WAGONGA Nyundo wa jijini Mbeya, Mbeya City fc jana walitoka kushinda mabao 3-2 dhidi ya Academie Tchite ya Burundi katika
mchezo wa kundi B wa michuano ya CECAFA Nile Basin Cup inayoendelea
mjini Khartoum nchini Sudan.
Mbeya City fc waliofika Khartoum
siku moja kabla ya mechi walianza kufungwa bao katika dakika ya 10 baada
ya Rashid kumtungua kipa wao, lakini walirudi mchezoni baada ya Paul
Nonga kusawazisha bao hilo dakika 5 baadaye.
Dakika ya 27, nahodha wa Mbeya
City fc, Mwegane Yeya kama ilivyo kawaida yake alifunga bao la pili kwa
njia ya kichwa. Them Felix `Mnyama` alihitimisha karamu ya mabao dakika
ya 37 baada ya kufunga bao safi na kuwapeleka Mbeya City mapumziko
wakiwa na furaha.
Kipindi cha pili, Waburundi walikuja na Presha kubwa na katika dakika ya 68 Manirakiza alifunga bao la pili.
Kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi aliwapongeza vijana wake kwa ushindi na kuahidi kufanya vizuri mchezo unafuata.
“Vijana walipunguza kasi kipindi cha pili, lakini nawasifu kwa kuvuna pointi tatu muhimu”. Alisema Mwambusi.
Mpinzani wake, Ndayizeye Jimmy aliwapongeza Mbeya City kwa soka safi.
Wafungaji wa mabao: Academie Tchite: (Rashid Patient-10’, Manirakiza 68’).
Mbeya City: (Nonga paul-15’, Mwagane Yeya 27’ and Themy Felix 37’).
Mchezo mwingine ulipigwa kuanzia
majira ya saa 2:00 usiku na kushuhudia AFC Leopard ya Kenya ikiibuka na
ushindi mabao 2-0 dhidi ya Etincelles.
No comments:
Post a Comment