Waamka kula daku wakutana na Nyoka mwenye Hirizi
Inatisha! Ndani ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, familia ya
mwanaume aliyetambuliwa kwa jina la Hamis Juma, imekumbwa na mauzauza
baada ya kuamka ili kula daku na kukutana na nyoka mwenye hirizi
mlangoni.
Tukio hilo lililozua taharuki lilijiri mapema wiki hii kwenye nyumba
ya familia hiyo inayoishi Mtaa wa Mkota Kata ya Kiwanja cha Ndege mjini
hapa.Baada ya kutonywa juu ya tukio hilo, Ijumaa lilifika kwenye familia
hiyo alfajiri na kushuhudia nyoka huyo aliyekuwa na hirizi na kitambaa
cheusi shingoni akiwa mlangoni.
Akisimulia kisa hicho baba wa familia hiyo, Hamis alisema kuwa
waliamka saa 7:00 usiku ili kupata daku kama kawaida kwani walianza
kufanya hivyo tangu walipofunga.“Wakati tukiwa sebuleni tunakula, tulianza kuona damu nzito ikisambaa kutokea mlangoni.
“Ukweli tulishtuka sana. Tulipofungua mlango tulishtuka kuona nyoka
mkubwa mlangoni akiwa na hirizi huku damu zikiendelea kusambaa kutoka
pale alipokuwa yule nyoka.
“Ilibidi tufunge mlango hadi alfajiri tuliamua kuwaita watu waje kushuhudia na kusaidia kumuondoa,” alisema Hamis.
Katika kutafuta msaada wa kumuondoa nyoka huyo na kusafisha damu
zilizozagaa, alitokea mjomba wa familia hiyo ambaye jina halikupatikana
akaanza kumtoa kwa kutumia mti, jambo lililosababisha taharuki kwa watu
waliokuwepo wakaanza kukimbia.
Baada ya kumtoa nyoka huyo, watu walianza kumpiga wakitaka kumchoma
moto lakini alitokea mwanaume asiyefahamika akamkwapua na kuanza
kukimbia naye mitaani.
Wakati akikimbia, kundi la watu lilikuwa likimkimbiza ndipo alimtupa na kutokomea kusikojulika.
Katika hali ya kushtua zaidi, nyoka huyo alibadilika, akawa hana hirizi
huku akionekana ‘kadogo’ jambo lililoibua madai ya ushirikina hivyo
watu wakamuua.
Kwa upande wake mke wa Hamis, Mama Nurdin ambaye ni mjumbe wa mtaa
huo, alishtushwa na tukio hilo na kusema familia yake imekumbwa na hofu
kubwa.
Uongozi wa Kata ya Kiwanja cha Ndege ukiongozwa na Diwani, Mohamed
Matikula na Afisia Mtendaji, Diha Zongo walifika eneo la tukio na
kuwachukua baba na mama wa familia hiyo hadi ofisi ya kata kwa mahojiano
zaidi.
No comments:
Post a Comment