Monday 3 February 2014

Mkenya mbaroni kwa cocaine

Raia wa Kenya anayeishi Mombasa, AbdulRahman Salim, amekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) akiwa na kete 141 za dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani zaidi ya Sh119 milioni.

Salim alikamatwa kwenye uwanja huo akitokeaa nchini Brazil na kisha kupitia nchi ya Ethiophia akiwa amepanda ndege ya Shirika la Ndege ya Ethiophia kuja nchini, ili aelekee Mombasa nchini Kenya.

Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya Kamanda, Alfred Nzowa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 31 mwaka huu saa 7 usiku akiwa uwanja wa ndege huo.

Alisema askari polisi wa uwanja huo walimshuku kuwa amemeza dawa za kulevya na kumweka chini ya ulinzi ambapo aliweza kutoa kete hizo.

Nzowa alisema baada ya kumpekuwa walikuta hati ya kusafiria yenye namba A2092241 iliyotolewa Novemba 8 mwaka 2013. Alisema walipomuhoji mtuhumiwa huyo alikuwa anaelekea mkoani Tanga kwa wakwe zake kwa kutumia usafiri wa mabasi na baadaye kwenda Mombasa.

Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa na mpango wa kupanda basi kuelekea Mombasa ambapo kutumia njia hiyo ni kuvikwepa vyombo vya dola.

“Mtuhumiwa Salim anaishi Mombasa amevunja rekodi ya kutoa kete nyingi ambazo ni 141 na hadi hivi sasa bado anaendelea kuzitoa akifuatiwa na Khadija Omari aliyekamatwa hivi karibuni alitoa kete 126,” alisema.

No comments: