Thursday, 23 July 2015

Yanga yaona mwanga Katika Michuano ya Kagame

MABINGWA wa Tanzania Bara Yanga, jana walizinduka katika michuano ya Kombe la Kagame baada ya kuifunga Telecom ya Djibout kwa mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi A uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga iliyoanza vibaya mechi za Kundi A kwa kufungwa 2-1 na Gor Mahia ya Kenya, sasa inaweza kwenda robo fainali iwapo itashinda mechi zijazo dhidi ya KMKM na Khartoum N ya Sudan.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na mwamuzi Issa Kagabo wa Rwanda aliyesaidiwa na Lee Okello wa Uganda na Yeatyew Belachew wa Ethiopia, mabao ya Yanga yalifungwa na wachezaji waliosajiliwa mwaka huu na hadi mapumziko walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Malimi Busungu amesajiliwa na Yanga Mei akitokea Mgambo JKT ya Tanga, ambako aliichezea kwa misimu mitatu akitokea Polisi Moro, alifunga mabao mawili, moja katika kila kipindi.
Godfrey Mwashiuya amejiunga na Yanga akitokea timu ya daraja la kwanza ya Kimondo ya mkoani Mbeya, ni chipukizi ambaye ameonesha mwelekeo mzuri katika timu hiyo, aliifunga bao la tatu katika kipindi cha pili.
Yanga iliuanza mchezo huo kwa kasi na alifanya shambulizi la kwanza la nguvu katika dakika ya nane na kupoteza nafasi ya wazi pale Busungu aliposhindwa kuunganisha wavuni krosi iliyochongwa na Haji Mwinyi.
Mrundi Amissi Tambwe aliikosesha Yanga bao jingine katika dakika ya 16 baada ya kupata krosi safi ya Busungu, lakini akashindwa kuutumbukiza wavuni. Baada ya kosakosa za mara kwa mara, Busungu aliifungia Yanga bao la kuongoza katika dakika ya 26 akiunganisha wavuni krosi ya Joseph Zuttah.
Yanga ilikosa penalti mbili katika dakika ya 39 na 45 wakati Tambwe na Msuva waliposhindwa kufunga. Penalti aliyopiga Tambwe ilitokana na Msuva kuangushwa na Marsama Hassan wa Telecom huku ile ya Msuva ikitolewa na mwamuzi baada ya mchezaji mmoja wa Telecom kumcheza vibaya katika eneo la hatari.
Yanga ilikianza kipindi cha pili kwa kuwaingiza Geofrey Mwashiuya na Kpah Sherman, ambao walichukua nafasi ya Tambwe na Msuva, ambao wote walikosa penalti katika kipindi cha kwanza, huku Telecon nao baadaye walimtoa Said Elim na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Said.
Busungu aliendelea kuwa mwiba mkali kwa Telecom baada ya kupachika bao la pili akiunganisha pasi ya chipukizi Mwashiuya. Mwashiuya alifunga bao la tatu kwa shuti kali katika dakika ya 72 kabla mpira huo haujaingia wavuni, uligonga mtambaa panya na kurudi uwanjani na baadae kumgonga kipa Nzokira Jeef na kujaa wavuni.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi tatu huku mkononi ikiwa na mechi mbili dhidi ya KMKM ya Zamzibar, ambayo jana ilifungwa 2-1 Khatoum National Club katika mchezo uliofanyika mapema kwenye Uwanja wa Taifa.
Yanga: Deogratius Munis, Nadir Haroub, Joseph Zuttah, Haji Mwinyi, Kelvin Yonda, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Malimi Busungu na Deus Kaseke.

No comments: