Sunday 18 May 2014

Bajeti ya wizara ya nishati na madini yaingia Mdudu

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono wameingia katika mvutano baada ya ujumbe wa maandishi wa kutaka kukwamisha bajeti ya wizara hiyo kusambazwa kwa wabunge.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilieleza kuwa kiini cha mgogoro huo ni ujumbe mfupi (SMS) ambao unamtuhumu Mkono kula njama za kutaka kukwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Gazeti hili limedokezwa kuwa, SMS hiyo inadaiwa kutumwa na Waziri Muhongo kwenda kwa baadhi ya wabunge akimtuhumu Mkono kuwahonga baadhi ya wabunge Sh3 milioni kila mmoja ili kukwamisha bajeti hiyo.
Ujumbe huo unasomeka ”Mhe Spika wa Bunge la Jamhuri, Sisi wabunge waadilifu tunakiri kwamba Mhe Mkono ametufuata na kutupatia fedha kila mmoja milioni 3 ili tukwamishe bajeti ya Nishati na Madini.
Ujumbe huo umeanza pia kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo Jamii Forums .
Mkono
Mkono ambaye pia ni Mwanasheria mashuhuri nchini, alipoulizwa jana kama ni kweli amelalamika kwa Spika juu ya jambo hilo, alikiri na kusema alichofanya ni kulalamika kwa Spika na amemwachia alishughulikie.
“Ni kweli nimelalamika kwa Spika. Unajua taratibu za Bunge ni kuna any complaint (lalamiko) unaliwasilisha officially (rasmi) kwa Spika… hilo jambo lipo nimelifikisha kwa Spika wao ndiyo watafuatilia kwa taratibu zao,”alisema.
Profesa Muhongo
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili alitolee ufafanuzi suala hilo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alituma ujumbe kwa simu ukisema:
“Tutavuka tukiwa na ushindi wa maskini na wanyonge wa nchini mwetu. Tutaendelea kujenga uchumi imara utakaotoa ajira mpya na matumaini mapya kwa vijana, maskini na wanyonge wa nchini mwetu. Watanzania wamechoshwa na wizi, udalali, ubabaishaji na rushwa.”
Mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel alipotafutwa jana alisema yeye hana taarifa juu ya jambo hilo akisema kama lipo, basi huenda likawa mikononi mwa Spika mwenyewe.

Mvutano huo unakuja siku chache baada ya Sakata la IPTL lililoibuliwa Bungeni Ijumaa iliyopita na mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye alisema kuna ufisadi wa zaidi ya Sh200 bilioni katika akaunti ya Escrow iliyopo chini ya Benki kuu ya Tanzania (BoT).
Akaunti hiyo ilikuwa ni ya pamoja kati ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhifadhi malipo ya kila mwezi kwa IPTL katika kipindi chote cha mgogoro kati IPTL na Tanesco ambao uliishia mahakamani.
Tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza sakata hilo.
Alhamisi wiki hii, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliliambia Bunge kuwa wapo watu wanaonunua mashahidi kuhusiana na sakata hilo ingawa hata hivyo hakuwataja kwa majina.
Serikali yahaha kutafuta fedha
Wakati mvutano huo ukiendelea, Serikali inahaha kutafuta fedha ili kuinusuru bajeti ya Serikali na sasa kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake, Andrew Chenge imekuwa ikikutana na Hazina karibu kila siku.
Habari zilizopatikana jana, zilidokeza kuwa bajeti inayoiumiza kichwa zaidi ni ile ya Wizara ya Maji ambayo baadhi ya Wabunge wameapa kuikwamisha endapo Serikali haitakuja na majibu ya kuridhisha.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Wabunge wamepania kukwamisha bajeti hiyo baada ya kugundulika kuwa wizara hiyo ilipatiwa asilimia 30 tu ya bajeti yote ya maji iliyopitishwa na Bunge mwaka jana.
Bajeti za wizara nyingine zinazoiumiza kichwa Serikali ni Wizara ya Ujenzi ambayo inasemekana inadaiwa mabilioni na makandarasi na pia baadhi ya miradi hasa ya barabara haijakamilika.
Habari zinasema Serikali inaumiza kichwa kuongeza fedha za kutoka katika Wizara hiyo ili imalize kutekeleza miradi ya barabara ikiwamo barabara zilizoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni 2010.
“Unajua uchaguzi mkuu ni mwakani… Serikali ina kibarua kigumu cha kutekeleza miradi ya barabara na inahofu CCM itakuwa na wakati mgumu endapo kama ahadi za Rais hazitatimia,”alidokeza mbunge mmoja.
“Kwa hiyo wabunge wengi tunachachamaa kwa sababu tusipopata majibu katika Bajeti hii tumeliwa takuwa na wakati mgumu majimboni na hili hatutalikubali kabisa,”alisisitiza mbunge mmoja kutoka kanda ya Ziwa.
Kuhusu Wizara ya Maji, wabunge wanadai pamoja na kupitisha bajeti ya ya ziada ya Sh184 bilioni mwaka jana, lakini bajeti iliyokwenda kutekeleza miradi ni kati ya asilimia 30 na 40 tu.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika aliituhumu Serikali kuwa ililidanganya Bunge kwa kushindwa kuongeza Sh184 bilioni zilizotakiwa kuongezwa katika bajeti yake ya mwaka 2013/14.
Mnyika aliongeza kusema “Kati ya Sh184 bilioni, Serikali imeongeza Sh86 bilioni tu…Maana yake ni kwamba Sh98 bilioni hazijatoka mpaka sasa kwenda kwenye miradi ya jamii”.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Serikali za Mitaa (Laac), Rajabu Mmbaruk, jana aliliambia gazeti hili kuwa kwa jinsi bajeti za wizara zinavyopigwa panga, ni dhahiri Serikali inapitia wakati mgumu.
Hata hivyo, mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, alisema inavyoonekana Serikali imekuja na mapinduzi makubwa ya bajeti kiasi kwamba haitaki tena kuwasilisha bajeti zisizotekelezeka.
“Wewe unakumbuka mwaka jana bajeti ya maji ilikwama hadi Serikali ikaongeza fedha, lakini hizo fedha zilienda zote? Na hili ndilo linaloleta shida hata kwenye bajeti ya mwaka huu,”alisema Mwijage.
Mwijage aliongeza kusema” huko nyuma Serikali ilikuwa inapitisha bajeti kuwafurahisha wabunge ili wapitishe bajeti, lakini kwa kweli nyingine hazitekelezeki na hilo limeleta mgogoro mkubwa kwa bajeti ya Maji”.
Kutokana na upepo huo mbaya, Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliandika barua kwa Spika akiomba bajeti ya wizara hiyo isogezwe mbele.
Katika barua hiyo ambayo Lukuvi alilithibitishia gazeti hili kuiandika, alipendekeza bajeti ya Wizara ya Maji na ile ya Nishati na Madini, zote zisogezwe mbele hadi mwezi Juni badala ya kusoma mwezi huu.
“Kwa kuwa Wizara hizi bado zipo katika mazungumzo na Wizara ya Fedha kuhusu bajeti zao, ninaomba ukubali wizara hizi kubadilishiwa tarehe za kuwasilisha ili ziwasilishe mwezi Juni,”inasema barua hiyo.
Barua hiyo ya Lukuvi ya Mei 10,2014 yenye kumbukumbu 1/CEB.274/420/02 iliyotumwa kwa Spika, Anne Makinda, ilitumwa pia kwa Waziri mkuu, Waziri wa Maji na Waziri wa Nishati na Madini.
Hata hivyo, taarifa iliyopatikana jana, zinasema katika kujaribu kukokoa jahazi, kamati ya bajeti, juzi ilikutana na walipa kodi wakubwa nchini ikiwamo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kubadilishana mawazo.
 Taarifa zisizo rasimi zinasema Serikali inakabiliwa na ukata mkubwa wa fedha na hiyo inasababishwa na bajeti nyingi za wizara kupunguzwa, mfano ukiwa wizara ya Mambo ya Ndani iliyopunguzwa kwa Sh500 bilioni.

No comments: