Wachezaji wa Azam FC wakipongezana baada ya Kipre Tchetche kuipatia timu yao bao la pili |
Timu ya Azam FC ‘wanalambalamba’
leo wametoa dozi ya magoli 5-0 kwa Adama City FC ya Ethiopia kwenye
mashindano ya Kagame Cup ambayo yanazidi kuchanja mbuga jijini Dar es
Samaa mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa.
Kipre Tchethe amefunga magoli
mawili kwenye mchezo wa leo, Kipre alianza kufunga goli la kwanza dakika
ya nane kipindi cha kwanza, Tchetche tena akarudi kambani kufunga goli
la pili kwa upande wa Azam dakika ya 19 ya mchezo.
Mlinzi wa Adama City (kushoto) akijaribu kumzuia mshambuliaji wa Azam FC Ame Ally ‘Zungu’ |
Shah Farid Mussa akaiandikia Azam
goli la tatu dakika ya 35 kipindi cha kwanza akiunganisha pasi safi
kutoka kwa Erasto Nyoni. Kipindi cha kwanza kilimalizika Azam wakiwa
mbele kwa magoli 3-0.
Kipindi cha pili Azam walirejea
uwanjani wakiwa bado wana njaa ya magoli kwani dakika nne baada ya
kipindi cha pili kuanza, Mudathir Yahya aliifungia Azam goli la nne.
Dakika ya 79 Agrey Morris
alifunga goli la tano kwa mkwaju wa penati baada ya mlinzi wa Adama City
Moges Tadese kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Kiungo wa Azam FC Himid Mao (kushoto) akiwa kwenye harakati za kumtoka mchezaji wa Adama City |
Wachezaji wa Adama City
walijikuta wakimaliza mpira wakiwa tisa kufutia wachezaji wao wawili
kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Wachezaji waliotolewa kwa kadi nyekundu
kwa upande wa Adama City ni Eshetu Menna na Moges Tedese.
Azam walifanya mabadiliko kipindi
cha pili kwa kuwatoa Kipre Tchetche na nafasi yake ikachukuliwa na
Didier Kavumbagu wakati Said Morad aliingia kuchukua nafasi ya Pascal
Wawa na Agrey Morris akapumzishwa kumpisha Kamagi Gadiel Michael.
Erasto Nyoni akiwa mwenye furaha baada ya kupiga krosi iliyozaa goli mfungaji akiwa ni Shah Farid Mussa |
Kesho michuano hiyo itaendelea
tena kwenye uwanja wa Taifa ambapo timu za kutoka Kundi A zitakuwa
vitani, mchezo utakaoanza saa 8:00 mchana utakuwa ni kati ya Gor Mahia
ya Kenya dhidi ya Telecom ya Djibouti wakati mchezo wa saa 10:00 jioni
utakuwa ni kati ya Yanga dhidi ya Khartoum National Club ya Sudan.
No comments:
Post a Comment