Tuesday 18 February 2014

Simba waigeukia JKT Ruvu J'pili

BAADA ya kuzoa pointi mbili ugenini, Wekundu wa Msimbazi Simba wamepanga kurudisha matumaini yao mapya katika harakati za kuwania ubingwa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuzoa pointi tatu katika mchezo wao wa Jumapili dhidi ya JKT Ruvu
Simba ilianza kutoa sare ya bao 1-1, na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, ikafungwa na Mgambo Shooting Uwanja wa Kwakwani Tanga na mwishoni mwa wiki ilitoa sare ya bao 1-1 na Mbeya City mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Kufuatia matokeo hayo, Simba wamepanga kurudisha heshima yake Jumapili ijayo watakapocheza na JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zdravko Logarusic alisema matokeo ya mechi ya ugenini yamemsikitisha sana na kufuta ndoto zake za kutwaa ubingwa wa bara, hata hivyo hatakata tamaa na badala yake watahakikisha wanafanya vizuri mechi zote zilizosalia.
"Mechi yetu na Mbeya City ilikuwa tushinde; mechi haikuwa ngumu kama wengi walivyotarajia, tatizo ni uzembe wa washambuliaji wangu ambao walipata nafasi nyingi za wazi za kufunga lakini hawakuzitumia," alisema Loga.
Alisema ana kazi kubwa ya kufanyia marekebisho kikosi chake hasa idara ya ushambuliaji ambako ndiko kwa sasa kuna tatizo, hivyo mechi ijayo dhidi ya JKT Ruvu hataki makosa hayo yajitokeze tena.
Pia kocha huyo aliwataka wachezaji wake kucheza kwa kujiamini na kuacha hofu wawapo uwanjani, endapo watacheza kwa kujiamini watafika mbali ikiwa ni pamoja na kushinda mechi zao zote za Ligi Kuu zilizosalia.
Kocha huyo alisema anaamini kabisa mechi yao ya Jumapili itakuwa ngumu na yenye upinzani mkali, hivyo watajiandaa vya kutosha ili kuhakikisha hawafanyi makosa na kujinyakulia pointi tatu.
Simba wanashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu, vinara ni Azam FC wenye pointi 36 sawa na Mbeya City tofauti ikiwa kwenye mabao ya kufunga na kufungwa, Yanga wana pointi 35 na wanashika nafasi ya tatu.

No comments: