Mchuano mwingine mkali unatarajiwa kuwapo katika Jimbo la Bunda Mjini ambako Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira atavaana na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya |
Akihutubia katika mkutano wa hadhara
uliofanyikia katika Viwanja vya Stendi ya zamani mjini Bunda jana,
Bulaya alisema wakati chama chake cha zamani kilipogundua mikakati yake
ya kuhamia Chadema, makada wake walimwendea wakimsihi asitoke, bali
abakie ili apatiwe ukuu wa wilaya au uwaziri.
Bulaya
aliyeambatana na Mbunge wa Kahama, James Lembeli ambaye pia alijiunga na
Chadema juzi, alisema baada ya kutafakari kwa muda mrefu uhalisia wa
maisha ya Watanzania hasa wa vijijini na jinsi ambavyo Serikali ya CCM
imekuwa ikiwatendea, aliamua kuachana na ahadi hizo na kujiunga na
Chadema kwa kuwa inalenga kuwakomboa Watanzania. “Ngojeni niwaambie,
niliahidiwa ukuu wa wilaya na uwaziri ilimradi tu nisihame CCM. Lakini
nikaona yote hayo ni upuuzi, bali cha muhimu ni kuwakomboa Watanzania,
nikaachana nayo yote nikaja Chadema,” alisema.
Bulaya
aliyejigamba kukulia na kufanya kazi ndani ya CCM, alisema chama hicho
hakina sera zozote za kuwakomboa Watanzania badala yake kuna za
kuwanufaisha wachache, jambo ambali yeye na Lembeli hawakulitaka.
Bulaya
alitangaza azma yake ya kugombea ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini,
akisema tayari ameshajaza fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho
kugombea nafasi hiyo.
“Niwaambie tu kwamba nimeshajaza
fomu na kuirejesha na kesho (leo) nitashiriki kura za maoni. Inshallaah
Mungu akinisimamisha nitagombea nafasi hiyo na nina uhakika wa
kushinda,” alisema Bulaya.
Akihutubia mkutano huo,
Lembeli aliwataka wakazi wa jimbo hilo kutoipigia kura CCM katika
Uchaguzi Mkuu ujao, badala yake waichague Chadema kwa nafasi zote bila
kumsahau Bulaya kwa ubunge kwa kuwa ni mtu mwadilifu.
Mwenyekiti
wa Bawacha, Halima Mdee akihutubia mkutano huo aliwataka Watanzania
wakubali kula fedha wanazogawa na makada wa CCM ili wachaguliwe kwa
nafasi mbalimbali za urais, ubunge na udiwani lakini kura zote waipatie
Chadema.
No comments:
Post a Comment