Tuesday, 11 February 2014

Kocha wa simba asema kuhusu kombe wanasimba wasahau

KOCHA Mkuu wa Simba Zdravko Logarusic amesema kuwa matokeo ya mchezo wao wa juzi dhidi ya Mgambo Shooting, yamezidi kumkatisha tamaa kabisa katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba juzi walijikuta wakipoteza mechi yao hiyo iliyopigwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kwa kukubali kichapo cha bao 1-0.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha huyo alisema hakutegemea kama timu yake ingepoteza pointi tatu katika mchezo huo, ikizingatiwa kuwa taarifa alizonazo kabla ya kuwa kocha wa Simba ni kwamba timu ya Mgambo mechi ya mzunguko wa kwanza walifungwa mabao 6-0.
"Kwa kweli ndoto za kutetea ubingwa wa bara zinazidi kupotea, nasikitika pia kwa jinsi matokeo ya mechi mbili zilizopita jinsi yalivyokuwa, kwa upande wangu imeniuma sana," alisema Loga.
Alisema hata hivyo atazidi kufanyia marekebisho kikosi chake, ili mechi zilizosalia wafanye vizuri hasa mechi ijayo dhidi ya Mbeya City ambayo anaamini itajaa upinzani mkubwa.
Hata hivyo kuna taarifa kuwa kuna hujuma katika timu hiyo na ndiyo maana matokeo yamekuwa mabaya kwa timu hiyo, hali ambayo jana iliwalazimu viongozi wa timu hiyo kukutana na Kocha Mkuu kwa ajili ya kujadili mwenendo wa timu hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa klabu hiyo Aden Rage alipanga kukutana na kocha mkuu, ambapo leo atakutana na wachezaji wote ili kujua nini tatizo mpaka kupelekea kufanya vibaya katika mechi mbili zilizopita.
Pia kuna taarifa kuwa huenda wachezaji hao wakawa katika mgomo baridi, baada ya kudaiwa kuwa walikasirishwa mechi yao na Mtibwa Sugar ambayo walitoka sare kufokewa na kocha wao timu hizo zikiwa mapumziko.

No comments: