WENYEVITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka
mikoa ya Geita, Simiyu, Kagera na Mwanza, wamekanusha taarifa
zilizotolewa juzi na vyombo vya habari zikipinga chama hicho kujiunga
na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Katika taarifa ya pamoja kwa waandishi wa habari mara baada ya kikao
chao cha dharura kilichofanyika katika Hoteli ya Vizano jijini Mwanza,
wenyeviti hao walisema hawamtambui mtu huyo aliyejiita Mwenyekiti wa
Makatibu Mabaraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Fikiri Migiyo.
Walisema kuwa kuonyesha kuwa mtu huyo sio kiongozi na wala hajui
mfumo wa utendaji ndani ya CHADEMA, waraka huo umeonyesha kuwa Mkoa wa
Simiyu uko katika Kanda ya Ziwa wakati sio kweli.
“Mkoa wa Simiyu umo katika Kanda ya Mashariki, tofauti na
alivyodanganya Migiyo, hivyo hatuko tayari kuacha watu aina ya Migiyo
kuendelea kukichafua chama na viongozi wake,” walisema wenyeviti hao
katika taarifa yao.
Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, alisema kutokana na tukio hilo, wameanza kuendesha uchunguzi kumsaka mtu huyo.
Aliongeza kuwa wanafanya mawasiliano na wanasheria wa CHADEMA, kuona
hatua watakazochukua dhidi ya vyombo vya habari vilivyochapisha
habari hizo bila kupata ufafanuzi kutoka kwa viongozi wa mikoa na taifa
kama maadili ya kihabari yanavyosisitiza.
“Hakuna sehemu yoyote ambapo sisi wenyeviti wa CHADEMA kutoka mikoa
ya Kanda ya Ziwa tumeketi na tukapinga viongozi waandamizi wa kitaifa
kujiunga na UKAWA. Hilo sio tamko letu.
“Tumekagua kwenye kumbukumbu za chama tukabaini hatuna mwanachama
wala kiongozi katika ngazi yoyote anayeitwa Fikiri Migiyo.
“Hivyo, hawa waandishi walishindwa nini kuwasiliana na uongozi wa
juu, na walikuwa na uhakika gani kwamba waliyeongea naye huko Geita ni
kiongozi ama msemaji kwa mujibu wa katiba yetu” alisema Mawazo.
Walisema habari zilizoandikwa na magazeti hayo (sio Tanzania Daima)
Mei 22, 2014 zikiwa na kichwa cha habari ‘Mbowe, Slaa wapewa siku 14
kujitoa UKAWA’ zililenga kuleta mpasuko ndani ya chama na kwa vyama vya
upinzani.
Nalo Baraza la Vijana wa CHADEMA mkoani Geita, limeitaka jamii
kupuuza habari hizo ilizoziita za kizushi kwa kuwa mkoa hauna katibu
mwenye jina hilo.
Baraza hilo limedai kuwa huenda waraka huo umeandikwa na wanasiasa
uchwara baada ya kuona nguvu kubwa ya UKAWA inayoungwa mkono na
Watanzania wengi.
No comments:
Post a Comment