Monday, 3 February 2014

Logarusc atetea uamuzi wake wa kuwatoa wachezaji watatu kwa mpigo

KOCHA Mkuu wa Simba, Zredvo Logarusc 'Loga' ametetea uamuzi wake wa kuwatoa wachezaji wake watatu kwa mpigo katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya JKT Oljoro iliyochezwa juzi uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji waliotolewa na kocha huyo katika kipindi cha pili ni Ramadhan Singano 'Messi', Amri Kiemba na Amis Tambwe, akawaingiza Uhuru Suleiman, Said Ndemla pamoja na Abdulhalim Humud.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Loga alisema kuna wakati analazimika kujitoa mhanga ili kuwalinda wachezaji wengine kwa ajili ya kuboresha mechi zijazo.
Akielezea sababu zilizomsababisha kufanya uamuzi huo, alisema aliamua kumtoa Messi kwani tayari alikuwa ana kadi mbili za njano na alishacheza kiwango cha kuridhisha hivyo aliona kuna sababu ya kumtoa, ili kumlinda na madhara ya kupewa kadi nyingine, kwani bado anahitajika kuendelea kucheza mechi kubwa zijazo.
"Kuna wakati mimi kama Kocha nalazimika nijitoe mhanga, ili mambo mengine kwenye timu yaendelee kuwa mazuri, nimemtoa Messi kama unavyojua ana kadi mbili za njano, hivyo lingeweza kutokea lolote ambalo pengine lingeleta madhara makubwa kwenye timu na bado tuna mechi kubwa zinatusubiri," alisema Loga.
Alisema kwa upande wa Kiemba, aliamua kumpuzisha kwa wakati huo ili kumlinda asije kuumia kwenye kipindi hicho cha pili kwani bado ananafasi kubwa ya kuendelea kucheza kwenye mechi zijazo, ambazo anaamini hizo ndiyo mechi kubwa zaidi.
Kocha huyo alisema alikuwa na kila sababu ya kumtoa, Tambwe kwani alishacheza kiwango cha kuridhisha hivyo alifanya hivyo pia, ili asiumie na aweze kuendelea kucheza mechi ijayo.

No comments: