MBUNGE
wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), ameuweka rehani ubunge wake kwa
kutishia kujiuzulu endapo Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Titus
Kamani ataonyesha fedha alizotenga kwa ajili ya ruzuku ya wavuvi.
Sambamba na hilo, Lugola alisema kuwa ataandika hundi ya sh milioni
50 endapo waziri huyo ataonyesha mahala alipotenga fedha hizo kwa ruzuku
kwa wavuvi.
Lugola alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia mjadala wa hotuba ya
makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha
2014/2015.
Huku akionyesha msisitizo, Lugola alisema amefikia hatua ya kuuweka
rehani ubunge wake baada ya waziri katika hotuba yake kudai serikali ina
mpango wa kutoa ruzuku kwa wavuvi.
“Nimesikia hotuba ya Waziri wa Uvuvi na Mifugo na mpango wake wa
kutaka kutoa ruzuku kwa wavuvi wadogo, nimeangalia vitabu vyote sioni
mahala alipotenga fedha hizo kwenye bajeti yake kwa mwaka huu wa fedha.
“Waziri akinionyesha mahala zilipo fedha hizo alizotenga kwa ruzuku,
naandika barua ya kujiuzulu leo hii jioni na nitaandika hundi ya sh
milioni 50 kumpa waziri,” alisema Lugola.
Mbunge huyo alimlaumu Waziri Kamani na naibu wake kwamba walipokuwa
wabunge walikuwa wakiilaumu sana wizara hiyo, lakini leo baada ya kuwa
mawaziri wamegeuka kuwa wababaishaji.
Alisema wavuvi wadogo hawahitaji ruzuku, bali wanahitaji kuwezeshwa
kwa kuwajengea mazingira mazuri ya uvuvi kwani wana changamoto nyingi
zikiwemo za kuibiwa nyavu na vifaa vyao vya uvuvi.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), alisema tatizo
linaloikabili serikali katika kuendeleza sekta ya uvuvi na mifugo ni
mipango dhaifu.
Alisema Tanzania ina kila kitu kuendeleza sekta ya mifugo na uvuvi,
lakini haina mipango ya kuzifanya sekta hizo zikue na kuleta tija katika
kukuza uchumi wa taifa.
“Hebu tujiulize, tusingekuwa na ng’ombe, kuku, mbuzi, tungetumia
kiasi gani kuagiza nyama kutoka nje?” alihoji Serukamba na kuongeza kuwa
viongozi wasipobadili fikra, Watanzania wataendelea kulalamikiana.
Akitolea mfano wa nchi ya Ethiopia, Serukamba alisema wamefanikiwa
sana katika sekta ya mifugo ambayo inaingiza pato kubwa la uchumi wa
taifa hilo na kutaka Watanzania wajiulize Ethiopia wamewezaje.
No comments:
Post a Comment