Tuesday 18 February 2014

Onyo la uwezekano wa shambulizi la kigaidi Uganda

Ubalozi wa Marekani Kampala wasema kuna ishara kwamba jumba la makumbusho la kitaifa ni mojawapo ya majengo yanayolengwa na magaidi

Ubalozi wa Marekani nchini Uganda umeonya juu ya uwezekano wa kutokea shambulizi la kigaidi katika mji mkuu wa Kampala.

Katika ujumbe uliotolewa Jumatatu jioni, ubalozi huo ulisema umepata habari kwamba huenda kundi la washambuliaji likiwa tayari kuvamia malengo kadhaa mjini Kampala mwezi Februari na Machi.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa kuna ishara kwamba jumba la makumbusho la kitaifa ni mojawapo ya majengo yanayolengwa. Lakini serikali ya Uganda haijatoa tamko la haraka juu ya onyo hilo.

Ujumbe huo haujawaonya Wamarekani kuondoka Kampala lakini umewatahadharisha kuepuka jumba la makumbusho na maeneo mengine yenye watu wengi.
Kundi la al-Shabab kutoka Somalia lilifanya shambulizi la kigaidi huko Kampala Julai 2010 na kuuwa watu 70.

No comments: