WIMBI
la matumizi mabaya ya fedha za umma limezidi kukiandama Chama Cha
Mapinduzi (CCM), ambapo hivi sasa kinatuhumiwa kutumia fedha za umma
katika ziara na ukaguzi wa miradi.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa kila ziara ya CCM inakofanyika,
mkurugenzi wa halmashauri husika hutoa magari au fedha za kuwakirimu
wahusika.
Imedokezwa kuwa miongoni mwa ziara ambazo zinatumia fedha za
halmashauri ni inayofanywa hivi sasa mikoani na Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana.
Inaelezwa kuwa ziara hizo hazipaswi kugharimiwa na fedha za serikali
kupitia halmashauri mbalimbali kwakuwa zinatokana na wananchi wenye
itikadi tofauti pamoja na wasio na itikadi.
Michango hiyo ndiyo inadaiwa kuwapa nguvu vigogo wa CCM na kuacha
kupitisha bakuli kuomba misaada kwa makada wake kama ilivyozoeleka siku
za nyuma.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa vyama vya upinzani na CCM vimekuwa na
utaratibu wa kuomba misaada kwa makada wao au wahisani, wafadhili wa
ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni utaratibu huo unaonekana
kutumiwa zaidi na wapinzani kutokana na kutokuwa na uwezo wa kuwaamrisha
au kuwashawishi wakurugenzi wa halmashauri kugharimia ziara zao.
Ukombozi iliwasiliana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye, ambaye alisema kuwa taarifa hizo zinalenga kukichafulia jina
chama tawala.
“Madai hayo ni ya kiupuuzi na kwamba misafara yetu inawaumiza
viongozi wa CHADEMA, sisi tunapoamua jambo tunakuwa na mipango sambamba
na kujitosheleza,” alisema.
Hata hivyo, Tanzania Daima limepata taarifa kuwa baadhi ya
halmashauri ambazo Kinana na timu yake wameshapita ziligharamia malazi,
chakula na usafiri wa ndani ikiwemo magari ya serikali kutumika.
Halmashauri ambazo taarifa zake zimekusanywa na gazeti hili ni pamoja
na Nzega, Igunga na Uyui zilizopo mkoani Tabora na Iramba iliyopo
mkoani Singida huku wakurugenzi wake wakikiri kutumia magari ya serikali
na baadhi ya watumishi kuhudhuria katika ziara hiyo.
Katika Wilaya ya Igunga, msafara wa Kinana ulikaa kwa muda wa siku
tatu ambapo halmashauri kupitia viongozi wa CCM wa wilaya hiyo
waligharimia usafiri wa ndani, chakula na malazi pamoja na kukodisha
pikipiki 50.
Pikipiki hizo zilitumika kumpokea Kinana na magari 10 yaliyotumika
kuwabeba wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo waliotakiwa
kuhudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Igunga.
Mbali na gharama hizo, pia ziara hiyo inaelezwa kusimamisha kazi
mbalimbali za kiutendaji katika maeneo wanayopita kutokana na watendaji
wa serikali kutakiwa kuwa sehemu ya ziara hiyo.
Chanzo kutoka ndani ya Halmashauri ya Igunga, kilieleza kuwa mbali na
gharama ya malazi, vyakula, usafiri na malazi, pia hakukuwa na malipo
iliyolipwa na chama hicho kwa kutumia ukumbi wa halmashauri kufanya
mikutano yake ya ndani.
Chanzo hicho kilieleza kuwa msafara wa Kinana ulikuwa na magari zaidi
ya 28 na kila gari likiwekewa lita 80 za mafuta kutembelea maeneo
mbalimbali.
Kigogo mmoja wa CCM, alidokeza kuwa walitakiwa kuandaa chakula cha
watu 200 huku sahani moja ya chakula ikiuzwa kwa shilingi 5,500.
Alisema walikodisha pikipiki 42 kwa sharti la kila mwenye pikipiki
aliyehudhuria mapokezi ya Kinana, atalipwa sh 7,000 na kuwekewa lita
mbili ya mafuta.
Alibainisha pia walitakiwa wahakikishe msafara wa Katibu Mkuu unapatiwa malazi.
“Sisi chama tulibeba jukumu lile kwa kuwa ni ugeni wa chama, lakini
hakuna hata senti moja tuliyotumia kutoka mfuko wa chama zaidi ya fedha
hizo kutoka ndani ya halmashauri yetu,” alieleza mtoa habari wetu kutoka
Igunga.
Katika Wilaya ya Nzega, Uyui na Iramba, msafara wa Kinana ulipatiwa
mafuta ya magari na chakula kwa fedha zilizotoka katika halmashauri na
kukabidhiwa viongozi wa CCM wa wilaya, huku suala la malazi likiachwa
kuwa jukumu la waliokuwa katika msafara.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wakurugenzi wa
wilaya zilizofanyiwa uchunguzi walikanusha kugharamia ziara hizo, lakini
wakikiri kutoa magari yaliyozunguka katika miradi iliyokuwa ikikaguliwa
na Kinana.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Igunga, Rusika Turuka, alipoulizwa juu ya
halmashauri yake kugharamia ziara ya Kinana, alitaka apewe muda kwa
maelezo kuwa yupo katika mkutano na hata alipopigiwa tena simu
hakupokea.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Nzega, Abraham Mndeme, alikiri ofisi yake
kutoa magari yaliyowabeba watumishi wa serikali na madiwani wa CCM
kuongozana na Kinana katika ziara hiyo wilayani mwake.
Mndeme, alisema ugeni uliofika katika wilaya yake ni wa kitaifa, na
kwamba miradi iliyohitaji kukaguliwa ni ile iliyosimamiwa na halmashauri
ya wilaya.
“Walioambatana na msafara wa Kinana ni madiwani na sisi tulitoa
magari ya kuwasafirisha kwenda kwenye miradi na kwa watendaji mimi
nilitumia gari moja na mhandisi wa manispaa,” alisema Mndeme.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Uyui, Hadija Mkauani, alipoulizwa juu ya
kugharamia ziara ya Kinana, alimuomba mwandishi akutane nae ofisini na
alipoambiwa simu inapigwa kutoka Dar es Salaam alikata simu.
“Baba naomba tuonane ofisini tuweze kuongea vizuri hayo mambo au
umtume mwakilishi wako hapa mkoani si mnaye huku, tutaongea vizuri tu,”
alisema Mkauani.
Kaimu Mkurugenzi wa Iramba, Mariam Mpita, alisema gharama za ziara
hiyo zilibebwa na CCM huku yeye, watendaji wa halmashauri hiyo
waliambatana na Kinana kukagua miradi ya maendeleo.
Nape afafanua
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, badala ya kujibu hoja ya ziara zao kutumia fedha za umma aliilaumu CHADEMA.
Alisema ziara zao zinawaumiza CHADEMA waliokuwa wakifanya ziara za
aina hiyo ili kujiimarisha, lakini sasa wanaona zinafanywa na CCM
wanahofia kuanguka mwaka 2015.
“Hata mtoto wa darasa la kwanza akisikia hayo madai atajua ni upuuzi,
lakini ulizeni halmashauri iliyochangia hata shilingi moja. Najua ziara
hizi zinawaumiza sana CHADEMA,” alisema.
Alipoulizwa kama ziara yao ina lengo la kuwaumiza CHADEMA au
kuangalia changamoto zinazowakabili wananchi, na CCM itakavyoishauri
serikali kutatua yatakayobainika, Nape alisema swali aliloulizwa ni
fikra za kijinga za CHADEMA.
Nape alisema CHADEMA hawana ujanja wa kukwepa kifo chao, huku akisema uzushi na uongo hautawasaidia kupona.
Wakati Nape akikana halmashauri hizo kugharamia ziara za chama hicho,
wiki iliyopita katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha,
Mkurugenzi wa jiji hilo, Juma Idd, alikiri kufanya hivyo.
Idd, alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya madiwani wa jiji
hilo waliohoji sababu za ziara za madiwani au viongozi wa CCM kutumia
magari ya halmashauri.
Idd, alisema walitoa magari hayo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya
serikali iliyotaka viongozi wa CCM kupita kukagua utekelezaji wa ilani
yao.
Alisema kuwa jiji walitoa wataalamu na gari kwa ajili ya kwenda kutoa ufafanuzi juu ya miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment