Wednesday, 15 July 2015

Aliyekamatwa na milion 700 Dodoma arudishiwa pesa zake, polisi wasema alikwenda Dodoma kununua nafaka

Aliyekamatwa na milion 700 Dodoma arudishiwa pesa zake, polisi yasema alikwenda Dodoma kununua nafaka
Jeshi la polisi mkoani Dodoma limekanusha taarifa zilizozagaa kuhusiana na Raia wa Asia kukamtwa na fedha zaidi ya sh. m.700 kwa madai ya kuwahonga wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM ili wamchague mmoja kati ya waliokuwa wanawania nafasi ya Urais
Polisi imesema kuwa uchunguzi uliofanywa na jeshi la polisi umebaini kuwa hakuna kosa la jinai lililothibitika licha ya kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma za rushwa ambazo ndiyo zilikuwa msingi wa ukamataji wa mtu huyo hazikuthibitika, kwa kuwa hakuna aliyeona akizigawa fedha hizo wala hakuna aliyedai kushawishiwa au kugawiwa fedha hizo.

Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, David Misime.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari na kamanda wa polisi mkoani hapa, David Misime mtu huyo aliyejulikana kwa jina la Amit Kevalramani aliyekamatwa juma lililopita kwenye hoteli ya St Gaspar mjini hapa ni mganyabiashara wa mazao ya nafaka ni siyo mpambe wa wanachama wa CCM waliokuwa wanawania Urais.
Misime amesema mnamo siku ya Julai 11 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi kuna baadhi ya wananchi walitoa taarifa kwa jeshi la polisi kwamba kuna mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia amekamatwa na wananchi akiwa na fedha nyingi na kuna vurugu kubwa katika hotel ya St Gaspar.
“Baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi mkoani hapa lilifika eneo la tukio ili kuona kama taarifa hizo ni za kweli, askari walithibitisha kuwa ni kweli, walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia ambaye alijulikana kwa jina la Amit Kevalramani (31), Mhindi, Mfanyabiashara, Mkazi wa Dar es Salaam akiwa na fedha kiasi cha sh. 722 milion ambacho alipohojiwa alisema kuwa Julai 10 mwaka huu alifika Dodoma kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka” amesema Misime na kuongeza kuwa,“Alipofika Dodoma hiyo siku majira ya asubuhi alifikia katika Hoteli ya St. Gasper na kesho yake Julai 12 aliamua kurudisha fedha benki kutokana na kuona mkusanyiko wa watu wengi wasioeleweka na wenye viashiria vya vurugu.”
Misime alisema kuwa akiwa katika harakati ya kurejesha fedha hizo benki, ndipo kundi la watu waliokuwa katika eneo la Hoteli hiyo ya St. Gaspar walimtilia mashaka na kumzuia asiondoke na ndipo taarifa zilitolewa polisi.
Alisema mashaka ya watu hao yalitokana na vuguvugu za kisiasa na mchakato wa uchaguzi kati ya makundi mbalimbali kuwa kuna watu wanahonga wajumbe. Taarifa za aina hiyo ambazo hata Jeshi la Polisi lilikuwa limepokea bila uthibitisho.
Alibainisha kuwa uchunguzi uliofanywa na jeshi la polisi umebaini kuwa hakuna kosa la jinai lililothibitika licha ya kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma za rushwa ambazo ndiyo zilikuwa msingi wa ukamataji wa mtu huyo hazikuthibitika, kwa kuwa hakuna aliyeona akizigawa fedha hizo wala hakuna aliyedai kushawishiwa au kugawiwa fedha hizo.
Aidha imethibitika fedha hizo ni mali yake halali na kwa kuwa hakuna ushahidi mwingine uliyo thibitisha vinginevyo amerejeshewa fedha zake.

No comments: