekuwa mlinda lango wa mchezo wa magongo Vladislav Tretiak pamoja na mchoraji wa barafu Irina Rodnina.

Katika siku 16 zijazo,karibia wanariadha 3000 watashiriki katika michezo mbalimbali 98 katika mashindano hayo yaliodaiwa kugharimu takriban dola billioni 50.

Umoja wa Mataifa waahidi misaada Syria

Valerie Amos, mkuu wa shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa

Mkuu wa shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa Valerie Amos amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada ya kimataifa hayatazuiwa kuendelea kutoa misaada nchini Syria kufuatia shambulio la Jumamosi katika msafara uliokuwa ukipeleka vyakula katika mji wa Homs.

Bi Amos amesema amesikitishwa sana na mashambulio hayo ambayo yamevunja makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku tatu ili kuruhusu misaada kupelekwa katika maeneo ya mji wa Homs.

Matukio hayo ni kielelezo cha hatari zinazowakabili kila siku raia na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada nchini Syria, amesema afisa huyo wa Umoja wa Mataifa.

Bi Valerie Amos amesema Umoja wa Mataifa utafanya kila uwezalo katika kufikisha misaada kwa wahitaji, lakini lazima wahakikishiwe usalama.

Msafara wa Umoja wa Mataifa ulishambuliwa kwa makombora na bunduki wakati ukiondoka Homs, Jumamosi, ikiwa ni siku ya pili ya kusitisha mapigano ili kuruhusu misaada kuwafikia watu wanaohitaji.

Serikali ya Syria imevilaumu vikundi vya waasi kutokana na shambulio hilo, lakini nao waasi wamesema majeshi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad yamehusika na shambulio hilo na kuchelewesha shughuli za usambazaji misaada Jumamosi asubuhi.

AY; Diamond ni mtoto mdogo kwangu

NYOTA wa muziki wa Bongo fleva nchini, Ambwene Yesaya ‘AY’, amesema msanii mwenzake, Naseeb Abdul ‘Diamond Platinum’, hawezi kuathiri muziki wake kwani kila mtu ana malengo yake katika fani hiyo.

AY alitoa kauli hiyo kutokana na hisia za wadau wa muziki huo kwamba kung’ara kwa Diamond katika muziki huo, kunaweza kumfunika.

Kupitia mtandao wa Bongo5, AY alisema kila msanii ana mashabiki wake, hivyo hawezi kuhofia uwepo wa Diamond katika tasnia hiyo zaidi anampongeza na kumtakia mafanikio.

“Kila mtu ana malengo na mikakati yake katika kuyafikia mafanikio, hivyo sipo kwa ajili ya kujilinganisha na wengine, ushindani wangu ni dhidi ya yule anayetaka kutengeneza mkwanja mkubwa zaidi yangu,” alisema.

Msanii huyo ni kati ya wasanii ambao wanafanya vizuri kimataifa kutokana na kazi zao kukubalika na kuwavutia mashabiki wa muziki huo hapa nchini.

Ajali ya ua wanafunzi wawili wa CBE

WANAFUNZI wawili wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) wamefariki dunia jijini Dar es Salaam juzi katika ajali ya gari iliyotokea katika viwanja vya Shabaha.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema ilikuwa saa 12 jioni, barabara ya White Sands, Mbezi Beach, baada ya gari lenye namba za usajili T 958 AXK aina ya Carina kuacha njia na kugonga mti.

Kamanda Wambura aliwataja waliofariki dunia eneo la tukio kuwa ni Ibrahim Kaliki (21) mwanafunzi wa CBE Mwanza na Samwel (23) anayesoma CBE Dar es Salaam.

Aliwataja majeruhi wengine katika ajali hiyo kuwa ni Christina Ami (20) mfanyabiashara na Maxon Kimaro (21) mwanafunzi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kamanda Wambura, gari hilo lilikuwa likiendeshwa na George Deo (21), ambaye ni mwanafunzi wa CBE Mwanza, likiwa na abiria watano wakitokea Whitesand Hotel kuelekea Barabara ya Bagamoyo.

Alisema gari lilipofika eneo hilo lilimshinda dereva na kuacha njia kisha kugonga mti, kupinduka na kuingia mtaroni.

Kamanda huyo alisema majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo na maiti zote zimehifadhiwa hospitalini hapo huku Jeshi la Polisi likimshikilia dereva kwa mahojiano na uchunguzi wa ajali hiyo.

Chadema ya itisha CCM

UCHAGUZI wa kata 27 za udiwani unaofanyika nchini leo unatarajia kutoa mwelekeo wa uimara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

CHADEMA ambacho kimeonekana kukipa wakati mgumu CCM, kinaingia katika uchaguzi huo wiki moja baada ya kumaliza Operesheni ya M4C Pamoja Daima, iliyokuwa na lengo la kukiimarisha chama hicho na kutoa elimu juu ya Katiba mpya.

Uchaguzi wa leo pia unatarajia kutoa mwelekeo wa watu wanavyokiunga mkono chama hicho ambacho katika siku za hivi karibuni kiliamua kuwafukuza chamani aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samsom Mwigamba.

Pia CHADEMA ilimvua madaraka yote Naibu Katibu Mkuu (Bara), Zitto Kabwe, ambaye mpaka sasa amefungua kesi mahakamani akizuia uanachama wake usijadiliwe hadi rufaa yake anayokusudia kuikata katika Baraza Kuu la chama hicho.

Operesheni hiyo iliyafikia majimbo 166 na mikutano 206 iliyofanyika ilizua gumzo kubwa ndani na nje ya chama hicho kikuu cha upinzani, huku CCM wakikishutumu kwa kutumia fedha nyingi kukodisha helikopta tatu.

Hata hivyo CHADEMA waliweka wazi kuwa ufanisi wa operesheni hiyo ndilo jambo linalotishia uhai wa CCM ambayo kwa muda mrefu ilizoea kuviona vyama vya upinzani vikifanya harakati za kujiimarisha kila chaguzi zinapokaribia, lakini kwa CHADEMA hali imekuwa tofauti.

Katika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 27 unaofanyika leo CHADEMA wanatetea kata mbili ambazo ni Nyasura iliyoko wilayani Bunda na Kiborloni iliyoko Moshi Mjini, huku zilizobaki ni za CCM.

Kwa upande wa CCM, uchaguzi huo utatoa taswira ya mapokeo ya wananchi juu ya utendaji usioridhisha wa mawaziri waliopachikwa majina ya ‘mizigo’ na viongozi wakuu wa chama hicho katika ziara zao walizofanya mwishoni mwa mwaka jana.

Kamati Kuu ya CCM ilipendekeza baadhi ya mawaziri wawajibishwe kwa kushindwa kuwajibika lakini Rais Jakaya Kikwete alipuuza ushauri huo alipofanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri hivi karibuni.

Kata zinazofanya uchaguzi pamoja na halmashauri zake kwenye mabano ni Segela na Mpwayungu (Chamwino), Ukumbi na Ibumu (Kilolo), Nduli (Iringa), Malindo (Rungwe) na Santilya (Mbeya).

Nyingine ni Tungi (Morogoro), Mkwiti (Tandahimba), Mkongolo (Kigoma), Sombetini (Arusha), Mrijo (Chemba), Magomeni na Kibindu (Bagamoyo), Mtae (Lushoto), Ubagwe (Ushetu) na Namikago (Nachingwea).

Kata nyingine ni Partimbo na Loolera (Kiteto), Kiwalala (Lindi), Kilelema (Buhigwe), Kiomoni (Tanga), Kasanga (Kalambo), Rudewa (Kilosa), Kiborloni (Moshi), Njombe Mjini (Njombe) na Nyasura (Bunda.

CUF watamba

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema chama chake kimejipanga katika maeneo mbalimbali walikosimamisha wagombea na wanatarajia kushinda katika kata husika.

Mtatiro alipuuza kauli iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kuwataka vijana wa chama hicho ‘Green Guards’ kuwa walinde wapiga kura, akisema hiyo ni kazi ya polisi.

CHADEMA

Nao CHADEMA wamesema wana uhakika wa kushinda kata zaidi ya kumi katika uchaguzi huo, huku wakitamba kuwa huko kutakuwa ni kuimega CCM, maana katika uchaguzi huu CCM ilikuwa na kata 25 ambazo leo inatarajia kuzitetea au izipoteze.

Akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya CHADEMA, Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche, alisema chama chake kitashinda kwa kishindo katika kata nyingi na CCM watarajie kushindwa vibaya katika uchaguzi huo.

Alibainisha kuwa alilaani kauli ya Nape, kwa kusema kuwa serikali imeshindwa kuwachukulia hatua viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na wafuasi wao ambao wanafanya kazi ya kuwateka viongozi na wafuasi wa CHADEMA sehemu mbalimbali nchini, hivyo amewataka vijana wa CHADEMA nao kulinda kura leo.

CCM watamba

Chama Cha Mapinduzi kupitia msemaji wake, Nape Nnauye, ameviomba vyombo vya dola na Tume ya Uchaguzi vitende haki.

“Uchaguzi huu sisi tutashinda, takwimu zinaonyesha kuwa tutashinda kata zote, lakini uchaguzi ni uchaguzi tu, sisi tutakubali matokeo yatakayotangazwa, ila tunaomba polisi na Tume ya Uchaguzi watende haki ili matokeo halali ndiyo yatangazwe,” alisema Nape.

Katika chaguzi ndogo zilizofanyika baada ya mwaka 2010, CHADEMA imekuwa ikipanda kwa kasi kwa kushinda katika kata na kupata kura nyingi katika chaguzi za majimbo ziliporudiwa.

Uchaguzi mdogo wa Igunga 2011, matokeo yalikuwa ni CCM kura 26,484 sawa na 47%, CHADEMA kura 23,260 sawa na 41%, CUF kura 2,104 sawa na 4%, AFP 282 sawa na 0.5% .

Wakati wa Uchaguzi Mkuu 2010, CCM Igunga ilipata kura 35,674, CUF kura 11,321, CHADEMA ilikuwa haina mgombea. Mwaka mmoja baadaye ilipata kura 23,260.

Mwaka 2012, matokeo ya uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, CHADEMA ilipata kura za Joshua Nassari 32,972, na kumshinda mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo, Sioi Sumari wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 26,757.

Mwaka 2013, katika uchaguzi mdogo, CCM ilishinda kata 16 dhidi ya 22, CHADEMA ikashinda kata tano, muda mfupi kabla ya CCM kuambulia sifuri katika uchaguzi wa kata nne za Arusha ambazo CHADEMA ilishinda zote.

Uchaguzi huu wa leo, hata kama CHADEMA itapata kata zake mbili na kushinda nyingine moja itakuwa ni pigo kwa CCM, hivyo CHADEMA ikishinda kata nyingi zaidi itakuwa ni pigo kwa CCM, kwani itakuwa inaonyesha kuwa CHADEMA inashamiri na CCM inazidi kunyauka.

Arusha

Uchaguzi wa Kata ya Sombetini wilayani Arusha unatazamiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na aliyekuwa diwani wa eneo hilo, Alphonce Mawazo, kuhamia CHADEMA na aliamua kutogombea.

Uchaguzi huu mdogo unavuta hisia za wakazi wengi wa jiji hili hasa kutokana na ushindani mkali uliopo baina ya wagombea wa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Ally Bananga na yule wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), David Mollel, huku yule wa Chama cha Wananchi (CUF), Ally Mkali, akionekana kuwasindikiza wenzake.

Uchaguzi huu ni kipimo cha kukubaliwa na wananchi kwa vyama vya CHADEMA na CCM ambavyo vimekuwa vikuchuana ikiwa ni takriban miezi sita baada ya kumalizika kwa uchaguzi mdogo ambao CHADEMA waliibuka na ushindi kwenye kata zote nne zilizokuwa zikirudia uchaguzi ambazo ni Elerai, Themi, Kaloleni na Kimandolu.

Mchuano wa CCM na CHADEMA unazidi kuchagizwa na kutafuta kura ya maamuzi kwenye vikao vya baraza la madiwani kwani kwa idadi ya sasa ambayo CHADEMA wana madiwani 15 ndio wenye uwezo wa kufanya maamuzi, kwani CCM wako 14 na TLP wako 2.

Hivyo CHADEMA wakiibuka na ushindi kwenye uchaguzi wa leo ina maana wataendelea kuiongoza halmashauri hiyo kimaamuzi bila kulazimika kutafuta kuungwa mkono na madiwani wa chama kingine katika kupitisha hoja zao.

CCM ambao wana madiwani 14 kwa sasa wanahitaji kuongeza idadi hiyo ya kura ili kuwaongezea nguvu ya maamuzi kwenye vikao vya baraza hilo ambapo wakiwa na idadi sawa na CHADEMA wote watakuwa wakihitaji kuungwa mkono na TLP ili kuweza kupitisha jambo wanalokusudia.

Kampeni za uchaguzi zilitawaliwa na vurugu kiasi cha kuamuliwa njia maalumu zitakazotumiwa na wagombea na wafuasi wa vyama vya CHADEMA na CCM kwa ajili ya kwenda na kurudi kwenye mikutano yao ya kampeni kwani kila wanapokutana hutokea vurugu.

NEC yaonya

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, aliwaonya viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kwenye Kata ya Sombetini kuacha kuchochea vurugu na badala yake wawahamasishe wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura.

Lubuva pia amelitaka Jeshi la Polisi mkoani hapa kutumia utashi na busara watakapokuwa wakiimarisha ulinzi wakati wa zoezi la upigaji kura kwenye kata hiyo ya Sombetini ili kuepuka kuwatisha wapiga kura.

Jaji Lubuva ameahidi kuongea na polisi ili awaombe wachukue tahadhari katika suala zima la kulinda na kuimarisha usalama ili wasitishe wapiga kura.