Thursday, 22 May 2014

UKAWA wakutana na Mama Maria Nyerere

Dk.Slaa aongoza msafara wa UKAWA nyumbani kwa Nyerere
Dr Slaa na Mama Maria Nyerere
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amewaongoza viongozi wenzake wa vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi) kuitembelea familia ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kijijini Butiama na kuiachia ujumbe mzito.
Viongozi hao kupitia Umoja wao wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wako kwenye ziara mikoani kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuwa na Katiba mpya bora, inayotokana na maoni yao waliyoyatoa kwenye Tume ya Mbadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Wakiwa nyumbani kwa mwalimu Nyerere juzi, Dk. Slaa kwa niaba ya wenzake aliwataka Watanzania kuwa makini na watu wanaofanya unafiki wa kumuenzi muasisi huyo kwa maneno ya jukwaani, huku wakimnanga kwa kufanya vitendo vya kifisadi na ubadhirifu aliyoyakemea.
Alisema kuwa wakati huu ambapo taifa linapitia kwenye changanmoto za kuandika Katiba mpya, wananchi wanatakiwa kumuenzi mwalimu kwa vitendo, wakipigania katiba inayozingatia maoni yao kwa ajili ya maisha yao na hatma ya taifa.
Dk. Slaa aliongozana na Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Mustapha Wandwi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa ya NCCR-Mageuzi, Hemed Msabaha pamoja na kiongozi wa Shura ya Maimamu, Suweid Sadiq.
Katika mazungumzo na familia ya Nyerere, Dk. Slaa aliwaonya viongozi walioko madarakani kuacha tabia ya kujitapa kumuenzi mwalimu majukwaani wakati wanafanya vitendo vinavyoliangamiza taifa kutokana na kukosa uadilifu na uwajibikaji.
“Ni kejeli kubwa kusema unamuenzi mwalimu Nyerere wakati unakataa rasimu ya Katiba mpya ambayo inapendekeza kuwepo kwa uwazi, audlifu na uwajibikaji, tena wananchi wametaka mambo hayo yawe ni tunu za taifa.
“Ni vyema viongozi wetu kama wanataka kweli kumuenzi Baba wa Taifa, tunawataka wafanye hivyo kwa vitendo na sio maneno kama wanavyofanya hawa wa serikali sasa na CCM,”alionya.
Dk. Slaa alitolea mfano akisema, mwalimu Nyerere alianzisha Azimio la Arusha ambalo liliweka misingi bora ya utaifa, kusimamia uadilifu, uwazi na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi wao na serikali kwa watu wake, lakini lilivunjwa na viongozi waliopo madarakani kwa kuweka mbele ulafi, ubinafsi na maslahi yao.
“Ni upuuzi mkubwa na unafiki kusema unamuenzi mwalimu Nyerere wakati hata Azimio la Arusha alilolianzisha kwa ajili ya kusimamia misingi ya uongozi bora mumelivunja. Wakati wa mwalimu tulikuwa tunaitana ndugu, leo wanaitana waheshimiwa, hali ambayo tayari inaweka matabaka.
“Sisi UKAWA tutamuenzi mwalimu kwa vitendo…kwa kupiga vita ufisadi, ubadhirifu…tutamuenzi kwa kupigania uwepo wa Katiba mpya na bora inayotokana na maoni ya wananchi ambao wamependekeza uadilifu, uwazi na uwajibikaji kuwa ni tunu za Taifa hili,”alisisitiza.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Katiba mpya lazima itokane na maoni ya wananchi ambao wataamua namna gani waongozwe na wajitawale. Pia akiwataka watawala wasikilize simulizi za mwalimu Nyerere kwa makini ambazo amekuwa akisisitiza umuhimu wa maslahi na matakwa ya watu kuwekwa mbele na viongozi.
Wengine waliofuatana na viongozi hao ni pamoja na Diwani wa Kata ya Kitaji, Haile Tarai (CHADEMA), Kamishna wa NCCR Mageuzi mkoa wa Mara, Stephen Sebeki.
Mtoto wa tatu wa Nyerere, Madaraka Nyerere ndiye aliwapokea viongozi hao na kuwatembeza katika kaburi la hayati muasisi huyo, ambapo walipata fursa ya kuweka mashada ya maua.
Akiwakaribisha viongozi hao, Madaraka alisema kuwa pamoja na kwamba Nyerere alikuwa mwana-CCM, lakini familia hiyo inatunza hadhi yake kwa kuwakaribisha watu mbalimbali kutembelea kaburi lake bila kujali itikadi za vyama.

No comments: