BASI tena. Hakuna jinsi. Huu ni mwisho wetu. Mchezaji mmoja muhimu katika kikosi cha Manchester United amekiri kwamba mabao matatu ya mshambuliaji Samuel Eto’o yamehitimisha matumaini yao ya kutetea taji lao msimu huu.
Nemanja Vidic, nahodha ambaye juzi Jumapili
alitolewa kwa kadi nyekundu katika pambano dhidi ya Chelsea huku
akishuhudia timu yake ikichapwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Stamford
Bridge amedai kwamba hawana tena matumaini ya ubingwa.
Kipigo hicho kimeiacha United nyuma ya viongozi wa
ligi hiyo Arsenal kwa pointi 14 na imeendelea kushikilia nafasi ya saba
katika msimamo huku matumaini ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao
yakiwa shakani.
Staa huyo wa kimataifa wa Serbia anaamini kwamba
pengo lililopo kati yao na Arsenal pamoja na wanaoshika nafasi ya pili
na ya tatu ni kubwa.
“Tuko nyuma sana na sasa itabidi tujikite katika
kusaka nafasi tatu au nne za juu. Inabidi tujitahidi kwa kweli. (dhidi
ya Chelsea) Hatukucheza vibaya. Walipiga mashuti matatu langoni na
kufunga mabao matatu na hiyo ndiyo ilikuwa tofauti ya mechi. Tumekuwa
tukiadhibiwa kila wiki kutokana na makosa hayo.” Alisema Vidic.
“Haitakuwa rahisi. Inabidi tupigane sana kupata
nafasi ya Ligi ya Mabingwa. Inabidi tujiamini na kuwa pamoja huku
tukifanya kazi ngumu. Tukipata bahati nadhani tutafanikiwa katika hilo,”
alisema mkongwe huyo.
Hata hivyo, kocha wake, David Moyes aliibishia
kauli ya Vidic huku akisema kwamba timu yake bado iko katika mbio za
ubingwa licha ya kipigo hicho cha mabao ya Eto’o.
Pamoja na kipigo hicho, Vidic amekataa kumlaumu
kocha wake huku akidai kwamba wachezaji wamechoshwa kumjadili kocha wao
ambaye kwa sasa yupo matatizoni.
“Hatuwezi kila siku tukawa tunaongea kuhusu
makocha. Wachezaji wamechoshwa kuongelea hilo kwa sababu kocha
anajitahidi kwa uwezo wake wote. Kwa mbinu leo tumefanya vizuri sana.”
Nemanja pia amekerwa na uamuzi wa mwamuzi kumtoa
nje kwa kadi nyekundu kwa rafu yake kwa Eden Hazard ambayo itasababisha
akae nje katika pambano la pili la nusu fainali dhidi ya Sunderland
Jumatano usiku.
“Hisia zangu ni kwamba ile ilikuwa ovyo kwa sababu
nilikwenda kwa ajili ya mpira. Tunajua kuwa Hazard ni mchezaji mwepesi
na aliusukuma mpira mbele. Kwa mtazamo wangu haikuwa kadi nyekundu na niliudhika kwa uamuzi ule.”
No comments:
Post a Comment