Wanafunzi 18,751 waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka
2014, wamekosa nafasi ya kujiunga na shule za kidato cha tano kwa sababu
mbalimbali ikiwamo ufinyu wa nafasi.
Kati ya hao, wanafunzi 479 wamechaguliwa kujiunga
na vyuo vya ufundi huku idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa
kujiunga na vyuo hivyo ikiongezeka kwa asilimia 25 kutoka wanafunzi 117
mwaka 2014 mpaka kufikia wanafunzi 147 mwaka huu.
“Baadhi ya wanafunzi wamekosa nafasi kutokana na
umri mkubwa na baadhi ya watahiniwa wa kujitegemea wanakosa sifa za
kuchaguliwa,” Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi),
Kassim Majaliwa alisema hapa jana alipokuwa akitangaza kuchaguliwa kwa
wanafunzi hao.
Alisema wanafunzi 55,003 sawa na asilimia 74.5 ya
wanafunzi 73,754 waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ndiyo
waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano.
Majaliwa alisema kuna ongezeko la ufaulu la
wanafunzi 918 mwaka huu, ikilinganishwa na wanafunzi 54,085
waliochaguliwa mwaka 2014 kujiunga na kidato cha tano.
Alisema wanafunzi waliokosa nafasi kuingia kidato
cha tano watadahiliwa na Baraza la Taifa la Ufundi (Nacte) kwenye fani
mbalimbali kama vile ualimu, afya, maendeleo ya jamii na kilimo.
Alisema ufaulu wa watahiniwa wa kidato cha nne
mwaka 2014 kuanzia daraja la ‘distinction’ hadi ‘credit’, yaani ufaulu
wa wastani (GPA) wa 5.0 hadi 1.6 ni watahiniwa 73,754 sawa na asilimia
37.4 ya wanafunzi 240,410 waliofanya mtihani huo.
Alisema uchaguzi ulifanyika kwa kufuata machaguo
matano ya tahasusi (combinations) yaliyojazwa na wanafunzi kwenye fomu
ya uchaguzi ‘Selform.’
Alisema mfumo wa kompyuta ulitumika katika
kumpanga mwanafunzi katika uchaguzi wake wa masomo na shule kwa kuanzia
na chaguo la kwanza. “Kama mwanafunzi atakuwa hana sifa katika machaguo
yote aliyoomba, hupangiwa chaguo la somo alilofaulu zaidi na katika
shule iliyopo karibu na wilaya yake ya makazi kulingana na tahasusi na
nafasi zilizopo,” alisema Majaliwa.
Alisema wanafunzi 29,744 watajiunga na masomo ya sayansi na 25,259 watajiunga na masomo ya sanaa na biashara.
Aliwataka wanafunzi waliochaguliwa kuripoti katika
shule walizopangiwa ili kuanza muhula wa kwanza wa masomo unaotarajiwa
kuanza Julai 18.
“Naagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule
walizopangiwa kwa wakati. Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti kwa
zaidi ya wiki mbili kuanzia tarehe ya mwisho ya kuripoti, nafasi yake
itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi,” alisema Majaliwa
ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, Lindi.
Aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri
kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kila tarafa kuwa na shule ya kidato
cha tano inatekelezwa kikamilifu ili kuwezesha wanafunzi wote
wanaofaulu kupata nafasi ya kuendelea na masomo. “Wadau wote wa elimu
pia wahakikishe kuwa shule zote zinazoanzishwa kwa ajili ya kidato cha
tano zinakuwa na mabweni kwa kuwa shule hizi ni za kitaifa na zinapokea
wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini,” alisema.
Kutokana na kuongezeka kwa ufaulu katika masomo ya
sayansi, Majaliwa alihimiza shule za kidato cha tano zinazoanzishwa
kuwa na maabara ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa tahasusi za sayansi
na kukidhi mahitaji ya shule husika.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment