Tuesday 18 February 2014

Wabunge wanawajibika kuimarisha elimu majimboni?

Hali ya elimu katika maeneo mengi nchini siyo nzuri. Kinachosikitisha ni kuwa baadhi ya maeneo hayo yanasimamiwa na wabunge waliojipambanua kwa uhodari na umahiri wao wa kujenga hoja bungeni.

Kinyume cha matarajio ya wengi, umahiri na umakini wao hasa katika masuala yanayohusu Taifa, vimeshindwa kujiakisi katika utendaji wa kufuatilia sekta ya elimu jimboni mwao.

Wajibu wa wabunge katika elimuKama ulivyo wajibu wa jumla wa wabunge katika kusimamia utendaji wa Serikali, wajibu wa mbunge katika kusimamia maendeleo ya sekta ya elimu unajumuisha mambo kadhaa ikiwamo, kusimamia mgawanyo wa rasilimali za umma kwa kuhakikisha unazingatia viupaumbele na mahitaji ya elimu na kubainisha changamoto za hali ya elimu na kuitaka Serikali kuboresha hali hiyo.

Mambo mengine ni kuwaunganisha wananchi kuainisha na kuzipatia utatuzi changamoto za elimu na kushirikiana na madiwani kusimamia utekelezaji wa mipango ya Halmashauri kwa kuhakikisha inakwenda sambamba na malengo ya mipango husika.

Hali halisi mikoani

Hata hivyo, kuna utafiti mpya unaoonyesha kuwa wabunge wengi wameshindwa kutekeleza wajibu huu, hatua inayosababisha sekta ya elimu kudorora katika maeneo mengi nchini.

Ilivyo ni kuwa uwajibikaji makini wa wabunge katika kusimamia masuala ya maendeleo, ndiyo chachu ya maeneo wanayosimamia kufanya vizuri katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu. Lakini, wabunge wetu wanawajibika ipasavyo?

Utafiti uliofanywa na Shirika la HakiElimu mwaka 2013, umebaini hali isiyoridhisha ya maendeleo ya elimu ya shule za msingi katika baadhi ya mikoa.

Ripoti ya utafiti huo iitwayo Juhudi za Kuboresha Elimu ya Msingi: Je, Mbunge wako anawajibika katika mkoa wako, kwa kiasi kikubwa inahusisha udhaifu uliopo katika elimu na utendaji usioridhisha wa wabunge, inaowasema wana wajibu wa kuisaidia jamii kuboresha elimu.

“Wabunge wana nafasi kubwa sana katika kuleta mapinduzi ya kubadilisha mfumo wa elimu ili kuinua kiwango cha elimu nchini,’’ inasema sehemu ya ripoti ya utafiti huo ambao kwa sehemu kubwa umetumia takwimu zilizomo katika kitabu cha takwimu za elimu msingi kwa mwaka 2012 (BEST -2012).

Takwimu za BEST

Kwa kutumia takwimu hizo za mwaka 2011/12, utafiti wa HakiElimu ulilenga kupima uwajibikaji wa wabunge katika kuimarisha elimu kwa ngazi ya mkoa.
Viashiria kadhaa kuhusu elimu ya msingi vilitumika kupima uwajibikaji, ikiwamo uandikishaji wanafunzi darasa la kwanza, uwiano wa walimu na wanafunzi darasani, uwiano wa darasa kwa wanafunzi, uwiano wa tundu la choo kwa wanafunzi, uhaba wa madawati, ufaulu na idadi ya wahitimu wanaochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.

Makala haya yanatumia uwiano wa tundu la choo kwa wanafunzi, kuonyesha namna baadhi ya mikoa nchini ilivyoshindwa kutimiza lengo la Taifa ambalo ni shule kuwa na uwiano wa tundu moja kwa wanafunzi 25 (1:25)

Mikoa hiyo na uwiano wake kwenye mabano ni kama ifuatavyo; Arusha ( 1:45), Dar es Salaam (1:70), Dodoma (1:62), Iringa (1:42), Kagera (1:60), Kigoma (1:70), Kilimanjaro (1:28), Lindi (1:45), Manyara (1:34), Mara (1:62) Morogoro (1: 53).

Mikoa mingine ni Mbeya (1:52), Mtwara (1:57), Mwanza (1:77), Pwani (1:44), Rukwa (1:51), Ruvuma (1:50), Singida (1:85), Shinyanga (1:77), Tabora (1:69), Tanga (1:49).

Kwa mujibu wa takwimu hizi, mikoa yenye hali mbaya kwa kukosa matundu mengi ya vyoo ni pamoja na Singida, Mwanza, Shinyanga, Kigoma, Dar es Salaam, Tabora, Mara na Kagera.

Baadhi ya mikoa hii ina wabunge machachari na walio na uwezo mkubwa wa kuhoji mambo hasa yanayohusu Taifa. Cha kushangaza wameipa kisogo mikoa yao, kiasi cha shule nyingi za msingi kukosa hata matundu ya vyoo!

Uhaba wa madawati

Kigezo kingine kilichotumika kupima uwajibikaji wa wabunge ni uhaba wa madawati. Ripoti inaonyesha wabunge katika mikoa mingi wameshindwa kuvisimamia vyombo husika kupambana na changamoto tete ya uhaba wa madawati shuleni.

Wakati lengo la Serikali kitaifa ni kuwa na shule ambazo kila mwanafunzi anakaa juu ya dawati, takwimu za BEST zinaonyesha bado katika mikoa mingi wanafunzi wanakaa chini.

Pamoja na rasilimali misitu ikiwamo yenye miti ya mbao, wabunge wameshindwa kuhamasisha mamlaka husika na jamii kwa jumla kulivalia njuga tatizo la uhaba wa madawati shuleni.

No comments: