Jiji la Mwanza jana ‘lilisimama’ kwa takriban dakika 10 wakati
risasi na mabomu viliporindima kutokana na mapambano kati ya
wafanyabiashara ndogondogo na polisi katika mitaa ya Lumumba, Rwagasore,
Makoroboi na Barabara ya Nyerere.
Mapambano hayo yalitokea kuanzia saa 5.00 asubuhi
baada ya wafanyabiashara hao, maarufu kwa jina la Wamachinga kuamua
kutunishiana misuli na polisi waliokuwa kwenye operesheni ya kuwaondoa
kwenye mitaa hiyo.
Wamachinga waliokuwa eneo la Hekalu la Wahindi
lililopo Mtaa wa Makoroboi, ambalo limekuwa likitawaliwa na vurugu za
kila mara baina ya pande hizo na eneo la Stendi ya Tanganyika,
waliwatupia mawe polisi waliokuwa kwenye operesheni hiyo na ndipo
walipoamua kupambana nao kwa kutumia risasi za moto na mabomu.
Tukio hilo limetokea zikiwa zimepita siku nne
tangu Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kumsifia Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, Magesa Mulongo kuwa amepunguza vurugu zilizokuwa zinatokea
Mwanza mara kwa mara, akisema siku hizi hawasikii tena purukushani ya
polisi, mgambo na wamachinga.
Mwandishi wa Mwananchi ambaye alikuwa karibu na
eneo la tukio jana, alishuhudia wamachinga wanaofanya biashara zao
wakitoa vitu walivyopanga pembezoni mwa barabara, huku wengine
wakikimbia.
Polisi mmoja alishambuliwa na wamachinga hao kabla ya kuokolewa na wenzake.
Wakati polisi wanapiga risasi za moto hewani,
wamiliki wa maduka waliyafunga haraka huku wapita njia wakijipenyeza
kwenye baadhi ya vichochoro ili kujinusuru.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Charles Mkumbo alisema walikuwa na operesheni ya kawaida ya
kuwaondoa watu wasiofuata utaratibu wa kufanya biashara kwenye maeneo
yasiyotakiwa.
Mkumbo alisema baadhi ya wafanyabiashara hao
walitaka kuwagomea askari waliokuwa kazini na kwamba, polisi
walilazimika kupiga risasi hewani ili kuwatawanya.
“Ni kweli kulikuwa na taharuki, lakini naomba
niseme hakukuwa na madhara yoyote na hali hiyo ilitokea baada ya baadhi
ya vijana kutaka kujaribu kutunishiana misuli na askari,” alisema Mkumbo
na kuongeza:
“Kutokana na vurugu hizo tunawashikilia watu watatu ambao kesho (leo) tutawafikisha mbele ya Mahakama ya Jiji.”
Akihutubia wananchi kwenye viwanja vya Furahisha,
Kinana alimsifu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kuwezesha kurudisha hali ya
utulivu jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment