Sunday, 26 July 2015

Wiki ya mtikisiko

Mwenekiti wa Chadema Freeman Mbowe akiwahutubiaNi wiki ya mtikisiko. Hivi ndiyo unavyoweza kuelezea hali itakavyokuwa nchini kutokana na matukio makubwa ya kisiasa yanayotazamiwa kutokea ndani ya wiki inayoanza leo ambayo yanaweza kubadili mwelekeo wa siasa za Tanzania.
Hali hiyo inatokana na vuguvugu la kisiasa linalohusisha viongozi wenye ushawishi kuhama vyama vyao vya siasa na kutimkia kwenye vyama vingine, ikiwa ni siku chache kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Ni wiki ambayo itapambwa na matokeo ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi wa CUF kilichofanyika jana mjini Zanzibar kuhusu mustakabali wake ndani ya Ukawa, ikizingatiwa kuwa hivi karibuni chama hicho kiliamua kujiweka kando ya vikao vya umoja huo hadi vikao vya juu viamue.
Hata hivyo, habari ambazo gazeti hili limezipata zinasema kuwa uwezekano wa chama hicho kujitoa ndani ya Ukawa ulikuwa mdogo kutokana na kuogopa hasira za wananchi wenye matumaini na umoja huo.
Aidha, kulikuwa na taarifa kuwa kikao cha jana kilikuwa kinaangalia jinsi watakavyoshiriki katika umoja huo na kwamba kulikuwa na matumaini makubwa.
Vile vile, hii ni wiki ambayo kura za maoni zinazoendelea katika vyama vikubwa vya siasa, kuonyesha baadhi ya vigogo wakiangushwa na kujaribu kutafuta upenyo wa madaraka katika vyama vingine.
Pia, ni wiki ambayo chama kikuu cha upinzani, Chadema kimeamua kusogeza mbele tarehe za kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea urais kutoka jana hadi Ijumaa, katika kile kinachotazamwa kama kusubiri mchakato wa kumpata mgombea urais.
Kana kwamba hiyo haitoshi, hii ni wiki ambayo minong’ono ya waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye jina lake limekatwa katika orodha ya wasaka urais wa CCM anaweza kuhamia Chadema.
Tayari baadhi ya viashiria vya hali hiyo vimeanza kuonekana ambapo wiki iliyopita wabunge wawili wa chama tawala cha CCM, James Lembeli na Ester Bulaya waliachana na chama hicho na kujiunga na Chadema huku chama hicho cha upinzani kikitamba kujiandaa kuwapokea vigogo wengine zaidi.
Kiashiria kingine cha mtikisiko ni hatua ya madiwani 18 wa CCM wilayani Monduli na wengine 10 wa UDP na CCM Bariadi kuhamia Chadema.
Lakini pia wapo wabunge na madiwani wanaohama Chadema kwenda chama cha ACT-Wazalendo.
Vuguvugu hilo la kisiasa limekolezwa na kauli za wanasiasa wawili vijana kwa nyakati tofauti, Godbless Lema na Zitto Kabwe kuwa wiki hii itakuwa ya mshikemshike kutokana na mambo yaliyopangwa kufanyika.
Zitto: Ni wiki ya mabadiliko
Akiandika kwenye kurasa zake za Facebook na Twitter jana, Zitto alisema, “Wiki ya kuanzia Jumatatu tarehe 27 Julai 2015 itashuhudia mabadiliko makubwa sana kwenye siasa za Tanzania. Kuimarika kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ni jambo jema kwa nchi yetu.”
Alipotakiwa kufafanua kauli yake, Zitto hakutaka kutaja matukio husika, lakini alisisitiza kuwa mtikisiko wa kisiasa utatokea na mazingira ya hali hiyo yataanza kubadilika kuanza kesho.
“Na huu ujumbe nilioandika hauna uhusiano na chama cha ACT-Wazalendo,” alisema.
Alipotakiwa kufafanua zaidi, alisema “Watanzania wasubiri mabadiliko ya siasa za Tanzania.”
Lema asema ni mtikisiko
Kwa upande wake Lema, akiwa jimboni kwake Arusha, alisema wiki hii itakuwa ya mtikisiko kwa CCM kwa sababu zaidi ya viongozi wake 950 kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa na taifa watahamia Chadema.
Akizungumza wakati wa kuwapokea vigogo watatu na wanachama 30 kutoka CCM jana, Lema alisema kuanzia kesho kimbunga cha viongozi na wana CCM kuhamia Chadema kitavuma kila kona ya nchi.
Vigogo hao ni Diwani wa Kata ya Moshono, Paul Matthysen na mwenyekiti wa CCM Kata ya Terat, Simon Mollel wote wa jijini Arusha.
Haya yametokea ikiwa ni siku chache baada ya katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Longido, Tostau Mollel kahamia Chadema, huku baadhi ya watiania wa udiwani na ubunge waliokamilisha maandalizi wakikacha kuchukua fomu za chama hicho.
Miongoni mwa waliokacha kuchukua fomu bila kutoa sababu ni mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Arusha, Robinson Meitinyiku, mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, Mathias Manga na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole, wote wakitajwa kuwa kwenye timu ya Lowassa.
“Hii iliyoanzia Bariadi, Monduli, Longido na Arusha mjini ni mvua za rasharasha. Masika yataanza wiki ijayo (kuanzia kesho Jumatatu) kwa zaidi ya viongozi 950 wa ngazi mbalimbali watakapohama CCM na kujiunga Chadema,” alisema Lema.
Alifananisha Chadema na kanisa au msikiti akisema milango yake iko wazi kuwapokea wanachama wa vyama vingine wanaotaka kutumikia umma kujiunga nacho kwa kutubu makosa yao na kusamehewa kabla ya kuingia kazini Oktoba 25, mwaka huu.
Wabunge wanne Chadema watua ACT
Wakati upepo ukivuma kutoka CCM kwenda Chadema, hali kama hiyo imekinufaisha chama kipya cha ACT-Wazalendo baada ya kuvuna wabunge watatu wa viti maalumu na diwani mmoja kwa mpigo kutoka Chadema.
Wabunge hao ni Mhonga Ruhwanya (Kigoma), Chiku Abwao (Iringa ) na AnnaMaryStella Mallac (Mpanda) wote kutoka Chadema, huku mwingine ambaye jina lake tunalihifadhi kwa kuwa hatukumpata, akitimkia CCM.
Wabunge hao wanaungana na Mbunge wa Kasulu mjini, (NCCR – Mageuzi ) Moses Machali aliyehama kutoka NCCR-Mageuzi kwenda ACT Wazalendo, hivi karibuni.
Akizungumza na gazeti hili jana, Zitto alisema atawatangaza wakati wowote wabunge wengine sita kutoka CCM, Chadema na CUF.
Kauli ya Chiku Abwao
Akizungumza kwa simu akiwa India, Abwao alikiri kuhamia ACT-Wazalendo akidai kutoridhisha na mwenendo wa Chadema na hasa taarifa anazosikia za Lowassa ambaye amekuwa akituhumiwa mambo mbalimbali kuhusishwa na Chadema.
“Mimi kwa historia yangu kitu kilichonipeleka upinzani ni kutafuta haki uwajibikaji na kupinga vitendo vya ufisadi na rushwa, lakini nimekishangaa chama changu katika suala hili,” alisema.
“ Licha ya mambo ya sintofahamu yanayoendelea Chadema lakini hili la Lowassa kama kweli atajiunga na chama hiki basi suala litakuwa ni moja tu, ni chaneli ya kuingia Ikulu, lakini haya mambo mimi siyapendi kwa sababu ni mtu wa kupinga ufisadi na kupigania haki za wanyonge,” alisema Abwao
Alisema ameamua kuhamia ACT-Wazalendo, kwa sababu ni chama pekee kitakachowakomboa Watanzania na kwamba ataenda moja kwa moja kugombea jimbo la Iringa Mjini badala ya Isimani.
“Niliamua kwenda Isimani kipindi kile ili kuijenga Chadema, lakini safari hii nipo huku ACT-Wazalendo nitaenda kupambana na Mchungaji (Peter) Msigwa na yeyote yule atakayepitishwa na CCM,” alisema Abwao.
Mhonga: Ni uamuzi tu
Mhonga Rhuwanya alipouliwa alijibu kwa kifupi, “Kama ulivyosikia ndiyo hivyo hivyo, mimi ni mtu mzima na nina maamuzi yangu kwani chama siyo dini.”
Alipoulizwa atagombea ubunge kupitia ACT-Wazalendo, alijibu, “Kwani mtu akihamia chama kingine ni lazima agombea ubunge… hata hivyo naweza kugombea tena.”
Mallac aenda kupokewa
Kwa upande wake, Mallac alisema alikuwa safarini kwenda Katavi kupokewa ACT-Wazalendo.
“Niko njiani naelekea Katavi mkoani kwangu kupokewa rasmi na kiongozi wangu wa chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe,” uliosomeka ujumbe mfupi wa maneno.
Zitto awapokea
Zitto alisema huo ni mwendelezo wa chama hicho kuwapokea wabunge kutoka katika vyama mbalimbali na hivi karibuni atawapokea wengine katika mikoa ya Kagera, Tabora, Rukwa na Zanzibar.
“Tabora wako wawili na Kagera mbunge mmoja wote wa CCM, kutoka wilaya ya Karagwe, pia Zanzibar wawili kutoka CUF na Chadema. Hawa wote wanasubiri mchakato wa kura za maoni umalizike ndipo tuwatangaze.
“Hawa wabunge tuliowapokea ni sawa na asilimia 10 kati ya 50 niliosema, maana watu walikuwa wananiuliza, ‘Zitto ulisema utawapokea wa kiasi kadhaa mbona kimyaa?’ mambo ndiyo yameanza sasa.”
Diwani Chadema atua ACT
Katika hatua nyingine, aliyekuwa diwani wa Kata ya Segerea (Chadema), Azuri Mwambagi amejiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ya uhusiano mbaya kati yake na viongozi wa Chadema wa jimbo hilo.
Mwambagi alisema kuwa amekuwa diwani wa kata hiyo kwa miaka mitano lakini hakukuwa na ushirikiano mzuri kati yake na uongozi wa jimbo hilo.
“Kila ninachokifanya wenzangu wanasema sijafanya kitu na wanaamua kunizunguka kwa wananchi, hali hii imenichosha,” alisema Mwambagi.
Katibu wa jimbo hilo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Anna alisema hata yeye amezisikia taarifa za diwani huyo kuhamia ACT- Wazalendo, lakini akakana kuwapo mizengwe aliyofanyiwa Mwambagi.
“Tupo katika mchakato wa kura za maoni na yeye ameomba kuteuliwa kugombea udiwani Kata mpya ya Liwiti, kama anahisi alikuwa kiongozi bora enzi za utawala wake kwa nini asisubiri matokeo ya kura za maoni ndipo afanye uamuzi huo?” alihoji Anna.

CHANZO: MWANANCHI 

No comments: