Tuesday 11 February 2014

Dk. Maua Daftari ashinda kesi dhidi yake

ALIYEKUWA Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dk. Maua Daftari, ameshinda rufani aliyokata dhidi ya mfanyabiashara Fatuma Salimini Said, aliyetakiwa alipwe sh milioni 100.

Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani linaloongozwa na Jaji Angela Kileo, Sauda Mjasiri na William Mandia.

Jopo hilo lilitengua hukumu ya awali iliyotolewa na Jaji Laurean Kalegeya Julai 9, 2010, iliyomtia hatiani Dk. Maua Daftari na kumtaka alimlipe malamikaji sh milioni 100.

Dk. Daftari ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM, alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani, kupinga Mahakama Kuu iliyomwamuru kumlipa mfanyabiashara huyo sh milioni 100.

Katika kesi ya msingi iliyofunguliwa mwaka 1999 mlalamikaji Fatuma Salimin Said, alikuwa akimlalamikia Dk. Daftari kumtapeli pesa taslimu pamoja na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya sh 200 milioni. Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Fatma alikuwa akimdai Dk. Daftari sh 100,092,400 alizompa ili amnunulie vifaa mbalimbali kati ya mwaka 1994 na 1997, lakini mlalamikiwa hakufanya hivyo.

Vitu hivyo ni pamoja mashine ya kusindika matunda kutoka nchini Afrika Kusini, king’amuzi kutoka Uingereza, magari na pesa.

Hata hivyo majaji wa Mahakama ya Rufani walisema baada ya kupitia hukumu iliyotolewa na Jaji Kalegeya, hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu suala linalolalamikiwa.

Majaji hao walisema wamekosa ushahidi wa kumtia hatiani mkata rufaa huyo Dk. Maua Daftari, hakukuwa na ushahidi wowote kuonyesha kuwa kiasi hicho cha sh milioni 100 kilipita kati ya mikono ya Fatuma Salmini kwenda kwa Maua Daftari.

Walisema walitaka swali la msingi lijibiwe kuonyesha ushahidi usiotiliwa shaka kuonyesha kama kweli mlalamikaji alimpa mlalamikiwa kiasi hicho cha fedha ambapo ilionekana kuwa mlalamikaji alilipa kiasi hicho cha fedha kwa njia ya hundi kupitia akaunti iliyokuwa haina fedha ya kiwango kinachotajwa, isipokuwa mlalamika aliegemea zaidi ushahidi wa mtu mmoja anayesadikiwa ndiye aliyepeleka hundi hiyo.

Kwa mujibu wa majaji, akaunti hiyo haikuwa na fedha, ndio maana hundi hiyo haikuheshimiwa ili malipo halali yafanyike.

Awali wakili wa mkata rufaa, Peter Swai, alidai Mahakama Kuu haikutenda haki kumhukumu Daftari kulipa kiasi hicho cha fedha.

Akizungumza na Tanzania Daima, Dk. Daftari alisema amefurahia uamuzi huo kwakuwa hakuna baya lolote alilofanya kwa mfanyabiashara Fatuma Salimini Said.

No comments: