Monday 26 May 2014

Lisu aanika wabunge walioomba Rushwa

 Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu



Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amewataja kwa majina mawaziri na wabunge aliosema bungeni kuwa wamekuwa ombaomba katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Baadhi ya waliotajwa ni pamoja na Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni Naibu Spika, Job Ndugai; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi; Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana na wabunge Betty Machangu (Viti Maalumu), Livingstone Lusinde (Mtera), John Komba (Mbinga Magharibi), Eugen Mwaiposa (Ukonga) na Gudluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi).
Hata hivyo, gazeti hili halijawataja majina mawaziri na wabunge wengine waliomo kwenye orodha hiyo ya Lissu kwa kuwa hawakupatikana jana kujibu tuhuma hizo.
Mbali na kuwataja kwa majina, Lissu pia ametoa vielelezo vinavyoonyesha jinsi walivyokuwa wakiidhinishiwa malipo kwa nyakati tofauti na Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF), kwa sababu mbalimbali.
Lissu alimwambia mwandishi wetu jana kuwa licha ya kiwango cha fedha kutokuwa kikubwa, lakini kinaweza kusababisha mgongano wa kimasilahi kati ya wajibu wa wabunge kwa umma na masilahi yao binafsi.
“Hali hii inaweza kusababisha Bunge likashindwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia Serikali na taasisi zake,” alisema Lissu huku akisisitiza azimio lake la kuwasilisha hoja binafsi kwa Spika wa Bunge ili iundwe tume kuchunguza suala hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Eliud Sanga jana alikiri kuwa shirika hilo liliidhinisha malipo kwa mawaziri na wabunge hao kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hata hivyo, alisema shirika hilo halitoi fedha taslimu, bali hununua vitu ambavyo viliombwa na viongozi hao kwa ajili ya kusaidia wananchi na si kufanya biashara.
Sakata lenyewe
Akizungumzia jinsi mawaziri na wabunge hao walivyosaidiwa, Lissu alisema LAPF ilitoa Sh2.5 milioni kwa ajili ya mradi wa madarasa Jimbo la Kongwa linaloongozwa na Ndugai.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Ndugai alisema hakuna tatizo lolote kwa mbunge kupewa msaada na mfuko wa kijamii.
“Huyo Lissu ana upungufu mkubwa. Hivi LAPF ikisaidia Sh2 milioni kwa ujenzi wa darasa unaogharimu Sh10 milioni ni tatizo hilo? Nchi hii inakwenda wapi jamani, siyo kila kitu wanachozungumza wapinzani ni hoja, kama LAPF wangekuwa wanatoa fedha lingekuwa tatizo lakini wanasaidia vifaa tu.”

Ndugai alisema hiyo ni mara ya kwanza Jimbo la Kongwa kupatiwa msaada na shirika hilo huku akihoji juu ya Lissu katika jambo hilo ambalo alisema ni la kawaida mno.
Pia Lissu alisema LAPF ilitoa Sh1.6 milioni kwa ajili ya kuisaidia Shule ya Isimani iliyopo katika jimbo la Waziri Lukuvi.
Alipoulizwa jana kuhusu madai hayo, Waziri Lukuvi alisema asingeweza kuzungumza lolote kwa sababu alikuwa akiuguza huko Iringa. Shirika hilo liliidhinisha Sh1.5milioni kwa ajili ya mradi wa maabara wa Jimbo la Arumeru Mashariki.
Lissu alisema Waziri Kairuki aliidhinishiwa fedha kwa ajili ya ununuzi wa kompyuta mpakato (Laptop) mbili kwa ajili ya vyama vya wafanyakazi. Akizungumzia tuhuma hizo Kairuki alisema: “Sina la kusema katika hilo pengine ungewauliza LAPF watakuwa na ufafanuzi zaidi kuhusu fedha wanazozitoa kwa ajili ya kusaidia masuala mbalimbali.”
Lissu pia alisema LAPF iliidhinisha Sh2.5milioni kwa Waziri Chana ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu kwa ajili ya taasisi ya Iringa Constituency Development Account.
Kuhusu madai hayo Chana alisema: “Mifuko ya kijamii ina idara za kusaidia jamii. Mtu yeyote anaweza kuomba msaada katika mifuko hii na akasaidiwa.”
Alisema hakuna sheria zinazombana mbunge kuomba msaada kwa ajili ya kusaidia wananchi wa jimbo lake na kusisitiza kuwa hata Rais huwa anaomba msaada.
“Sijui huyo Lissu anasaidiaje wananchi wake jimboni. Kuna mifuko ya kusaidia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi. Sijaelewa dhambi iko wapi katika hili. Benki ya NMB hivi karibuni ilitoa msaada wa mashuka Wilaya ya Ludewa, sioni tatizo,” alisema.
Kuhusu Mbunge wa Ukonga, Lissu alisema Aprili 5 mwaka jana, LAPF iliidhinisha malipo ya Sh500,000 kwa ajili ya taasisi ya Ukonga Constituency Development Trust Fund inayoongozwa na Mwaiposa.
“Hiyo Saccos ipo mpaka leo na kuomba siyo kosa. Sisi kama wabunge tuna dhamana ya kushirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo. Si dhambi kuomba fedha za ujenzi wa madarasa,” alisema Mwaiposa.
Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema alisema Februari 2013, uongozi wa LAPF uliidhinisha Sh2.8 milioni kwa Machangu kwa ajili ya taasisi inayoitwa Iyana Education Trust.
Hata hivyo, Machangu alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Ni muongo kabisa (Lissu) yeye inamhusu nini hiyo?”

Lissu alisema nyaraka alizonazo zinaonyesha kuwa Agosti, 2013 LAPF iliidhinisha fedha za kununulia pikipiki mbili kwa ajili ya vituo vya afya vya Jimbo la Mtera linaloongozwa na Lusinde.
Kama ilivyokuwa kwa Mwaiposa, Lusinde naye alisema kuomba si kosa na kwamba amekuwa akiomba misaada sehemu mbalimbali kwa ajili ya kulisaidia jimbo lake.
“Fedha hizo tumeshapata na pia tuliomba nyingine katika Kiwanda cha Saruji cha Wazo bado hatujapata,” alisema Lusinde na kusisitiza kuwa mbunge hawezi kuona mambo hayaendi katika jimbo lake kisha akakaa kimya.
Lissu pia alisema LAPF ililipa Sh1.5 milioni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa ajili ya Mfuko wa Nyasa Foundation uliopo katika eneo la jimbo linaloongozwa na Komba ambaye pia ni mlezi wa mfuko huo.
Komba alifafanua kuhusu fedha hizo na kusema: “Zilikuwa za Harambee na tuliomba sehemu nyingi lakini mimi siyo niliyeomba. Wao ndiyo waliomba na hata hundi walichukua wao.”
Lissu pia alisema LAPF iliidhinisha Sh1.5 milioni kwa ajili ya mradi wa maabara wa Jimbo la Arumeru Magharibi la Medeye madai ambayo mbunge huyo aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema ili ayajibu anataka mwandishi awe pamoja na Lissu na wakae wote watatu kwa pamoja.

No comments: