Katika Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara lipo shimo la ajabu lijulikanalo kama ‘Shimo la Mungu’ lililochukua robo tatu ya ukubwa wa wilaya hiyo.
Shimo hili linalotajwa kuwa moja ya vivutio mkoani Mtwara limesheheni hifadhi za misitu, mito, mabonde, mawe ambayo yanapendeza kwa macho pia kipo kisima cha maji Newala.
Jambo hili linawasumbua wale wanaojua historia yake ni taarifa za kutupwa kwa watoto, kupotea kwa watu wale wanaojaribu kuingia bila ruhusu, wabishi wasioamini tambiko na mambo mengine kadhaa ambayo hata hivyo ni vigumu kuyathibitisha.
Ni shimo la asili ambalo limekuwapo miaka mingi, na wenyeji wa Mji wa Newala wanaliita ‘Shimo la Mungu’ kutokana na kile wanachoeleza kuwa ni maajabu ambayo hutokea yakianzia katika shimo hilo.
Miongoni mwa maajabu hayo ni yale ambayo hutokea nyakati za asubuhi kipindi cha masika ambapo upepo mkali sana huvuma kutoka lilipo shimo hilo.
Wanasema wakati mwingine hutokea moshi mzito ambao husambaa na kuufunika Mji wa Newala na kusababisha giza nene katika makazi ya watu kiasi cha watu kushindwa kuonana kwa kati ya dakika tatu na dakika saba.
Mkazi wa Newala, Sophia Saidi (90) anasema: “Sisi tumezaliwa tumelikuta, kutokana na shimo hilo kutotengenezwa na mtu yeyote ndio maana tukaliita ‘Shimo la Mungu”.
Bibi Sophia kama anavyojulikana na wengine anasema anaongeza: “Sehemu hiyo huwa panatokea miujiza kama hiyo ambayo inaleta upepo mkali, mara giza hata sisi hatujuwi ni nani ambaye ana sababisha kuwe na giza kutoka sehemu ya shimo hilo hadi sehemu ya makazi ya watu”.
Kutokana na umaarufu wake, eneo hilo limekuwa kivutio kikubwa cha watu ambao hufika kwa ajili ya kufanya matambiko ya jadi, ikiwa ni sehemu ya mila na desturi za wakazi wa Newala na wilaya nyingine jirani.
Maimuna Pinda (55) ambaye pia ni mwenyeji wa eneo hilo anasema hata waganga wa jadi kuingia na kutoka ndani ya ‘Shimo la Mungu’ kwa ajili ya kuchukua dawa mbalimbali za miti shamba ambazo hutumika kutibia magonjwa kadhaa. Pinda anasema kabla ya mtu hajaingia ndani ya shimo hilo ili kutalii au kuchukua dawa, lazima afanywe tambiko.
Pembezoni mwa shimo hilo huota uyoga ambao ni kitoweo kwa wakazi wanaolizunguka, lakini kwa maelezo ya wenyeji uchumaji huo huwa ni hatari kwani mara kadhaa watu wamepoteza maisha kutokana na kupatwa na kizunguzungu kisha kutumbukia kwenye shimo.
Kivutio kingine kuhusu ‘Shimo la Mungu’ ni madai ambayo yamekuwa yakitolewa kwamba ndege haziwezi kuruka juu yake kutokana na kuwamo kwa mvutano wa asili hivyo kuwa kikwazo cha usafiri wa anga.
Mkazi mwnigine na Newala, Said Omary (54) anasema: “Newala tuliwahi kuwa na uwanja wa ndege zamani ambao ulikuwa unajulikana kama Uwanja wa Nangwanda na ulikuwa karibu na makazi ya watu”.
Aliongeza: “Wakati zilipokuwa zikiruka, zilikuwa zikielekea sehemu ya shimo hilo na kuna habari kwamba ndege mbili zimewahi kuangukia kwenye shimo hilo ndio maana wakaamua kuhamisha kiwanja hicho katika kijiji cha Mtangalanga kati ya Makonga eneo lililopo mbali na makazi ya watu.”
Hata hivyo mmoja wa waongoza ndege mkoani Mtwara, Emmanuel Wanje alisema hakuna kumbukumbu za matukio hayo na kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yanapotokea kwa haraka husababisha ndege kushindwa kuruka kwenda juu kutokana na mvutano uliyopo kwenye ardhi.
“Sababu ambazo zinazofanya ndege kushindwa kuruka angani ziko mbili ni (winds shear pamoja na Ant- Mosipheric Pressure) upepo unazunguka kwenda juu ukajikusanya kama kibunga husababisha ndege kuwa katika hali isiyo ya kawaida husababisha kukosa mweleko na hatimaye kuanguka,” alisema Wanje.
Wanje alisema wakati ndege zinapokuwa katika harakati za kutua hutegemea Ant-Mosipherec Pressure na kwamba wakati huo ndege hutumia mafuta mengi, kama ilivyo wakati wa kupaa.
Hazina ya Utamaduni
Wakazi wa Newala wanalitizama ‘Shimo la Mungu’ kama hazina ya mila, desturi na utamaduni wa wakazi wa Mikoa ya Kusini inayojumuisha makabila makubwa matatu; Wayao, Wamakua na Wamakonde.
Katika shimo hilo ndiko wakazi hawa wanakopata miti kwa ajili ya kudumisha utamaduni wao wa kuchonga vinyago vya mapambo ya vyombo mbalimbali, ambavyo husambazwa ndani na nje ya nchi, asili yake ikiwa ni mkoani Mtwara.
Mkazi wa Newala Rashidi Ramadhani anasema: “Sisi watu wa Kusini tunapenda sana utamaduni wetu na bado tunauendeleza mfano kila mwaka tunafanya maonesho ya michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ngoma za asili ambazo huashilia kuendelea kudumisha mila na desturi za mkoa wetu.”
Kutokana na umuhimu huyo wananchi wa Newala wanasema Serikali inapaswa kuweka ulinzi kwenye eneo hilo ili kutunza uoto wa asili kwani watu wasiofahamu umuhimu wake hukata miti ovyo pembezoni na ndani ya shimo hilo kwa matumizi mbalimbali hasa kuchoma mkaa.
“Tungependa misitu ibaki kama ilivyo ili itumike kwa ajili ya maombi kwa wenyeji na wageni. Watu inabidi waheshimu sehemu hiyo ambayo inaheshimiwa na kila mtu, wageni kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huu huja kufanya maombi hivyo watu waache kwenda hovyo kwenye shimo hilo kutokana na majabu yanayojitokeza tokea enzi na enzi,” alisema Pinda.
Ofisa Utamaduni wa Wilaya ya Newala, Pontian Mutegeya anasema shimo hilo lipo katika hifadhi ya Mlima Makonde na kwamba muda si mrefu wanategemea liwe ni eneo la hifadhi kwani watu mbalimbali wamekuwa wakifika kwa ajili ya kufanya tafiti.
“Sasa Idara ya Ardhi imepima viwanja vinne karibu na shimo, tunarajia kujenga hoteli za kitalii ambazo zitakuwa ni kivutio kwa wageni kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Tanzania,”anasema Mutegeya.
Alisema elimu ikitolewa ipasavyo, ‘Shimo la Mungu’ linaweza kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa ndani na nje ya nchi, kwani limesheheni hazina ya hisotria ya mambo ya kale hasa kwa miko ya Kusini.
Maliasili Mtwara
Mkoa wa Mtwara unajivunia maeneo mengi kuwa ya uoto wa asili na sehemu kubwa ya maeneo hayo bado yanatunzwa na wazee wanaojua asili yake.
Ofisa Wanyamapori wa mkoa huo, Richard Katondo anasema misitu inachukua asilimia 42.4 ya mkoa mzima na kati ya hiyo asilimia 93.7 inahifadhiwa na Serikali Kuu.
Katondo anasema zinafanywa jitihada za kutangaza vivutio vilivyopo mkoani humo likiwamo ‘Shimo la Mungu’ pamoja maajabu mengine katika Wilaya za Masasi na Nanyumbu.
“Nasema hivyo kwani hifadhi hizo bado hazijajengewa uwezo wa kuingiza pato ndani ya mkoa ila ni hifadhi ambazo zikiangaliwa na kuandaliwa vizuri zinaweza kuokoa wilaya husika na mkoa kwa ujumla kwa kuingiza mapatao makubwa na fedha nyingi za kigeni,” alisema Katondo.
No comments:
Post a Comment