WAKATI sakata la kuzagaa kwa CD yenye mlengo wa kumpigia kampeni
mgombea urais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, likizidi kushika kasi
jijini Dar es Salaam, baadhi ya wapenzi na wanachama wa klabu hiyo
wamemtaka mwenyekiti anayemaliza muda wake, Ismail Aden Rage, ajibu
tuhuma dhidi yake zilizoelezwa katika CD hiyo.
CD hiyo inamnukuu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria
Hanspope akizungumza na baadhi ya matawi ya Wilaya ya Kinondoni huku
akitoa kauli za kashfa kuwachafua baadhi ya wagombea katika
kinyang’anyiro cha uchaguzi huo utakaofanyika Juni 29.
Kwa mujibu wa CD hiyo, Hanspope anasikika akimnadi Aveva kwa vigezo
mbalimbali ikiwamo kama mmoja wa vigogo wa Kundi la Friends of Simba,
huku akimnanga mmoja wa wagombea urais, Michael Wambura na uongozi
unaomaliza muda wake chini ya Rage ‘Tutu Vengere.’
Hanspope ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba,
aliyechaguliwa na Rage, ananukuliwa akidai kuwa muda wote waliokuwa
madarakani, shughuli zote za usajili alikuwa akiachiwa yeye na kwamba
vikao vyao havikuwa vya kimaendeleo zaidi ya Rage (Mwenyekiti), kuwa
mtu wa ‘kubagain’.
CD hiyo ambayo inamnukuu Hanspope akizungumza na wanachama hao wa
Kinondoni, pia imelalamikiwa na Wambura, akilia dhidi ya kitendo hicho
cha mpinzani wake kuanza kupigiwa kampeni kabla ya wakati.
Mmoja wa wanachama wa Tawi la Simba Mtongani, Juma Zozo, ameonyesha
kusikitishwa na kauli ya Hanspope kupitia CD hiyo, kwani naye ni
miongoni mwa Kamati ya Utendaji inayomaliza muda wake, hivyo alikuwa
wapi kuyasema kabla ya kuanza harakati za uchaguzi.
Aliongeza kuwa hivi sasa kuna baadhi ya wanachama wameweka pingamizi
dhidi ya kamati nzima inayomaliza muda wake kwa kuvunja Katiba ya
Simba, ikiwamo Hanspope kama angekuwa ni mmoja wa wagombea, hivyo
anashangazwa na kauli hiyo inayolenga kuwahadaa Wanasimba, wakati naye
alikuwa kundini.
Yassin Yussuf, amemtaka Rage aeleze ukweli kuhusiana na madai ya Pope
kwamba uongozi wao ulikuwa wa ‘magumashi’ na yeye alikuwa ni mtu wa
‘kubagain’ badala ya kuangalia maendeleo ya klabu.
Alipotafutwa Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini jana, simu ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, Dk. Damas Ndumbaro,
amenukuliwa akimtaka Wambura kama ana ushahidi wa hayo, aufikishe kwa
kamati husika ili hatua ziweze kuchukua mkondo wake.
Kwa upande wa Hanspope, alikiri kuzungumza na matawi hayo na kuongeza
kuw, haoni tatizo kwani yeye si mgombea, bali ni mwanachama na haoni
kama anahusika na kipengele hicho cha kampeni.
Kamati ya Uchaguzi ya Simba, ilionya watu kuanza kampeni kabla ya
muda ambao umewekwa, na kwamba watakaobainika kanuni zitachukua mkondo
wake.
No comments:
Post a Comment