Sunday, 11 May 2014

Polisi wakurupushana na Machinga Kariako

Mitaa ya Kariakoo imegeuka kuwa uwanja wa  mapambano baada ya polisi na wafanyabiashara ndogo ndogo, kushambuliana kwa mawe na mabomu ya machozi.
 Hali hiyo ilitokea juzi saa 11 jioni ambapo Mwananchi ilishuhudia wafanyabiashara wakitaharuki na kufunga maduka yao hasa baada ya sauti ya milipuko ya mabomu ya machozi kusikika.
Mapambano hayo yalizuka baada ya kijana ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja kumvamia na kumkaba askari polisi mmoja aliyekuwa katika kikosi kazi kinachotekeleza operesheni ya kuwaondoa wamachinga hao katika maeneo yasiyoruhusiwa kufanya biashara.
Kitendo cha kijana huyo kilisababisha polisi wengine kuingilia kati na kupambana naye ambapo hata hivyo alimwachia askari huyo akiwa amekata vifungo vya shati lake huku wanachinga wengine wakiamua kurusha mawe ili kupambana. 
Msimamizi Mkuu wa Operesheni hiyo wa Manispaa ya Ilala, Charles Wambura alisema ni changamoto kubwa waliyokutana nayo ingawa haiwezi kuwarudisha nyuma katika harakati zao za kuwaondoa wafanyabiashara hao katika maeneo yasiyoruhusiwa pamoja na kuweka jiji katika hali ya usafi.
Mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Ester Joshua alisema operesheni hiyo iwe ni ya kudumu, ili kuwawezesha wafanye biashara zao katika hali ya amani na  kujipatia kipato.
“Jiji wamekuwa wakifanya operesheni za namna hii kisha hujisahau ingawa sasa kuna tofauti ni vyema wasiache,” alisema Ester.

No comments: