MTOTO wa kike mwenye umri wa miaka nane mkazi wa Muungano Tungi Kigamboni, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, amenajisiwa hadi kuzirai, kisha kutelekezwa pembezoni mwa makaburi eneo la Magogoni .
Akizungumzia tukio hilo akiwa hospitalini Temeke anakoendelea na matibabu, huku akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili ikiwa ni pamoja na usoni, mtoto huyo (jina linahifadhiwa) alisema alifanyiwa unyama huo na kijana ambaye hamfahamu.
Alisema wakati akitoka shuleni alitokea kijana huyo akiwa na baiskeli, ambapo alimwambia apande ili amsaidie kumrudisha nyumbani.
Alisema baada ya kupanda baiskeli hiyo kijana huyo alimpeleka eneo ambalo halifahamu na kumfanyia unyama huo. Akizungumzia tukio hilo, mama wa mtoto huyo (jina tunalo) alisema baada ya kuona mtoto anachelewa kurudi nyumbani alitoa taarifa kwa mume wake na ndipo walianza kumtafuta.
Alisema walitoa taarifa Kituo cha Polisi Kigamboni na ilipofika saa 12 jioni mtoto huyo alikutwa na wasamaria wema akiwa amepoteza fahamu eneo la makaburi ya Magogoni ambapo alifikishwa kituo hicho akiwa hajitambui.
Aliongeza kuwa mtoto huyo alipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili, hasa katika paji lake la uso ambapo inaonekana alikwaruzwa na na kucha na kupata jeraha sehemu ya shavuni.
Kwa upande wa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Tungi, Farida Jumbe, alisema hatua mbalimbali zilichukuliwa kumsaidia mtoto huyo kwani baada ya kufikishwa Polisi Kigamboni alipewa PF3 kwa ajili ya kwenda kutibiwa hospitali.
"Hadi sasa anaendelea na matibabu Hospitali ya Temeke," alisema. Naye Ofisa Jamii wa Tungi, alisema mara nyingi matukio kama haya yanaweza kutokea katika maeneo mengi ya vichaka.
Alishauri juhudi zifanyike ili kupunguza vichaka vinavyotumika kufanyia vitendo hivyo.
Juhudi za kumpata Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke kuzungumzia tukio hilo, ziligonga mwamba.
No comments:
Post a Comment