Familia za zaidi ya watu 300 zimenusurika vifo wilayani Mwanga baada ya mvua iliyoambatana na upepo kuezua mapaa ya nyumba zao 110 .
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga aliliambia gazeti hili jana kuwa hali katika eneo hilo ni mbaya.
Ndemanga alisema mvua hiyo ilinyesha juzi kati ya saa 10:30 na saa 11:30 jioni na kuezua mapaa ya nyumba hizo katika Kata mbili za Mwaniko na Kifula.
“Upepo hasa ulioleta madhara ulivuma kwa dakika kama tano tu hivi japo mvua ya upepo ilinyesha kwa saa moja.... Nimetoka huko hali ni mbaya,”alisema.
Ndemanga alisema upepo huo uliezua paa za nyumba 44 katika Kata ya Mwaniko na nyumba 64 katika Kata ya Kifula huku maelfu ya ekari za migomba zikiwa zimeathiriwa vibaya.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, upepo huo umeezua mapaa ya madarasa saba ya Shule ya Msingi Mangio, ofisi ya walimu na choo cha wanafunzi.
“Kutokana na athari za maafa hayo ni wanafunzi wa darasa la saba, sita na nne tu ndio watakaoendelea na masomo na wengine watabaki nyumbani,”alisema.
Ndemanga alifafanua kuwa, leo wataalamu wa ujenzi watapiga kambi katika shule hiyo kuhakikisha inarejea katika hali yake ya kawaida ndani ya siku saba.
Alisema familia ambazo zimekumbwa na maafa hayo zenye watu wasiopungua 300 zimepatiwa hifadhi na ndugu wakati serikali ikiwa katika harakati za kufanya tathmini ya haraka ili kubaini uharibifu huo..
“Ni hali ya kutisha, lakini mpaka sasa hakuna taarifa za vifo licha ya nyumba mbili kubomoka kabisa....kwa kweli tunamshukuru Mungu kuwa hakuna madhara zaidi ambayo yamejitokeza hadi sasa,” alisema.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo ametuma salamu za pole kwa waathirika wa maafa hayo yaliyotokana na mvua kubwa .
Ndesamburo ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Mjini, kupitia Chadema, leo atafanya ziara katika wilaya hiyo ambapo pamoja na mambo mengine kujionea athari za maafa hayo.
“Kesho (leo) Ndesamburo atafika Mwanga na baada ya kujionea hali halisi ndio atatoa tamko rasmi” alisema Basil Lema, Katibu wa Chadema mkoa.
No comments:
Post a Comment