Sunday 25 May 2014

Shiboli niko tayari kucheza timu yoyote

 Ali Ahmed 'Shiboli'
MCHEZAJI mahiri wa soka aliyewahi kung’ara na timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes,’ KMKM na Simba, Ali Ahmed ‘Shiboli’, amesema bado yupo katika kiwango bora cha kucheza Ligi Kuu.
Shiboli aliyetikisa msimu wa 2010/11 baada ya kugombewa na klabu za Simba na Yanga, amesema yu tayari kujiunga na timu ya Ligi Kuu baada ya kupumzika vya kutosha.
Alisema aliamua kupumzika kwa muda baada ya kushindwa kumalizana na KMKM iliyokuwa ikijiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mapema mwaka huu.
Akizungumza kwa simu kutoka jijini Tanga, Shiboli alisema bado ana uwezo wa kucheza Ligi Kuu Bara na kwamba anaaamini atapata timu ya kuicheza msimu ujao.
“Muda mrefu nilikuwa najifua pale Vingunguti, niliamua hivyo kutokana na kuwa na matatizo na viongozi wangu wa KMKM. Sitaki kuzungumzia hilo kwa sasa, naangalia maisha yangu ya baadaye,” alisema Shiboli.
Alisema kwa umri wake na mazoezi anayoyafanya, vinamruhusu kucheza ligi ya ushindani kama ilivyo ya Bara, hivyo yu tayari kusajili klabu yoyote kama watafikia muafaka kwa maana ya maslahi.
Jina la Shiboli lilivuma zaidi katika michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 2010, baada ya kuwindwa vikali na timu kubwa za Simba na Yanga, wakati huo akichezea Zanzibar Heroes.
Wakati nyota huyo akiwaniwa na Yanga, Simba walimkatia denge na kufanikiwa kupata saini yake, jambo ambalo lilikuwa gumzo kubwa kwa wapenzi na mashabiki wa klabu hizo mbili.

No comments: