Friday 14 February 2014

Watu 70 wauawa Mashariki mwa Congo-UM

Ndege za umoja zizizokuwa na Rubani Goma
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, umesema kuwa zaidi ya watu sabaini waliuawa mwisho wa mwezi uliopita na mapema mwezi huu.

Katika mahojiano na BBC, afisa mmoja wa shirika la Monusco, mjini Goma, Ray Tores, amesema kuwa ndege ya wanajeshi wake, iliyokuwa ikifanya uchunguzi, katika eneo hilo iligundua kuwa vijiji vitatu viliteketezwa na kuharibiwa kabaisa.

Amesema kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa watazuru eneo hilo baadaye hii leo ili kufanya uchunguzi zaidi.

Jeshi la kutunza amani la Umoja wa Mataifa limeimarisha juhudi zake katika eneo hilo, hasa tangu ilipoisambaratisha kundi la wapiganaji wa waasi wa M23, Novemba mwaka uliopita.

Bwana Torres, amesema kuwa zaidi ya makundi arubaini ya waasi yanajulikana kuendesha operesheni zao katika eneo hio la Goma.

Manne kati yao yamekuwa yakifanya mashambulio ya mara kwa mara na hivyo kuwa tishio kubwa la usalama.

Umoja wa Mataifa, umesema kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na makundi ya waasi yaliyojihami katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, ili kuwatia watu wanaoishi katika eneo hilo hofu.

Afisa huyo amesema kuwa wengi wa waliouawa walikuwa na majeraha ya mapanga.
Wanajeshi wa DRC wakishika doria mjini Goma

No comments: