Tuesday, 18 February 2014

Kili Music Awards 2014 yazinduliwa

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), ambao ni wadhamini wa Tuzo za Muziki za Kilimanjaro (KTMA), jana imezindua rasmi kinyang’anyiro cha tuzo hizo mwaka huu, huku ikiondoa kipengele kimoja na kufanya marekebisho kadhaa ya majina kwa baadhi ya tuzo.

Kati ya marekebisho hayo ni kukabidhi kwa wadau na mashabiki wa muziki nchini mchakato wa kupiga kura za kupendekeza washiriki kwa kila kipengele, tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita ambako mashabiki waliwapigia kura wateule.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema tuzo zitakazotolewa katika fainali ya shindano hilo Mei 3 ni 36, badala ya 37 kama ilivyokuwa mwaka jana, ambako Tuzo ya Mtayarishaji Bora Anayechipukia imeondolewa kwa mapendekezo ya wadau.

Alisema kwa mwaka huu wamerudisha uamuzi kwa wananchi ambao ndio watakaopendekeza majina ya wasanii watakaopenda waingie katika kinyang’anyiro hicho, kabla ya baadaye kuwapigia kura za nani awe mshindi katika kila kipengele.

“Majina ya wasanii, bendi, watayarishaji na washindani wengine yatapitishwa kwa kupigiwa kura na mashabiki kwa kutumia tovuti ya www.kilitime.co.tz/ktma, kuponi za magazeti, barua pepe na simu za kiganjani kwa kutuma ujumbe mfupi kwenda namba 15440, ” alisema Kavishe.

Aliongeza kuwa baada ya mashabiki kupitisha majina hayo, yatapelekwa katika kundi la wana ‘Academy’ watakaokaa na kuhakiki majina ya wasanii ambayo yamependekezwa kama yanakidhi vigezo na masharti na kuweka sawa.

Akielezea sababu za kukiondoa kipengele cha Mtayarishaji Bora wa Mwaka, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza, alisema ni kutokana na kukosekana kwa ujio wa watayarishaji wapya, hivyo kujirudia kwa majina ya washiriki, huku wapya wengi wakiwa hawajasajiliwa katika Baraza hilo.

Naye Mratibu wa tuzo hizo zinazoratibiwa na Basata, Kurwijira Ng’oko, alitoa msisitizo kwa watayarishaji na wasanii, kujisajili mapema, la sivyo ataishia kutangazwa na hatapokea tuzo hizo kama atashinda Mei 3.

No comments: