January Makamba afunguka baada ya kukatwa Jina lake
ALIYEKUWA mgombea urais
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) January Makamba, amefunguka na
kuwataka wananchi wasife moyo kwa yeye kuishia nafasi ya tano kwa vile
muda bado upo na kwamba hivi sasa wafanye kampeni za kufa mtu ili John
Magufuli aliyechaguliwa na chama hicho aweze kushinda na kuingia Ikulu.
Akizungumza kwenye
mkutano maalum wa Umoja wa Wanawake wa CCM wilayani hapa, ulioitishwa
kwa ajili ya kuchagua madiwani wa viti maalum, Makamba aliyeomba tena
kuchaguliwa kuwa mbunge katika jimbo la Bumbuli, alisema kwamba
anawashukuru wote waliokuwa wakimuunga mkono hadi kufikia nafasi hiyo
ambayo haikuwa yake, bali ni ya wananchi wa Lushoto waliomlea na
Watanzania wote."Mafanikio niliyoyapata
ya kuingia tano bora si yangu peke yangu ni fahari ya nyie wazazi
wangu, msife moyo wakati bado upo lakini kwa sasa lazima tuhakikishe
ndugu John Pombe Magufuli anakipatia chama chetu ushindi na kuingia
Ikulu," alisema Makamba na kushangiliwa na akina mama hao.
Katika mchakato wa
urais kupitia chama hicho January aliingia hatua ya tano bora pamoja na
Bernad Membe, Amina Salum Ali, Dkt. Asha Rose Migiro na Dkt. Magufuli
aliyeshinda kutoka kundi la watu 38 waliorudisha fomu na kupitia michujo
mbalimbali ya CCM.
Akizungumza katika
mkutano huo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani hapa (MNEC), Dkt.
Najim Msenga, aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kubadilika na kuwachagua
viongozi wanaolingana na January ili kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa
bora kwa viongozi watakaojali maslahi ya wananchi na waondoe watu
wanaofanya 'unafki' kwa wengine.
"Ondoeni zama za
unafiki chagueni watu wanaofaa na ambao wanafanana na January ambaye
hata Rais amemwamini na kumchagua kwenye tano bora wakati wa
kinyang'anyiro cha urais...Lushoto lazima mbadilike msichague kwa
mazoea, chagueni viongozi watakaotusaidia shida zetu," alisema Najim.
Dkt. Najim alisema
kwamba yeye hakuweza kugombea nafasi ya ubunge kama ambavyo baadhi ya
wengi walivyotarajia kutokana na kuridhika na nafasi aliyochaguliwa na
hakutaka kuwa na tamaa ya kugombea ubunge ingawa amekuwa na sifa na
uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi wa Lushoto, amezingatia nafasi
yake ambayo anataka kuonesha uwezo katika kuwatumia kichama.
"Mimi MNEC wenu nina
sifa za kugombea ubunge lakini sikuchukua fomu jimbo lolote maana
mmenipa nafasi hii bado sijawatumikia mkaona uwezo wangu, lakini
nawaeleza hakikisheni mnachagua viongozi watakaoleta maendeleo yetu
msichague mizigo," alisema Dkt. Najim.
Awali Katibu wa CCM wa
wilaya Ramadhani Mahanyu na Katibu wa CCM mkoani Tanga, walipopata
nafasi ya kuwasalimia wajumbe wa mkutano huo, walimsifia Makamba kwamba
kitendo cha kuingia tano bora katika mbio za urais ni cha kujivunia
wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla lakini pia kimeonesha kijana huyo ni
azina kwa chama hicho katika siku za usoni
No comments:
Post a Comment