Thursday 13 February 2014

Kesi ya Zitto dhidi ya Chadema kutajwa leo Mahakama Kuu Dar es salaam

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe .

Kesi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe dhidi ya chama chake hicho inatarajiwa kuanza kutajwa leo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alifungua kesi hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema, akiiomba mahakama hiyo ikizuie chama kujadili uanachama wake, hadi rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama kupinga kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.

Katika kesi hiyo namba 1 ya 2014, Zitto pia aliiomba mahakama hiyo imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilichomvua nyadhifa zote alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini.

Kesi hiyo ambayo inasikilizwa na Jaji John Utamwa imepangwa kuanza kutajwa leo kabla ya kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa rasmi.

Tayari mahakama imeshatoa amri ya zuio la muda kwa Chadema kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.

Uamuzi huo ulitolewa Januari 7 na Jaji Utamwa, kutokana na maombi ya Zitto, kupitia kwa Wakili wake Albert Msando.

Awali mawakili wa Chadema, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na Mkurugenzi wake wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya kupewa zuio la muda.

Katika uamuzi wake, Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa zuio hilo.

No comments: