VIONGOZI na wanachama wapatao 50 wa Klabu ya Simba, jana wametembelea eneo la mradi wa uwanja wao ulioko Bunju 'B' jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari wa Simba, Asha Muhaji, katika ziara hiyo, wanachama hao walifanya kazi ya kulisafisha eneo hilo kwa kufyeka ikiwa ni hatua za awali za kutaka kuuendeleza, ambalo linakadiriwa kuwa na ekari 25.
Alisema lengo la kufanya ziara pamoja na kusafisha eneo hilo ni mkakati wa klabu hiyo, kutaka kuanza rasmi mipango ya uendelezaji wa eneo hilo.
Asha alisema eneo hilo linatarajiwa kujengwa uwanja wa mpira wa miguu utakaokuwa ukimilikiwa na klabu hiyo, pamoja na majengo mengine muhimu yatakayoendana na sura ya kimichezo.
Msemaji huyo alisema katika hatua za awali, klabu hiyo imepanga kufyeka pamoja na kupitisha greda lengo likiwa ni kusafisha eneo hilo, tayari kwa ujezi wa uwanja utakaoweza kutumiwa na timu yake kwa ajili ya mazoezi na mechi nyingine za kirafiki.
Alisema Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga ameahidi mpaka kufikia Aprili mwaka huu, eneo hilo litakuwa na sura ya kiwanja cha michezo, huku jitihada zingine zikiendelea kufanywa na uongozi kwa ajili ya mradi mkubwa wa kituo hicho, ambacho hapo baadaye utahusisha hosteli ya wachezaji, mgahawa, gym pamoja na bwawa la kuogelea.
Msemaji huyo alisema kwa mujibu wa Katibu huyo, mpango wa awali utahusisha kuzungusha uzio eneo lote, pamoja na ujenzi wa uwanja wa kuchezea mpira.
Kamwaga alisisitiza mradi wa ujenzi mkubwa wa eneo hilo bado unafanyiwa kazi na uongozi wa klabu hiyo, ili kumpata mkandarasi atakayesimamia ujenzi huo na mipango itakapokuwa tayari, itawekwa wazi isipokuwa kwa sasa wanachofanya ni hatua za awali za uendelezaji wa eneo hilo
No comments:
Post a Comment