WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira, amemshukia Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema na kudai ndiye chanzo cha vurugu ambazo zinatokea katika mji huo na kuzorotesha soko la utalii kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Bw. Wassira aliyasema hayo juzi katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, Kata ya Nyasura, Jimbo la Bunda, mkoani Mara.
Alisema awali Mji wa Arusha ulisifika kwa kuwa na amani lakini baada ya Uchaguzi Mkuu 2010, Mji huo umepoteza sifa ya kutembelewa na wageni mbalimbali kutokana na siasa za fujo, vurugu na mapigano.
"Wananchi wanapandikizwa chuki dhidi ya Serikali yao, wanasiasa mfano wa akina Lema ndio wanaovuruga amani ya nchi yetu hivyo wakazi wa hapa Nyasura epukeni watu kama hawa," alisema Bw. Wassira.
Alisema hivi sasa kuna njama zinazopangwa na CHADEMA ili vijana wao wakafanye vurugu katika uchaguzi wa udiwani ili kuwatia hofu wanawake na wazee wasijitokeze kumchagua diwani wanayemtaka Februari 9 mwaka huu.
Aliongeza kuwa, vyombo vya usalama vimejipanga kudhibiti fujo hizo na kuwatoa hofu wananchi akiwataka wajitokeze kwa wingi kupiga kura siku hiyo.
"Naomba wananchi mfanye tathmini juu ya siasa zinazofanywa na viongozi wa CHADEMA kwa kulazimisha wananchi kuvunja sheria za nchi, mwanasiasa mzuri anapaswa kutumia nguvu ya ushawishi kwa kujenga hoja si kuchochea chuki, ugomvi na matusi kwa wananchi," alisema.
Alimtuhumu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Bw. Freeman Mbowe na kudai anawapotosha wananchi ili waunge mkono Serikali tatu wakati Katiba Mpya ni ya Watanzania wote.
"Lazima tujadili mfumo wa Muungano wa Serikali mbili kwa kuzingatia maslahi ya Taifa kihistoria, kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama lakini si kwa maslahi ya chama fulani, kama tutaona mfumo wa Serikali tatu haifai kwa nchi yetu ni vyema tukaachana nao," alisisitiza Bw. Wassira.
Alisema Rasimu ya Pili ya Katiba itajadiliwa katika Bunge Maalumu la Katiba na baadaye wananchi watapewa fursa ya kutoa maoni yao na kuwataka wananchi, wajihadhari sana na mfumo wa Serikali tatu.
Operesheni ya CHADEMA
Akizungumzia Operesheni ya Mabadiliko Pamoja Daima inayofanywa na CHADEMA, Bw. Wassira alisema imelenga kuokoa mpasuko wa ndani ya chama chao ambao umeikumba kambi ya Bw. Zitto Kabwe na Bw. Mbowe.
Bw. Wassira alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa, CHADEMA si chama cha kuwatetea wananchi maskini bali wanatumia umaskini wa Watanzania kutaka kuingia Ikulu jambo ambalo linapingwa na wananchi wengi wanaotambua dhamira hiyo.
"Mwanzilishi wa CHADEMA ni Edwin Mtei aliyetofautiana na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, wakati Mwalimu anatetea maskini kwa siasa ya ujamaa na kujitegemea, Mtei alitetea ubepari hivyo Mwalimu akamfukuza serikalini.
"Jambo hili lilimkasirisha Mzee Mtei akaamua kupambana na TANU na hatimaye CCM, leo wanatudanganya kwamba wanawatetea Watanzania maskini," alisema Bw. Wassira.
Alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea wa CCM, katika kata hiyo, Bw. Alexander Mwikwabe akiwataka wananchi watumie vizuri kura zao kumchagua mgombea wao.
No comments:
Post a Comment