WANAFUNZI
wa Chuo Kikuu cha Stella Maris (STEMUCO) mkoani Mtwara, wameandamana
juzi wakidai kutolipwa posho za malazi na chakula na Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu kwa miezi mitatu mfululizo.
Maandamano hayo yalianzia chuoni hapo saa 9 alasiri na kuelekea kwa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, lakini
walipofika maeneo ya Bima yalizuiliwa na polisi na kutakiwa kueleza
kilio chao.
Akizungumza kwa jazba, mmoja wa wanafunzi hao, alisema kwa miezi
mitatu hawajalipwa fedha ya kujikimu, na hakuna tamko lolote ambalo
wameambiwa wakati wana haki kama vyuo vingine.
“Hatujalipwa fedha za malazi na chakula kwa miezi mitatu sasa, ndiyo
maana tumechukua hatua hii ya kuandamana, tunakwenda kwa Mkuu wa Mkoa
tumuelezee matatizo yetu, kwani yeye ndio rais wa mkoa huu.
“Hakuna mwenye silaha wala hakuna anayetaka kuhatarisha amani hapa,
tunaomba msaada wenu polisi, ili tumuone Mkuu wa Mkoa,” alisema
mwanafunzi huyo.
Mwanafunzi mwingine alisema mbaya zaidi uongozi wa chuo umekaa kimya,
hali inayochangia baadhi ya wanafunzi kujiuza ili waweze kujikimu.
“Uongozi wa chuo umekaa kimya hadi leo na hawajaongea chochote, na
inafikia kipindi hadi watoto wa kike wanajiuza na kama unabisha fanya
uchunguzi, pita jioni maeneo ya baa utakuta watoto wa kike wako wengi
hadi mahudhurio ya darasani yanakuwa si mazuri,” alisema.
Akizungumza na wanafunzi hao, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara,
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Ralph Meela, alisema amezungumza na mkuu
wa chuo na kuwashauri kukutana na uongozi huo kukutana na viongozi wa
wanafunzi hao na kuongozana nao katika ofisi wanayotaka kwenda.
Baada ya kukubaliana na wanafunzi hao, aliongozana nao na baada ya
kuwapeleka katika ofisi ya mkuu wa mkoa walipelekwa kwa Kamanda wa
Polisi Mkoa.
No comments:
Post a Comment