Tuesday 11 February 2014

Liverpool ya sababisha mauaji Kenya

MWANAMUME raia wa Kenya anayeshabikia klabu ya soka ya Uingereza ya Liverpool amechomwa kisu na mwenzake wa klabu ya Arsenal na kufa katika eneo la Meru Mashariki mwa Kenya.
Kwa mujibu wa polisi wa eneo hilo, wawili hao walianza malumbano baada ya mechi kati ya vilabu hivyo kumalizika hapo Jumamosi.
Kwa mujibu wa BBC, mashabiki hao walikuwa katika baa moja iliyojaa wapenzi wa timu hizo mbili.
Shabiki wa Arsenal anayefanya kazi ya bodaboda alijawa na hasira baada ya timu yake kuzomewa na shabiki wa Liverpool kiasi cha kumchoma mwenzake kisu mara kadhaa, kabla ya kutoweka.
Watu waliokuwa karibu na eneo la tukio, walimsaidia majeruhi aliyetambuliwa kwa jina la Anthony Muteithia na kumpeleka Hospitali Kuu ya Meru, ambapo alifariki wakati akipatiwa matibabu.
Mkuu wa polisi eneo la Meru, Tom Odero, amesema wanamsaka shabiki huyo wa Arsenal ambaye amekwenda mafichoni.

No comments: