Thursday 2 July 2015

Ajali ya treni, basi yaua watano

WATU watano wamekufa papo hapo na wengine 25 kujeruhiwa kutokana na ajali iliyohusisha basi dogo na treni, eneo la Kibaoni katika kijiji cha Chanzuru nje kidogo ya Mji wa Kilosa mkoani Morogoro.
Ajali hiyo ilitokea saa 1: 30 asubuhi jana ambapo baadhi ya waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Kilosa, mkoani hapa.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Mussa Marambo alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ya basi ndogo, mali ya kampuni ya Huwel.
Alisema gari hilo liligonga treni iliyokuwa ikitokea mjini Morogoro kwenda Dodoma na katika ajali hiyo watu wanne walifariki dunia na wengine 25 kujeruhiwa.
Hata hivyo, alisema eneo hilo lilikuwa na kona kabla ya kuvuka njia ya reli na kutokana na mwendo kasi wa dereva huyo alishindwa kusimama ghafla na kuligonga.
Alisema basi hilo lenye namba za usajili T 837 CTM, aina ya Izuzu Journey likiendeshwa na Bakari Nyange (35), mkazi wa Kilosa na linafanya safari zake kutoka Kijiji cha Tindika, Kilosa na Morogoro mjini na liligonga treni hiyo yenye namba 88U3 iliyokuwa ikiendeshwa na Inea Chipindula (48), mkazi wa Morogoro.
Miongoni mwa watu waliopoteza maisha ni dereva wa basi dogo, Bakari Nyange (35) ambaye alikufa wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Alisema watu wengine waliokufa ni Salehe Gombaye (35), mkazi wa Tindiga Kilosa, Aman Mohamed (35), Mwajili Ally (48) pamoja na Salati Mwajili (7).
Kamanda alisema chanzo cha ajali hilo ni uzembe wa dereva wa basi kukatiza barabara bila kuchukua tahadhari yoyote huku akijua kuwa kuna njia ya treni.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Denis Ngalomba alisema kufuatia ajali hiyo hospitali yake, ilipokea majeruhi 25 kati ya hao, wanaume ni 10 na wanawake 15 ambao wameumia sehemu mbalimbali za miili na wote wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

No comments: