Monday, 12 May 2014

Sudan Kusini yaahirisha uchaguzi mkuu


Wananchi wa Sudan Kusini wanaishi katika mazingira ya kusikitisha huku vita vikiendelea
Sudan Kusini imeahirisha uchaguzi wake uliotarajiwa kufanyika mwaka ujao ili kutoa fursa kwa pande zinazozozana kuweza kufikia makubaliano ya amani.
Kauli hii imetolewa na Rais Salva Kiir.
Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar walitia saini mkataba wa Amani siku ya Ijumaa kwa lengo la kumaliza vita vilivyozuka Disemba mwaka jana.
Alisema kuwa serikali ya muda itaendesha shughuli za serikali hadi uchaguzi utakapofanyika mwaka 2017 au 2018.
Salva Kiir alitia saini mkataba wa amani na hasimu wake Riek Machar Ijumaa wiki jana
Maelfu ya watu wameuawa na wengine kutoroka makwako baada ya kushambuliwa.
Bwana Machar ametuhumu serikali kwa kukiuka mkataba wa Amani na kushambulia waasi.
Umoja wa Mataifa hata hivyo umetuhumu pande zote katika mgogoro huo kwa kukiuka haki za binadamu na kutenda uhalifu kama vile mauaji na ubakaji.
Sudan Kusini ndio taifa la hivi karibuni duniani kupata uhuru wake mwaka 2011 baada ya kujitenga na Sudan.
Mapigano yalizuka Disemba mwaka jana baada ya Rais Kiir kumfuta kazi Riek Machar aliyekuwa makamu wake wa Rais Riek Machar kufuatia madai kuwa alipanga njama ya kupindua serikali.

No comments: