Monday, 24 February 2014

J k; Misri tuko nyuma yenu

RAIS Jakaya Kikwete, ameihakikishia nchi ya Misri kuwa Tanzania itaunga mkono jitihada za nchi hiyo kurejeshewa uanachama wake katika Umoja wa Afrika (AU), baada ya nchi hiyo kufanya Uchaguzi Mkuu wa kidemokrasia Aprili mwaka huu.
Alisema kwa mujibu wa makubaliano ya uanzishwaji wa AU, itakuwa vigumu kwa nchi hiyo kurejeshewa uanachama wake katika mazingira ya sasa.
Rais Kikwete aliyasema hayo jijini Dar es Salaam juzi baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Bw. Nabil Fahmy ambaye aliwasilisha ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa muda wa Misri, Adly Mansour.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Fahmy aliiomba Tanzania kuunga mkono jitihada za Misri kurejeshewa uanachama wake AU ambao umesitishwa baada ya kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa nchi hiyo aliyekuwa amechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, Bw. Mohamed Morsi mwaka 2013.
Akitoa msimamo wa Tanzania kuhusu matumizi ya maji ya Mto Nile, Rais Kikwete alisema nchi zote ambazo mto huo umepita kwa namna moja ama nyingine, zina haki sawa ya kutumia maji yake kwa maendeleo ya nchi hizo.
"Tunaamini nchi zote ambazo mto huu unapita zina haki ya kutumia maji, haki ya aina hii ndiyo inayotumika hata Tanzania kulingana na matumizi ya maji kwenye mito mbalimbali ndani ya nchi yetu," alisisitiza Rais Kikwete.
Mapema Bw. Fahmy alimwambia Rais Kikwete kuhusu umuhimu wa maji ya mto huo kwa Misri akisema kuwa; "Sisi katika Misri, hupata mvua siku tatu kwa wastani katika mwaka.
"Maji yote tunayotumia yanatokana na Mto Nile hivyo unaweza kuelewa umuhimu wa mto huo kwa uhaki na ustawi wa nchi yetu," alisema.
Rais Kikwete aliishukuru Serikali ya Misri kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania na kuunga mkono jitihada hizo kwa kutoa misaada katika sekta mbalimbali na hasa za maji na afya.
Bw. Fahmy alikuwa nchini kwa ziara ya siku tatu ambapo jana amerejea nchini kwao.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete juzi aliongoza harambee ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya matibabu kwa ajili ya wodi ya watoto katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar es Salaam.
Katika harambee hiyo, zaidi ya sh. milioni 602 zilipatikana wakati lengo lilikuwa kukusanya sh. bilioni moja. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wastaafu akiwemo Rais wa Pili wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Tatu za Tanzania, Mzee Benjamin Mkapa kama walezi wa Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania (PAT).
Katika halfa hiyo, Ikulu ya Rais Kikwete imetoa mchango wa kununua mashine iitwayo Infant Radiant Warmer yenye thamani ya dola za Marekani 15,300.
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA ) inayoongozwa na Mama Salma Kikwete imechangia ununuzi wa mashine iitwayo Compressor Nebulizer ambayo gharama yake ni dola za Marekani 12,000.

No comments: