.
Wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili na wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja sasa wanatumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi aina ya Truvada kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo badala ya kutumia mipira ya kondomu.
Mwananchi lilizungumza na baadhi ya
wafanyabiashara ya ngono jijini katika maeneo ya Mwananyamala Hospitali,
Komakoma na Vingunguti ambao walisema kuwa wanatumia dawa hizo kwa
ajili ya kuzuia maambukizi ya VVU ili kuwaridhisha wateja wasiopendelea
mipira hiyo.
Baadhi ya wafanyabiashara hao walidai kuwa
wanatumia Truvada kuzuia maambukizi pindi wanapokutana na wanaume
wakware ambao huwabaka au kuwalazimisha kufanya mapenzi bila kinga.
“Hizi dawa tunazipata katika hospitali na wakati
mwingine katika maduka makubwa ya dawa. Kwa sababu zinazuia maambukizi
ya Ukimwi na sisi ni watu ambao tunafanya kazi katika mazingira
hatarishi,” anasema Leyla Musa, mmoja wa wanawake hao.
Si hivyo tu, kwa kuwa hii ni biashara baadhi yao
hukubali kufanya mapenzi bila mipira ili kupata fedha nyingi kutoka kwa
wanaume.
Wengine hukimbilia huduma ya PEP
Baadhi ya wanawake hao wanasema kuwa baada ya
kufanya mapenzi na wanaume kadhaa asubuhi huenda katika kliniki
zinazotoa huduma za ARV na kudanganya kuwa wamebakwa na kisha hupewa
huduma za dharura za ARV zinazoitwa kwa kitaalamu Post-exposure
prophylaxis.
Kwa kawaida mtu aliyebakwa au kujikata hupewa dawa aina ya Lamivudine, Zerophidine au Truvada kulingana na uzito wa tatizo.
“Tunatumia hizi dawa mara kwa mara lakini
tunafanya hivyo katika kliniki tofauti ili tusigundulike,” alisema mmoja
wao, mkazi wa Mwananyamala, Mariam Leshaniki.
Kwa maelezo ya Dk Rachel Baggaley, mtaalamu wa
masuala ya Ukimwi wa Shirika la Afya Duniani anasema dawa za PEP zipo
maeneo mengi duniani kwa sasa na zinafanya kazi kwa ufanisi pia hazina
madhara kwa mwanamke.
“Dawa hizi siyo sumu mwilini, zinaingia kwenye
mfumo wako wa damu kabla virusi havijajizatiti na inavizuia ili mradi
uzitumie ndani ya saa 72,” anasema Dk Baggaley.
Dawa ya Truvada, ambayo ina mchanganyiko wa dawa
aina ya Tenovofir na Emtricitabine, imethibitishwa kuwa salama kwa
kupunguza makali ya VVU pia kuzuia maambukizi mapya. Dawa hizi
zinazotengenezwa nchini India, zimekuwa msaada mkubwa wa tiba kwenye
nchi zinazoendelea.
Mkurugenzi wa Sera, Mpango na Utafiti wa Tume ya Taifa ya
Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk Raphael Kalinga alisema Tume hiyo
inakemea kwa nguvu zote tabia inayofanywa na watu hao, kwani hakuna
tofauti na kuvaa chuma kisha kujitumbukiza kwenye moto uwakao.
“Wanachofanya siyo sahihi. Ina maana kama una
kinga ya malaria basi unatakiwa ukae karibu na mbu wakuume. Si
unawakimbia… huo siyo uamuzi sahihi kabisa na ninawataka waondokane na
tabia hiyo,” alisema.
Hata hivyo, Dk Kalinga alikiri kuwa ni kweli dawa
hizo zinazuia maambukizi, lakini bado inategemea wingi wa virusi
alivyonavyo mgonjwa pia mtu anaweza kuambukizwa magonjwa mengine ya
zinaa kama kisonono, kaswende na pangusa.
“Kwa kweli tunakemea kwa nguvu zote na
tunawashauri kwa usalama wao waondokane na mawazo hayo na wala
wasijaribu hata mara moja kuacha kutumia kondom kuzuia maambukizi,”
alisema.
Kama njia hii ya kuzuia maambukizi ya VVU
itaendelea kufuatwa basi itabadilisha mfumo mzima wa kupambana na virusi
hivyo ambao unahimiza matumizi ya kondomu kama kinga. Tangu mwaka 2010,
tafiti tatu tofauti kuhusu dawa ya Truvada zimefanyika na kuonyesha
uwezo mkubwa wa kuzuia maambukizi ya VVU iwapo zitanywewa kila siku.
Wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsi moja waliotumia dawa hizo kila siku,
walipopimwa damu walionekana kuwa salama kwa asilimia 99.
Wakati Dk Kalinga akipinga matumizi ya Truvada
kama kinga ya VVU, Daktari wa magonjwa ya kuambukiza wa New York,
Anthony Fauci, alisema ni vyema dunia nzima ikakubaliana na mpango wa
kuanza kutumia dawa hizo ili kuokoa mamia ya watu walio katika hatari ya
maambukizi.
“Kaswende, kisonono kinaweza kutibiwa na dawa za
viua sumu (antibiotics), lakini Ukimwi ukiupata ni wa maisha yote
hauwezi kutibiwa,” alisema Dk Fauci.
Kituo cha Kuzuia Magonjwa cha Marekani, kinaeleza
kuwa hata kama itakubaliwa Truvada zitumike kama kinga, basi zitatolewa
kwa wale ambao bado hawajaambukizwa. Pia, watatakiwa kupimwa kila baada
ya miezi mitatu kuhakikisha kuwa hawajapata maambukizo na kupimwa ili
kujua kama hawapati madhara yoyote yanayosababishwa na dawa hizo pia
kama hawana magonjwa ya zinaa.
Watafiti waliogundua Truvada wanaeleza kuwa dawa
hiyo kwa sehemu kubwa inakinga VVU na upande mwingine inasaidia kuua
virusi vya Ukimwi kwa mtu ambaye tayari ameshaathirika. Hata hivyo, FDA
na watafiti hao hawajaeleza kama Truvada inatibu moja kwa moja,
isipokuwa wanasisitiza: “Inamkinga mtu kupata maambukizi mapya,
inamsaidia mwathirika kwa kuua VVU pamoja na kumkinga dhidi ya magonjwa
nyemelezi.”
Mtafiti wa Masuala ya Ukimwi, Dk Edward Maswanya
anakana kuwa Truvada inazuia maambukizi na kusema siyo sahihi kutumia
dawa hizo kama kinga.
“Kinga inayoaminika na kukubalika kuzuia maambukizi ni kondomu pekee hiyo Truvada haizuii kabisa,” alisema.
Alisema wanaofanya biashara ya ukahaba wanajiweka hatarini kupata maambukizi ya VVU pia wapo hatarini kuambukiza wengine.
Baadhi ya wanawake wanaofanya biashara ya ngono wa eneo la
Temeke, Tandika na Mbagala Zakhem walipohojiwa walidai kuwa mipira ya
kiume imekuwa siyo salama kwao tena, kwani kuna wakati wanaume huitoboa
kwenye chuchu na mara nyingine huzama ukeni kiasi cha kusababisha
wafanyiwe upasuaji.
“Kondomu zinasaidia, lakini kwa wanaume
wastaarabu, lakini ninapomeza hizi dawa hata nikibakwa zinazuia
maambukizi na zinasaidia kama ninao nisiwaambukize,” alisema mmoja wa
wanawake hao.
Mashoga nao
Mwanamume anayeshiriki mapenzi ya jinsi moja, Aly
maarufu kama Aunt Aly, mkazi wa Kinondoni anasema ingawa anaishi na VVU,
lakini yeye huzitumia dawa hizo kuepuka kupata maambukizi mapya na
kuzuia asiwaambukize wengine, kwani hubakwa mara kwa mara na vibaka.
“Mara kwa mara sisi tunaingiliwa kwa nguvu na
wakati mwingine wabakaji hawavai mipira sasa, tunakunywa hizi kama
sehemu ya kinga, ingawa mimi nazinywa kama ARV za kawaida,” alisema.
No comments:
Post a Comment