Wednesday, 8 July 2015

Vikao vya CCM vya kumpata mgombea wa nafasi ya urais vimeanza mjini Dodoma.


Vikao vya juu vya chama cha mapinduzi CCM vya kumpata mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao vimeanza mjini Dodoma ambapo sekretarieti ya halmashauri kuu taifa imekutana pamoja na mambo mengine imepitia maandalizi kuelekea mkutano mkuu July 12 ambao ndio utachagua jina la mgombea wa nafasi hiyo.
Akitoa ratiba ya vikao hivyo  huku akitahadharisha kubadilika wakati wowote katibu itikadi na uenezi CCM Nape Nnauye amesema baada ya kufanyika kwa kikao cha sekretariet ya NEC July 7 kitafuatiwa na kikao cha usalama na maadili chini ya mwenyekiti wa chama hicho rais Jakaya Kikwete July 8 na kisha kamati kuu ya halmashauri kuu itakutana  July 9 
 
Vikao hivyo vitaendelea tena July 10 ambapo halmashauri kuu ya taifa itakutana pamoja na mambo mengine itapitia ilani ya uchaguzi CCM na kupokea majina matano kutoka kamati kuu na kuyapigia kura kupata majina matatu ya ambayo yatapelekwa kwenye mkutano mkuu unaotarajiwa kuanza july 11 na kutoa jina la mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
 
Aidha chama hicho kimewataka wagombea ambao majina yao yataondolewa katika kinyang'anyiro hicho wakubaliane na matokeo.
 
Kwa upande wao wakazi wa mkoa wa Dodoma wamezitaka mamlaka husika kuimarisha ulinzi na usalama kutokana na wingi wa wageni wanaokuja katika vikao hiyo lakini pia wakasikitishwa na hali ya mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali ikiwemo vyakula huku wengine wakionekana kuchangamkia fursa za biashara.
 
Wakati hayo yakiendelea mkuu wa mkoa wa Dodoma Luteni Mstaafu Chiku Galawa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama amesema hali ya usalama imeimarishwa maradufu huku baadhi ya makada waliokwishawasili mkoani hapa wakiwataka viongozi wa serikali kutoingilia masuala ya chama kwani ni haki ya kila mwanachama kujua namna mchakato huo unavyokwenda

No comments: