Tuesday 11 February 2014

Waandishi wa habari waigomea CCM

SIKU moja baada ya kukamatwa, kupigwa na kisha kuporwa vifaa vyake vya kazi, mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi wilayani Bunda, Christopher Malegesi, na kiongozi mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa, Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), kimetangaza kugoma kuandika habari za chama hicho.

Mwenyekiti wa chama hicho, Emanuel Bwimbo, aliiambia Tanzania Daima kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kuona kitendo hicho kimefanyika kwa makusudi.

“Kitendo alichofanyiwa ni cha kinyama na kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 18. Sisi kama chama pia tumeamua kamwe hatutaandika habari za CCM, bali tutaandika maovu yao kama yakijitokeza.

“Kamwe hatutaenda katika ziara zao na wala mikutano yao maana wao ni mabingwa wa kupiga,” alisema Bwimbo.

Alisema kwa muda mrefu waandishi wa habari wamekuwa wakionewa na kupigwa katika mikutano ya CCM huku serikali ikifumbia macho, jambo ambalo limekuwa likiweka chuki kati ya waandishi na chama hicho.

Bwimbo aliwataka watendaji wa serikali likiwemo Jeshi la Polisi na CCM kutambua kuwa taaluma ya habari inatambulika ulimwengu mzima, na kwamba kama CCM wanataka kufanya mchezo basi wataona nguvu ya kalamu.

Awali akizungumzia tukio la kupigwa kwa mwandishi huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ferinandi Mtui, pamoja na kulaani kitendo hicho aliahidi kusimamia suala hilo na kuhakikisha waliofanya hivyo wanafikishwa mahakamani.

No comments: