Friday 14 February 2014

Fifa yabariki Okwi kuchezea Yanga

Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), limemaliza utata kwa kumruhusu mshambuliaji Emmanuel Okwi kuitumikia Yanga kama usajili wake umekidhi vigezo.

Yanga ilimsajili Okwi wakati wa usajili wa dirisha dogo, lakini mwanzoni mwa mwezi uliopita, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimsimamisha wakitaka ufafanuzi Fifa baada ya Mganda huyo kuwa na kesi tatu kwenye shirikisho hilo.

Barua ya Fifa iliyotua kwa TFF, ilisema kuwa suala la malipo ya Simba kwa Etoile du Sahel hayahusiani na Okwi kucheza mpira.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliliambia gazeti hili jana kuwa taarifa hiyo ya Fifa imemruhusu mshambuliaji huyo acheze mpira iwapo ametimiza vigezo vyote vya usajili ikiwemo ITC.

“Fifa wametuletea taarifa leo (jana) saa nne asubuhi. Wametaka Okwi aruhusiwe kucheza mpira kama anakidhi vigezo vyote, sasa vigezo ni pamoja na ITC ambayo Okwi anayo, hivyo ni ruksa kucheza mpira.”

Naye Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema aidha Fifa, imeiondoa shaka Simba kwa kuwaambia kuwa kesi yao ya madai ya fedha zao za usajili wa Okwi dhidi ya Etoile haiwezi kuingiliana na masuala ya usajili.

“Tumewajulisha Simba kwamba wasiwe na shaka kwamba kesi yao ya madai ya fedha bado inashugulikiwa na Fifa, wametuahidi watatoa majibu mara baada ya kumaliza taratibu zao. Watulie,” alisema Mwesigwa.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji, Richard Sinamtwa alitoboa siri kwa kudai kuwa Simba ilimwekea pingamizi Fifa mshambuliaji huyo raia wa Uganda asicheze Yanga.

Alisema Simba iliwasilisha pingamizi hilo mwaka jana ikiwa imeandikwa kwa lugha ya Kiswahili ambapo Fifa iliirudisha kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuomba itafsiriwe kwa lugha ya Kiingereza ili waweze kuielewa kwa ufasaha.

“Sisi tulimzuia kwa sababu Simba wamemwekea pingamizi Okwi asicheze Yanga, ndiyo maana tulimsimamisha, usajili wake CAF upo cleared kabisa hauna matatizo yoyote. CAF haijatoa leseni yake kwa vile wanasubiri Fifa itoe hukumu, imehofia isije ikatoa leseni halafu ikajikuta inaingia kwenye mkanganyiko na FIFA,” alisema.

Kwa upande wa Yanga, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Mussa Katabaro, alisema wamezipokea taarifa hizo kwa furaha kubwa, ambapo walikuwa na uhakika wa kile walichokifanya wakati wanamsajili mchezaji huyo.

No comments: